Saa tatu asubuhi tu, uwanja ‘nyomi’

Muktasari:

Kuna waliotembea kwa miguu, waliopanda bodaboda mbali na hao, wapo waliokwenda na magari yao binafsi, yote ni kwa ajili ya ofa iliyotangazwa na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.

Saa 12 asubuhi, daladala zinakatiza ruti kwenda Uwanja wa Taifa kutoka kona mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.

Kuna waliotembea kwa miguu, waliopanda bodaboda mbali na hao, wapo waliokwenda na magari yao binafsi, yote ni kwa ajili ya ofa iliyotangazwa na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.

TFF ilipanga kufunga milango saa 5:00 asubuhi, lakini Msemaji wake, Alfred Lucas anasema, wamelazimika kufungua milango saa 3:00 baada ya umati kujaa nje ya uwanja

Baadhi ya waliofika uwanjani, hawakupata hata nafasi, waliishia kupigwa mabomu, kumwagiwa maji ya kuwasha, kupata kashkash za polisi. Waliokuwa ndani ni wengi na walikuwa nje walikuwa wengi zaidi.

Uwanjani na katika mitandao ya kijamii, kulikuwa na mijadala mirefu kuwa kujaa mashabiki 57,000 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 5:40 asubuhi milango ilipofungwa kuna maanisha nini?

Baadhi walidai kuwa ni ishara kuwa maelfu hawana kazi na kukubali kupoteza muda mwingi uwanjani, wengine walidai sekta binafsi mtu hujiamulia afanye nini kwa kuwa habanwi.

Wengine walifunga kwa muda shughuli zao kwa kuwa Yanga na TP Mazembe haitajirudia.

Mijadala ya uwanjani na mitandaoni ilisema pia kuwa wengine walikuwa uwanjani kwa kazi zao wanatakiwa wawapo, wengine walikuwa shifti za usiku kwa hiyo wanapata muda wa kuangalia mpira na wengine waliweka watu kuwashikia kazi katika sehemu zao za kazi. Hiyo yote ni kutokana na mahaba, ushabiki. Sasa, kundi lingine ni la wanafunzi kuwa wengi wamefunga shule na kwamba ilikuwa nafasi kwao wakati kundi lingine ni la wasiokuwa na kazi.

Hawa inaelezwa kuwa ni wengi na zaidi ilionekana kwa mwonekano wao wakiwamo mateja.

Spoti Mikiki ilifanya mahojiano na watu mbalimbali kwa hali hiyo:-

Wasemavyo Mashabiki

Suzy Shoo, anasema kitendo cha mashabiki kujaa uwanjani kuanzia saa 3:00 asubuhi, ni kutokana na ofa ya kuingia bure uwanjani, pia waliyowahi ni wale wasiyo na kazi kwa wenye majukumu wamezuiwa baada ya kuchelewa kuweka sawa majukumu yao. “Licha ya mwenyekiti Yusuf Manji, kuwa mzalendo kwa wapenzi wa Yanga, lakini cha kusikitisha wale wanasoka na mashabiki wa kweli wamekosa kuuona mchezo kwani walipochelewa walizuiliwa uwanjani kutokana na uwanja kujaa, hivyo wamekuwa na manung’uniko,” anasema.

Shabiki mwingine, Mussa Kilasi anasema: “Ofa ya Manji siyo sababu ya watu kujaa mapema uwanjani anachoona ni mashabiki wa Yanga kupenda timu yao hasa kwa kipindi hiki ambacho ipo kwenye kiwango cha hali ya juu, hivyo hata wangetaja viingilio bado uwanja ungejaa.

“Nimefika saa 4:00 asubuhi, siyo kweli kwamba ofa ndiyo sababu nadhani mashabiki wanaendana na upepo wa timu yao kuwa kwenye uwezo wa juu, hivyo ofa haina nafasi,” anasema.

Salehe Kaitani anasema kujaa kwa mashabiki mapema ni kwamba wengi wanataka kuwashangaa TP Mazembe na mastaa ambao wanawasikia tu kwenye vyombo vya habari.

“TP Mazembe tu hapa na ndiyo sababu ya watu kujaa mapema, hata kama kungekuwa na kiingilio, nakwambia watu wangejaa ukichukulia imemtoa Mbwana Samatta ambaye ana mafanikio makubwa kisoka na ndiyo maana wengi wamesitisha shughuli zao,” anasema.

Anasema pia kuwa bure waliyoipata, imetoa mwanya kwa vibaka kuja kutumia fursa hiyo na siyo kutazama mechi.

“Tunawajua wanaopenda soka na wale mashabiki wa kweli wa Yanga, wengi ni vibaka tumejikuta tukiwa na kazi ngumu ya kulinda usalama na mali za raia ambao wamefika uwanjani kutazama mechi hiyo,” anasema.

Sylvester’s Boats alishauri endapo ikitokea kuchezwa mechi kubwa kama hiyo, haifai bure kwa ajili ya usalama wa watu na pia kulinda heshima mbele ya wageni kuona Tanzania kuna vitu vya ajabu.

Hata hivyo anasema mashabiki kujaa mapema wengi walikuja kuwashangaa mastaa na kuwanyima fursa wapenzi wa kweli wa Yanga, kuisapoti timu yao.

“Sioni ajabu uwanja kujaa ila ajabu umejaa mapema, kwani hata mechi ya Simba na Yanga, wanajaa kutokana na ushindani wa timu hizo ila siyo mapema kama ilivyo sasa inaonyesha watu wengi hawana kazi mjini na ndiyo maana walifika asubuhi na kusubiri hadi saa 3:00” anasema.

Sefu Hamis Chuma anasema binadamu wanapenda vitu vya bure na ndiyo maana wameacha kazi na kupoteza muda kusubiri kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi 10:00 jioni muda wa mechi na akasema wakati mwingine vya bure vina karaha. “Siku zote vya bure vina karaha na ndiyo maana mabomu yanarindima kutokana na watu wanapenda mteremko lakini wengeweka kiingilia usingesikia hayo mabomu,” anasema.

Simon Magawa anasema watu kujaa mapema ni mapenzi yao kwa Yanga na wamejua wanacheza na timu kubwa yenye mafanikio na imemtoa Mbwana Samatta, kucheza Ulaya. “Hakuna ambaye hakutaka kuishuhudia Yanga, inapoweka historia ya kucheza na TP Mazembe hata wangeweka kiingilio watu wangeingia mapema kuwahi nafasi za kukaa ili wakiangalia mechi wasipate usumbufu,” anasema.

Mlema Samson: “Ikumbukwe TP Mazembe ina mafanikio, wengi walikuwa na hamu ya kuwashuhudia nyota wa kikosi hicho bila kusimuliwa.”

Matondon Laurent; “Mazembe ni sababu kubwa kwani ingecheza Yanga na Majimaji, hata wangesema bure sidhani kama ingefikia hapa na watu kuondoka kwa manung’uniko kutokana na kukosa nafasi.”

Satana Kuboma anasema, bure imewavuta hata wasiopenda kuja mpirani na hii kumechochea zaidi na wale wasiyopenda kufika uwanjani kuja mapema.

Shabiki mwingine, Temeck Sanga ‘Bilionea’: “Ninadhani wangeandaa utaratibu mapema na siyo ghafla kama ilivyo, kwanza wangeanza na mechi za kawaida wangekuwa na tiketi mbili za kiingilio na za bure kwa ajili ya mechi ya TP Mazembe, hiyo ingewapa urahisi wale Wanayanga wa kweli kutopata usumbufu kama ule,” anasema.

Masho Bavuna ‘George’: “wasingefanya bure angalau kungekuwa na kiingilio cha chini kuliko walichokifanya.”

“Kama ningekutana na Manji leo (wiki iliyopita), ningemshauri hii asiifanye tena, watu walipe japo Sh2,000,” anasema Abdallah Majura, mmoja wa waandishi wakongwe wa habari na mmiliki wa Radio BM iliyopo mkoani Dodoma.

Hata wasomi walichangia yao

Profesa Benedict Mongula kutoka Taasisi ya Masomo ya Maendeleo (IDS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, UDSM anasema: “Wengine wanafanya kazi binafsi siyo waajiriwa wa Serikali, hivyo wanajipangilia kazi zao, hilo linakuwa gumu kujua ni wangapi wanaweza kuathiri uchumi wa taifa…ingawa sioni kama kuna shida umati wa watu kujaa uwanjani naona kama wamepata muda wa kuburudika.”

Profesa Mongula alimuunga mkono Mwenyekiti wa Yanga, Manji kwamba amefanya jambo la msingi kuwapa nafasi wale ambao walikuwa hawana uwezo kiuchumi kwani imewasaidia kubadili mazingira

“Kuna wengine walikuwa hawana uwezo wa kulipia tiketi, lakini kitendo cha kuwafanya waingie bure amewapa raha kujiona wanathamani japokuwa si wote.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana anasema: “ikumbukwe kuwa mechi hiyo imechezwa jijini Dar es Salaam, ambako kuna watu wengi ambao hawana kazi maalumu, hivyo kwenda kujitokeza kwa wingi taifa siku ya juzi Jumanne, hakuwezi kuleta madhara makubwa.

“Ingekuwa ni tukio la kila wiki, ingekuwa mbaya, lakini kwa jinsi ambavyo hili jiji lina watu ambao hawana kazi zinazoeleweka, imewasaidia kwenda kubadilisha mazingira na wengine ndoto zao kufufuka upya pindi wanapoona wengine wamefanikiwa,” anasema.

Dk Bana anaeleza kwamba hata mataifa ya Ulaya kuna matukio ambayo husimamisha kazi kwa ajili ya tukio maalumu, huku akisema TP Mazembe ni timu kubwa ambayo ni kama tukio la hatua la kukua kwa soka nchini. “Wana haki ya kwenda, lilikuwa tukio kubwa, ingawa lazima kuna nguvu ya kiuchumi itakuwa imeyumba kwa wale wenye ajira zao,” anasema.