Sababu za kukosekana walimu wa sayansi

Kutokuwapo kwa mazingira bora ya kufundisha na ujifunzaji shuleni, ni moja ya sababu ya Tanzania kuwa na idadi ndogo ya walimu wa masomo ya sayansi. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Maelezo zaidi ya sera hiyo yanasema kuwa katika wanafunzi wanaosoma sekondari nchini, 30 hadi 35 kati ya 100 ndiyo wanaosoma masomo ya sayansi wakiwa kidato cha tatu na nne.
  • Idadi hii ya wanafunzi ndiyo inayotegemewa kusomea kozi za sayansi na teknolojia katika vyuo na taasisi za elimu ya juu nchini, kundi ambalo ndilo tunalitegemea pia kupata walimu wa sayansi.

Kwa mujibu wa sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, asilimia tano ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi ndiyo wanaofika mpaka kidato cha tano na sita. Asilimia nne wanajiunga na masomo ya elimu ya juu.

Maelezo zaidi ya sera hiyo yanasema kuwa katika wanafunzi wanaosoma sekondari nchini, 30 hadi 35 kati ya 100 ndiyo wanaosoma masomo ya sayansi wakiwa kidato cha tatu na nne.

Idadi hii ya wanafunzi ndiyo inayotegemewa kusomea kozi za sayansi na teknolojia katika vyuo na taasisi za elimu ya juu nchini, kundi ambalo ndilo tunalitegemea pia kupata walimu wa sayansi.

Baadhi ya wanafunzi shuleni wamechagua kusoma masomo ya sanaa kwa hofu ya kufeli masomo ya sayansi kwa kukosa walimu wanaoweza kuwasaidia kimasomo na ukosefu au upungufu wa vifaa vya kujifunzia masomo hayo, hivyo kuendeleza dhana ya kuwa masomo ya sayansi ni magumu.

Zisemavyo takwimu

Kwa mujibu wa takwimu za elimu ya msingi Tanzania (BEST), hadi kufikia mwaka 2013, kulikuwa na vyuo vya ualimu 17 tu kati ya vyuo 34 vya Serikali ambavyo vilikuwa na maabara za sayansi. Hizi ni maabara ambazo zinategemewa kuandaa walimu wa sayansi kwa shule takribani 3,528 za Serikali nchini.

Kwa upande wa sekondari, ujenzi wa maabara unaendelea kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete linalotaka kila sekondari ya Serikali nchini kukamilisha zoezi hilo ifikapo Juni mwaka huu.

Kukamilika kwa maabara hizi ni hatua moja kwani bado kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya maabara na walimu wa sayansi ambao hawatoshelezi.

Takwimu hizo kwa mwaka 2013, zinaonyesha kuwa uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi katika ngazi ya sekondari ulikuwa 1:25. Uwiano unaopendekezwa na Serikali kwa shule za sekondari ni 1: 40.

Pamoja na uwiano huo mzuri bado kuna uhaba wa takribani walimu 27,000 wa masomo ya sayansi nchini. Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa kati ya walimu 12, 438 waliokuwa wakisomea Stashahada ya ualimu ni walimu 3,120 sawa na asilimia 25.1 ndiyo waliosomea sayansi. Waliobaki walisomea mengine.

Upungufu huu unaakisi tatizo sugu la walimu wa sayansi na ipo wazi kuwa tatizo ni kubwa zaidi katika mikoa ya pembezoni mwa Tanzania ambapo walimu ama huyakimbia mazingira au kuna mgawanyo wa Serikali usiozingatia mahitaji.

Kilio cha walimu wa sayansi

Pamoja na serikali kutoa ufadhili kwa walimu wanafunzi wa masomo ya sayansi, bado changamoto zinazowakabili walimu ni nyingi na kwa kiasi kikubwa zinaathiri ufundishaji.

Serikali inaweza kuaandaa walimu wengi wa sayansi lakini mazingira duni ya kazi ya walimu yanawavunja moyo walimu kufundisha kiasi cha kukatisha tamaa shauku waliyonayo ya kuwasaidia wanafunzi.

Licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali kuongeza idadi ya walimu haina budi kuandaa mazingira mazuri ya kazi ili walimu wabaki shuleni na kufundisha.

Takwimu aidha zinaonyesha kuwa takribani asilimia 77 ya walimu nchini huacha kazi na kwenda kufanya kazi nyingine zenye maslahi zaidi, na hii inaonyesha kuwa uzalishaji wa walimu na namna ya kuwabakiza kazini bado ni tatizo nchini.

Ufumbuzi wa tatizo

Lazima Serikali iwe na mipango ya muda mfupi na muda mrefu ya kuandaa walimu na kuwajengea mazingira mazuri ya kazi. Moja ya mipango ya muda mfupi ni Serikali kuajiri walimu wa sayansi kutoka nchi za nje hususani zile zenye mfumo wa elimu kama wetu.

Vilevile Serikali itoe posho kwa walimu wanaofundisha katika mazingira magumu ili kuwapa hamasa. Ikumbukwe kuwa Novemba 2011 wakati wa vikao vya Bunge, aliyekuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa Serikali ilipanga kutoa Sh 500,000 kwa kila mwalimu atakayepangwa kufundisha katika mazingira magumu.

Hatuna uhakika kama Serikali inatekeleza ahadi yake hii njema.

Aidha, Serikali pia ipunguze gharama za uingizaji wa vifaa vya elimu vinavyoingizwa nchini, hasa vifaa vya maabara na kupunguza kodi kwa vile vinavyotengenezwa nchini.

Mpango wa Serikali wa kutoa ufadhili kwa walimu wanafunzi wa masomo ya sayansi na kujenga maabara uendane na kuwekeza vya kutosha katika huduma za msingi shuleni na kumpa mwalimu stahiki zake pamoja na huduma nyingine za kijamii.

Katika ulimwengu wa sasa ulioendelea katika nyanja mbalimbali, hatuwezi kupiga hatua kielimu kama mwalimu atabaki katika maisha yaleyale ya zamani na bado tukategemea matokeo makubwa ya elimu.