Sababu tano za wanaume wengi wanatamani tendo la ndoa tu na sio kuoa

Muktasari:

  • Wanasema wanaume wamepoteza moyo wa dhati wa kuwapo kwenye uhusiano. Wanaonekana kama hawana mapenzi tena, wao kila siku ni kuuliza tu tendo la ndoa, na kama halipati basi anaweza kuondoka muda wowote kuelekea huko anakolipata.

Wanawake wengi wanalalamika namna wanaume walivyo kwenye uhusiano. Wanasema wanaume wamepoteza moyo wa dhati wa kuwapo kwenye uhusiano. Wanaonekana kama hawana mapenzi tena, wao kila siku ni kuuliza tu tendo la ndoa, na kama halipati basi anaweza kuondoka muda wowote kuelekea huko anakolipata.

Hali hii inasumbua uhusiano na uchumba wa wengi na wengine wamelazimika kuvunja uchumba wakiwa karibia kuingia kwenye ndoa. Wanawake hawa wanalalamika wakisema wako wapi wale wanaume wenye kiu ya ndoa? Wako wapi wale wanaume wenye kuongelea kutaka kuoa na kuanza familia na kuwapenda watoto wao?

Wako wapi wale wanaume wenye kiu ya mafanikio na kudumisha maisha pamoja na wake zao, mbona kama wamemalizika na waliobaki wana kiu za kula bata tu na kufanya mapenzi pasipo kumaanisha.

Yamkini na wewe unayesoma makala hii unajiuliza maswali haya pia. Wanawake wengine wamekuwa wakinieleza kuwa wanaume waliobaki siku hizi ni wavivu, hawana hamasa ya maendeleo, atakuwa na wewe kama ana uhakika wa tendo la ndoa tu. Leo nimekuja kuzungumza na wasichana na wanawake ambao nao wana mawazo na maswali kama haya, ni kweli vilio na malalamiko yenu ni ya kweli na tunasikitika pamoja kwenye hili lakini pia tafiti zinasema iko sababu ya hali hii.

Ni vyema mkafahamu kuwa kwa kiasi kikubwa mifumo au mbinu za mchezo wa mahusiano zimebadilika sana, nadharia za zamani nazo zinaonekana kubadilika na hii imewafanya wanaume wengi kubasili aina ya maisha yao.

Fuatilia sababu zifuatazo ili kulielewa hili sawia. Kumbuka kuwa sababu hizi zimetokana na majibu ya wanaume wengi kwenye tafiti;

Mgawanyo wa majukumu baina ya wanaume na wanawake umeingia doa

Wanaume wa kawaida hupenda kufanya kazi ili kujitafutia kipato chao na familia, na wakitoka kazini au kwenye majukumu yao ya kila siku wanataka kupumzika na kufanya kile wanachojisikia kufanya iwe ni kulala, kuangalia televisheni, kusikiliza redio.

Sio kukimbizana na vijishuhuli vya nyumbani kama vile kusaidia kupika, kusafisha vitu, kukaa na watoto na kazi nyingine ambazo wao wanaona sio zao.

Ndani yao wana kiu ya kuona wapenzi wao wanawakaribisha kwa upendo, kuwaandalia maji, kuwasaidia kuweka mazingira ya wao kupumzisha akili na mwili baada ya kula chakula, wanakiu ya kuona tabasamu, sauti nzuri, na ikiwezekana kupata penzi. Kwao hali hii kuwapa nguvu tayari kuwaandaa na siku nyingine ya kesho.

Tatizo linakuja pale mwanaume huyu anajikuta ameoa mwanamke mfanyakazi au mwenye majukumu mengi yamkini kumzidi hata mume, akikaa, akilala anawaza kazi, anawaza biashara anawaza miradi na vingine vingi, akirudi nyumbani mwanamke huyu anakuja amechoka na hajiwezi kimwili na kiakili kama vile vile alivyo mume wake, mke na mume wote wamechoka sana, mke na mume wote wana msongo wa mawazo na wanahitaji kupepewa maana hawajiwezi kwa kuchoka.

Mwanamke amechoka hana hamasa ya kufanya kazi ndogondogo za nyumbani au hata kuwashuhulikia watoto. Ulimwengu wa kazi na majukumu umeshamfanya mwanamke kuwa na misuli ya kukimbizana na maisha kama mwanaume.

Hali hii inawafanya wote wawili wanarudi nyumbani wamechoka kabisa na kila mmoja anauhitaji wa msaada wamwenzake wakati hakuna aliyetayari wala aliyena nguvu ya kumsaidia mwenzake.

Katika hali kama hizi vijihasira na vihisia hasi huamka kwa urahisi sana na magonvi huweza kupenye hapohapo. Ule uwiano wa masaidiano umeshapotea na kilichoota ni hatari sana kwa mahusiano ya wawili hawa.

Wachunguzi wanasema ndio maana zipo jamii na imani fulani ambazo mke huachwa nyumbani akimsubiri mume wake na mume kazi yake ni kuhakikisha anafanya kila jitihada kuilisha na kuitunza familia, sio kwamba hawataki mke afanye majukumu ya baba la hasha, wanamuandaa kuweza kumhudumia mumewe vilivyo.

Najua hoja za wengi pia zina mashiko kwamba wanawake wengine wangependa kukaa ka kuwasubiria waume zao ili wawaenzi lakini wanaume wengine wameshindwa kubeba majukumu yao kama wanaume na viongozi wa familia na hiyo imewalazimu wanawake kusimama na kufunga mkanda. Pamoja na hayo hali ya masumbufu haijapungua.