Sababu za kuulinda Muungano tunazo

Muktasari:

Marais wa nchi hizi mbili ambazo sasa zinaunda Tanzania, Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar) walitia sahihi mkataba wa kuunganisha nchi zao, unaojulikana kama “Hati ya Muungano” (Articles of union) na hivyo kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho inaadhimisha miaka 54 tangu ilipoasisiwa Aprili 26, 1964 baada ya nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar kuungana katika tukio la kihistoria.

Marais wa nchi hizi mbili ambazo sasa zinaunda Tanzania, Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar) walitia sahihi mkataba wa kuunganisha nchi zao, unaojulikana kama “Hati ya Muungano” (Articles of union) na hivyo kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Huu ni Muungano wa kihistoria kutokea Afrika na duniani kote, yapo mataifa mbalimbali yalivyojaribu kuungana lakini hayakufika mbali na matokeo yake kusambaratika.

Mifano ipo mingi, lakini tutakumbuka Februari Mosi 1982, mataifa mawili ya Afrika Magharibi ya Senegal na Gambia yaliungana ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofanywa na viongozi wa nchi hizo na kutiwa saini Desemba 12, 1981.

Ingawa lengo la muungano huo lilikuwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili, lakini haukudumu na Septemba 30, 1989, Senegal iliuvunja baada ya Gambia kutoonyesha nia ya kuungana.

Mfano huu unaonyesha wazi jinsi baadhi ya mataifa yalivyojaribu bila ya mafanikio kuungana, lakini hayakufanikisha kutokana na sababu nyingi kubwa ikiwa ni utashi wa dhati wa kisiasa pamoja na masilahi.

Tanzania imefanikiwa katika hili na sasa tunapozungumza ni zaidi ya miaka 50 tunasherehekea kuungana kwetu. Tunayo kila sababu ya kuwapongeza waasisi wa Muungano kwa wazo lao la kuungana.

Lakini pia, baada ya kuungana huko wapo viongozi mbalimbali waliousimamia wakiwamo marais wa vipindi mbalimbali ambao pamoja na mambo mengine walihakikisha Muungano wetu hauvunjiki.

Ni dhahiri kwamba wamefanya kazi kubwa iliyotukuka ambayo itaendelea kuenziwa na vizazi vya sasa na vijavyo.

Wakati tukisherehekea miaka hii 54 ya umoja wetu, hatuna budi Watanzania wote kuuenzi Muungano wetu na kutoruhusu mahasidi kuubomoa.

Lakini pia, viongozi wana jukumu la kuendeleza jitihada za kutatua kero zote za Muungano ambazo zimekuwa zikikwamisha baadhi ya shughuli za kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, kero za Muungano ambazo hazijatatuliwa ni chache ukilinganishwa na 15 zilizokuwapo awali.

Hali ya kupuuzia na hata kuuchezea Muungano wetu ni hatari sana. Mathalani Wazanzibari wakiamua kujiengua kwenye huu Muungano, hawatabaki salama. Mwalimu Nyerere alishawahi kusema ya kuwa “wakifika kwenye hatua hiyo watagundua kuwa ndani yao kuna Wazanzibari na Wazanzibara”. Nao wataamua kuwafukuza wale wa Wazanzibara, lakini hiyo haitakuwa mwisho. Punde si punde watajigundua kuwa nao (Wazanzibari) wamegawanyika kwani kuna Wapemba na Waunguja, na wakifikia hapo pia hawatakuwa salama.

Vivyo hivyo kwa watu wa Bara (Tanganyika), ni rahisi kwao kutafunwa na dhambi ileile ya ubaguzi watakayo anzisha nje ya uwepo wa Muungano. Ni rahisi sana kwa ukabila, udini, ukanda na hata U-rangi kutamalaki ndani ya jamii wakishafikia hapo.

Tukumbuke Muungano huu tulionao unawafanya wageni, mataifa ya nje na watu wote wenye hila kuogopa kutugusa na kutuvuruga kutokana na kuwepo kwa nguvu kubwa ya umoja, ushirikiano na mshikamano baina yetu.

Muungano wetu unatupatia fursa kubwa ya uhuru wa kusafiri kwa pande zote ama iwe ni bara au visiwani. Leo hii ni rahisi sana kwa mtu wa bara kwenda visiwani na hata wale wa visiwani kuja Bara kwa uhuru zaidi kwani Uhuru huo wa uwepo wa nafasi hiyo umeshalipiwa na huu Muungano wetu tulionao.

Pia, si jambo geni tena kwa sasa kuona pesa zikivuka bahari na kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya ufanyaji ununuzi wa biashara mbalimbali kama magari, nazi, karafuu na tende.

Licha ya kero kadhaa Muungano huu unatuzidishia fursa ya mianya ya uwanja mpana tena usio na kikomo wa ufanyaji biashara. Hautubagui au kuwa na upendeleo wa upatikanaji wa elimu, huduma za kijamii lakini kubwa hautugawi wala kuwa na upendeleo.

Njia mojawapo ya kuwaenzi vyema waasisi wetu ni kwa kuudumisha Muungano wetu ambao ni urithi wa aina yake waliotuachia. Watanzania inatupasa tuuenzi Muungano wetu kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwani ni nguzo na fahari ya kipekee na ya aina yake barani Afrika.

Tuadhimishe Miaka 54 ya Muungano kwa kuudumisha na kufanya kazi kwa bidii na endapo itatokea yeyote mwenye malengo ya kuubomoa au kuuvunja Muungano huu, basi ajue dhambi hii itamtafuna.

Mungu atuepushe na mawazo ya kuuvunja Muungano huu vichwani mwa viongozi na watawala wetu lakini pia kwa Watanzania wenyewe. Kheri ya miaka 54 ya maadhimisho ya Muungano.