SMZ haijakosea kufuatilia wanaohujumu mahujaji

Muktasari:

Inapotokea kiongozi wa msikiti, kanisa, hekalu au kikundi cha watu wanaoshughulikia masuala ya dini wanafanya mambo yenye sura au harufu ya uhalifu au hadaa wanajamii hushangaa.

Katika jamii nyingi viongozi wa dini na wote wanaotumikia taasisi zinazohusika na masuala ya ibada hutegemewa kuwa mfano mzuri wa utu na uadilifu kwa watu wengine.

Inapotokea kiongozi wa msikiti, kanisa, hekalu au kikundi cha watu wanaoshughulikia masuala ya dini wanafanya mambo yenye sura au harufu ya uhalifu au hadaa wanajamii hushangaa.

Hii ni kwa sababu watu waliomo katika kundi hili hutegemewa kuwa waadilifu na kuwa mbali na maovu ya aina hii.

Kwa bahati mbaya hapa kwetu, tumeshuhudia mara nyingi katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya viongozi hawa na wasaidizi wao wakijihusisha na hadaa, wizi na utapeli.

Matukio haya yamehusisha hata safari muhimu kuliko zote zinazofanywa na waumini wa dini ya Kiislamu katika maisha yao.

Hii ni safari kwenda kufanya ibada ya hijja katika mji mtukuufu kwa Waislamu, Makkah nchini Saudi Arabia.

Karibu kila mwaka kila inapofanyika ziara hii tukufu utaona mahujaji wengi wanakwama viwanja vya ndege na safari zao kuvunjika.

Wengine hufanyiwa hadaa ya kutozwa malipo makubwa ya nauli, kupandishiwa kiujanja malipo ya viza, ada za makazi wanapokuwa Makkah na Madina na gharama nyinginezo huko Saudi Arabia.

Wakati mmoja palisikika madai ya hata wafanyakazi wa Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar waliopo katika idara inayohusika na masuala ya Kiislamu, kuwaibia fedha mahujaji.

Ukichunguza utaona waziwazi kwamba baadhi ya watu wanaojifanya waumini waadilifu wa dini ya Kiislamu wamezigeuza hizi safari za kila mwaka za watu kwenda kufanya ibada ya hijja kuwa ni kitega uchumi. Kwa kweli hii ni hatari kubwa ambayo haistahiki kuvumiliwa hata kidogo.

Kutokana na kuwepo mwenendo huu mbaya hivi karibuni yamesikika maombi ya viongozi wa serikali na taasisi za dini ya Kiislamu ya kuwataka wale wote wanaohusika na kusafirisha mahujaji kuachana na ubabishaji na udanganyifu.

Kwa hakika jamii yoyote ile yenye waumini wa kweli wa dini haiwezi kuvumilia uchafu wa aina hii unaofanywa na hawa madalali feki wa hizi safari za hijja.

Ukichunguza utagundua kuwa wengi wa hawa mahujaji hujinyima raha za dunia na hata kubana matumizi muhimu ya chakula na mavazi kwa miaka kadhaa ili waifanye safari ya hijja ambayo ni moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu.

Lakini, wakati wakiwa wameshajitayarisha na hata kuaga familia zao, ndugu na marafiki kwa hii safari, wanatokea watu kuivunja au kuichafua katika hatua za mwisho.

Haiwezekani vyombo vya sheria vinahusika zaidi na wezi wadogo au wanaotukana au kupigana katika kumbi za dansi na rusha roho, lakini wanawafumbia macho matapeli wa safari za hijja.

Ni muhimu kuzichunguza taasisi zote zinazohusika na safari za hijja wakiwamo watendaji wake.

Lakini, lilio muhimu ni kuhakikisha kila anayehusika kuwahadaa mahujaji ashughulikiwe na vyombo vya sheria.

Pia, uwepo mpango madhubuti wa kuratibu na kutathmini shughuli zao, hasa baada ya kufanyika safari ya hijja.

Ushauri kwa Serikali

Moja ya njia inayoweza kusaidia ni kuwepo kwa fomu maalumu za tathmini ya safari zitakazojazwa kwa usiri na kila mtu aliyefanya safari ya hijja.

Katika fomu hizi mahujaji atakiwe kueleza gharama zote walizotozwa, matayarisho ya safari, hali ya safari na malazi ilikuwaje walipokuwa Saudi Arabia na yale yote yaliyowaridhisha au kuwasikitisha.

Vilevile maofisa wetu wa ubalozi waliopo Saudi Arabia watumiwe kufuatilia hali ya watu wanaokwenda hijja na badaye watume ripoti itakayoeleza yale yote waliyoyagundua kwa vikundi mbalimbali vilivyo simamia safari ya hijja.

Mpango huu itasaidia sana kupata undani wa mipango na mwenendo wa watu wote wanaohusika na kuwasafirisha mahujaji.

Ni kwa kuelewa tu kwamba mwenendo wao unafuatiliwa kwa karibu na wanaofanya utapeli wanashughulikiwa kisheria ili watakaopanga safari hizo wawe na uhakika watasafiri salama na kwa uaminifu.

Sheria zitakapochukua mkondo wake zitasaidia kupunguza na hata kumaliza kabisa vitendo visivyo vya haki dhidi ya wanaofanya safari za hijja.

Ushauri wangu vyombo vya sheria vianze mchakato wa kulishughulikia kwa amani suala hili linaloitia aibu nchi, hasa kutokana na vitendo hivyo kufanyiwa watu ambao wamo katika ibada.

Kama kuwapa onyo watu hawa basi hili limeshafanyika mara nyingi na kwa upole na sasa tuseme basi na tuziachie sheria za nchi kufuata mkondo wake.

Ni kweli siku hizi ujambazi wa aina mbalimbali wa akili, kalamu na silaha upo kila pahala, lakini hili la safari za hijja ni uhalifu mkubwa zaidi.

Tusikubali tena kuridhia uhalifu wa aina hii. Tuwatendee haki wanaokwenda safari za ibada ya hijja, kwani wengi wao wanazipata fedha kwa taabu na wengine kudunduliza kwa muda mrefu.