SOKA YA KULIPWA Sikia hii Watanzania wanaopasua anga za kimataifa

Muktasari:

  • Ni wazi kuwa zama zimebadilika, awali kulikuwa na uhaba wa wachezaji wa kimataifa ambao wamekuwa na manufaa makubwa kwenye mataifa yanayo fanya vizuri katika mabara yote duniani.

Japo sio kama ilivyo kwa mataifa ya Afrika Magharibi yalivyo na nyota wengi wa kimataifa, kipindi hiki Watanzania nao wanaweza kujivunia kwa kuwa na nyota kadhaa wa kimataifa ambao wanafanya vizuri kwenye mataifa mbalimbali.

Ni wazi kuwa zama zimebadilika, awali kulikuwa na uhaba wa wachezaji wa kimataifa ambao wamekuwa na manufaa makubwa kwenye mataifa yanayo fanya vizuri katika mabara yote duniani.

Mabingwa wa Kombe la Dunia, Ujerumani pamoja na ligi yao ya Bundesliga kuwa bora lakini wamekuwa na utaratibu wa kuwaita nyota wake wote muhimu wanaocheza soka la kimataifa nje ya Ujerumani kama Mesut Özil wa Arsenal (Uingereza), Toni Kroos wa Real Madrid (Hispania) na wengine kibao.

Nyota wa kimataifa wanaaminika kuwa uwezo wa ziada kwenye vikosi vingi vya timu za Taifa kutokana na namna walivyojengeka kiushindani hasa kwa wale ambao wanacheza kwenye ligi zilizoendelea.

Spoti Mikiki inakuletea nyota wa Kitanzania wanaofanya vizuri kwenye ligi mbalimbali kuanzia Ulaya na yupo Mbwana Samatta hadi Afrika kwenye mataifa kama Morocco, Afrika Kusini, Kenya na mengineyo.

Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji)

Kuna kipindi Samatta (24) alikuwa ameandamwa na ukata wa mabao na kuandamwa kwake na ukata huo kwa kiasi fulani uliifanya timu yake ya Genk kuyumba kwa kushindwa kupata matokeo ya ushindi kwenye michezo mfululizo.

Urejeo wa mshambuliaji huyo kwenye makali yake baada ya siku 72 bila bao ambazo ni sawa na miezi miwili tuliona namna alivyofunga kwenye mchezo uliopita dhidi ya Club Brugge, tuachane na huu ambao wamecheza na Kortrijk, ugenini.

Kabla ya mchezo huo ambao Samatta alifunga bao la pili kwenye ushindi wa 2-0 pia alitengeneza bao kwenye mchezo wa nyuma yake ambao waliifunga Anderlecht, ugenini kwa bao 1-0.

Makali ya Samatta yameifanya timu yake kwa mara ya kwanza kushinda michezo mfululizo kuanzia huo ambao alitengeneza dhidi ya Anderlecht na ambao alifunga na Club Brugge.

Michael J. Lema (Sturm Graz/Austria)

Kinda Lema (18) anayechipukia kwenye kikosi cha Sturm Graz alipandishwa na ilikuwa aweke rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya awali.

Kwa bahati mbaya hakupata nafasi ya kucheza kwenye mechi zote mbili na kuishia kushudia kwenye benchi la wachezaji wa akiba timu yake ikiondoshwa kwenye mashindano hayo na Fenerbahçe ya Uturuki kwa jumla ya mabao 3-2.

Majeruhi yalimfanya kinda huyo kurudishwa kwenye kikosi B ili kutafuta ufiti kabla kuendelea na ratiba ya kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambayo imekuwa na mwenendo mzuri kwenye ligi.

“Nacheza kikosi cha vijana ambacho kipo madaraja ya chini sijui lini wataona nimeshakuwa fiti ili nirejee kikosi cha kwanza, majeruhi yameniharibia kwa sababu ndiyo kwanza nilikuwa nimepandishwa.

“Sikupata hata muda wa kucheza mechi japo moja ila ninaamini mambo yatakuwa sawa, ni kiasi cha muda tu,” anasema Lema kutoka Austria.

Farid Mussa (CD Tenerife/Hispania)

Farid (21) bado hajawa kwenye kikosi cha kwanza CD Tenerife ambayo inacheza Ligi Daraja la Kwanza Hispania maarufu kama Segunda, kuna kipindi kulikuwa na tatizo la kupata kibali cha kucheza ligi hiyo hasa baada ya kudaiwa kupandishwa kikosi cha kwanza.

Mambo yanaonekuwa kutokuwa mazuri kwa winga hiyo wa zamani wa Azam kwa sababu amesalia kwenye kikosi B cha timu hiyo ambacho kinacheza daraja la nne Hispania kama sehemu ya kuwajenga wachezaji kiushindani kabla ya kupandishwa vikosi vya kwanza.

Mataifa mengi ya Ulaya yamekuwa na utaratibu huo ambao umekuwa pia ukiwasaidia hasa vijana wao kwa kupata muda wa mwingi wa kucheza.

Orgeness Mollel (FC Famalicão/Ureno)

Mwanzoni mwa msimu wa 2017/2018, Mollel (19) alipandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha Famalicão, kutokana na kutopata kwake nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza ilibidi atolewe kwa mkopo na kwenda AD Ninense.

Kwa sasa winga huyo wa kulia yupo AD Ninense, amekuwa na wakati mzuri akiwa na timu yake hiyo ambayo kwa mujibu wa kipingele kilichopo kwenye mkataba wake inawezekana kwa gharama za fedha za Kitanzania ambazo ni sawa na Sh68milioni.

Albert Mandari (ASF/Ukraine)

Mandari (23) alivunja mkataba wake na PFC Nyva Ternopil ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Ukraine, yote hiyo inadaiwa kuchangiwa na anguko la kiuchumi la timu hiyo hivyo ilibidi wachezaji wote kupunguziwa mishahara yao.

“Sikuwa tayari na kuamua kuvunja mkataba, nipo kwenye kituo cha ASF ambacho kipo chini ya Wahispania nimeomba nafasi ya kuwa nafanya nao mazoezi ili kujiweka fiti, ningepata timu ila kibaya kipindi cha usajili kilikuwa kimepita.

“Mpaka sasa nina ofa mbona ya kujiunga na timu ya Ligi Kuu Ukraine, Olympic Donetsk na mkataba wa awali nimeshasaini nasubiri dirisha la usajili lifunguliwe ili niingie nao makataba rasmi,” anasema Mandari.

Hata hivyo kiungo huyo amekuwa akipata nafasi ya kucheza michezo ya kirafiki na kituo hicho ambacho na chenyewe kimejiingiza kwenye dili la Mtanzania huyo ili kiweze kunufaika kwa mauzo yake.

Martin Tangazi (Gazişehir Gaziantep FK/Uturuki)

Moja ya nyota wa Kitanzania ambaye naye ni zao la kituo cha Aspire. Martin (19) yupo Uturuki anacheza soka kwenye kikosi B cha Gaziantep.

Kinda hilo limekuwa likitajwa kuwa na uwezo mzuri wa kuutumia mguu wake wa kushoto kwa kucheza kama beki/mshambuliaji wa kushoto.

Gazişehir Gaziantep FK ipo kwenye mazingira mazuri ya kupanda daraja hivyo huenda mchezaji huyo wa Kitanzania akaanza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza wakati ikiwa ligi kuu.

Saimon Msuva (Difaâ Hassani El Jadidi/Morocco)

Wamorocco wanamfananisha Msuva na Mane wa Liverpool kutokana na kasi aliyonayo na uwezo wa kufunga mabao,tangu atoke Yanga na kujiunga na Difaâ amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho chenye maskani yake mjini El Jadidi.

Msuva alikuwa chachu ya Difaâ kusonga mbele kwenye robo fainali ya Kombe la Mfalme ‘Coupe du Trone’, kama si uwezo wake binafsi wa kutengeneza na kufunga huenda wasingetinga hatua hiyo.

Difaâ ilipoteza ugenini na wenyeji Chabab Rif Hoceima kwa mabao 2-1, Msuva ndiye alifunga bao lao ambalo liliwafanya kuwa na matumaini ya kupindua matokeo, kwenye mchezo wa marudiano ambao walishinda 2-0 alipika bao la pili.

Uwezekano wa kutinga hatua ya fainali ni mkubwa kwa timu ya Msuva kutokana na mwanzo wao kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza ugenini walitoshana nguvu ya bila kufungana 0-0 na RSB Berkane.

Kwa mujibu wa ratiba ya kombe hilo la mfalme watakuwa nyumbani Jumanne ya Oktoba 31 kumalizia mchezo wa nusu fainali ya pili, ushindi wa namna yoyote utawafanya kutinga fainali ambapo wanaweza kucheza na mshindi jumla kati ya Raja Casablanca au FAR Rabat.

Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini)

Banda (22) amekuwa ni kama nguzo kwenye timu ya Baroka ambayo inashiriki Ligi Kuu Afrika Kusini ‘PSL’ kwenye sehemu ya ulinzi.

Baroka ikiwa na Banda ilicheza michezo nane bila ya kupoteza mpaka pale ambapo Bidvest Wits ilipovunja rekodi hiyo kwenye mchezo wa tisa kwa kuwafunga nyumbani bao 1-0.

Elias Maguri (Dhofar/Oman)

Japo amekuwa hafungi mara kwa mara lakini amekuwa sehemu ya msaada mkubwa kwa Dhofar kuwa nafasi ya kwenye msimamo wa ligi hiyo ambayo ina jumla ya timu 14.

Salum Shebe (Al-Midhaibi/Oman)

Sio kazi nyepesi kujinasua kutoka nafasi ya mwisho kwenye msimamo hadi nafasi ambazo zinamfanya Shebe na timu yake hiyo ngeni Ligi Kuu Oman wapumue.

“Kushinda michezo mfululizo kumetusaidia ilikuwa tupo kwenye hali mbaya hasa baada ya kufungwa michezo mingi ya mwanzoni mwa msimu,”anasema Shebe.

Abdul Hilal (Tusker/Kenya)

Hilal amesimama kwa niaba ya Watanzania wengine wanaocheza Ligi Kuu Kenya kama Aman Kyata wa Chemelil Sugar F.C., Himis Abdallah wa Sony Sugar na wengine kibao.

“Ligi ipo ukingoni, zimebaki mechi 3 kabla ya kumalizika kwa msimu, tulikuwa kwenye mazingira mazuri ya kuchukua ubingwa lakini imeshindikana kwa sababu hata kama tukishinda michezo iliyosalia hatuwezi kufikia pointi za Gor Mahia.

“Gor Mahia ndiyo mabingwa, wenzagu wakina Aman na Hamis timu zao hazipo kwenye nafasi mbaya kwenye msimamo,binafsi namshukuru Mungu hata kama tumekosa kuwa mabingwa, tutamaliza kwenye nafasi ya pili,” anasema Hilal.