Sababu za wanafunzi kupungua madaraja mbalimbali ya elimu

Muktasari:

  • Hali ilivyo ni kuwa wanaobahatika kumaliza ngazi moja ya elimu, karibu nusu wanashindwa kuendelea na ngazi nyingine.

Miongoni mwa changamoto tete za sekta ya elimu nchini ni pamoja na mdondoko wa wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu.

Hali ilivyo ni kuwa wanaobahatika kumaliza ngazi moja ya elimu, karibu nusu wanashindwa kuendelea na ngazi nyingine.

Kwa mfano, muhtasari wa takwimu za elimu kwa elimu awali, msingi na sekondari mwaka 2016 uliotolewa na Tamisemi unaonyesha wanafunzi waliokuwa wakisoma darasa la saba mwaka 2013 walikuwa 885,749.

Mwaka uliofuata (2014), wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza walikuwa 588,873. Miaka minne baadaye waliofanya mtihani wa kidato cha nne wakawa 385,938.

Unaposoma takwimu hizi, hukosi kugundua kuwa kadri wanafunzi wanavyopanda madaraja ndivyo wanavyopungua idadi yao.

Hali hii si kwa wanafunzi kuanzia mwaka 2013; ni ada ya miaka nenda rudi. Kwa mfano, wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2012 walikuwa 894, 881, walioanza elim ya sekondari kati yao walikuwa 560,706.

Hata hivyo, miaka minne baadaye (2016) waliomaliza walikuwa 349,524 kati ya 560,706 walioanza kidato cha kwanza. Zaidi ya wanafunzi 211,182 hawakumaliza elimu ya sekondari ya kidato cha nne.

Hali hii ya upungufu wa wanafunzi inaendelea hadi madaraja ya juu ya elimu ya sekondari. Kwa mfano, wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2014 walikuwa 297,488, lakini ni wanafunzi 73, 692 waliofanikiwa kufika kidato cha sita mwaka 2017. Wanafunzi 223,796 waliishia kidato cha nne. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Kwa nini wanapungua?

Mhadhiri wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Joviter Katabalo ananasibisha hali hiyo na utoro anaosema unasababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo mimba na ndoa za utotoni, biashara na wanafunzi kujiingiza katika makundi ya kihuni. ‘’Sababu kubwa ambazo zimeandikwa kitaalamu ni utoro mfano mwaka 2016 wanafunzi 61,488 waliacha shule,”anasema.

Anasema miaka 2016 kurudi nyuma utoro ulisababishwa na wazazi kushindwa kuwalipia watoto wao ada.

“Lakini kwa sasa Serikali imefuta suala la ulipaji ada kuanzia shule za msingi hadi sekondari, kwa hiyo hawa wanafunzi wanaoacha shule wanaamua tu kukaa nyumbani anasema na kuongeza:

“Mfano ukienda maeneo ya wafugaji utakuta vijana wengi wapo huko, pia kwenye madini, machimbo na biashara ndogondogo.

INAENDELEA UK.16

INATOKA UK.15

Mkurugenzi mkuu wa shirikisho la watoaji elimu wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara, Benjamin Nkonya, pamoja na kukiri sababu za utoro na mimba kwa wasichana, anasema usimamizi mbovu hasa shule za sekondari za Serikali unachangia mdondoko wa wanafunzi.

“Kwa jitihada hizi za elimu bure, hazina budi kwenda sambamba na usimamizi katika sekta hii, ili kuhakikisha elimu inakua na wanafunzi wanazidi kufanya vizuri,” anasema.

Mwamko mdogo wa wazazi unatajwa kuwa sababu kama anavyosema mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mpwapwa, Lukonge Mwiro

‘’Mzazi kutokuwa karibu na mwanawe kufuatilia maendeleo yake, inachangia mtoto kuyumba kielimu na kuamua kuacha shule kwani ni wanafunzi wachache ambao wazazi wao wapo karibu nao,’’ anaeleza.

Mazingira yasiyo rafiki

Mazingira yasiyo rafiki yanajumuisha ubovu na uduni wa miundombinu kama vyumba vya madarasa, vyoo pamoja na tatizo la lugha. Hizi ni sababu zinazowakatisha tamaa wanafunzi na hatimaye baadhi wanajikuta wakiacha masomo.

“Unakuta mwanafunzi anakuja hapa hajui kabisa lugha inayotumika kufundishia kwa mtu huyu unawezaje kumsaidia?” Anahoji mwalimu Mwiro na kuongeza: “Tumejaribu kutoa ushauri kwa wanafunzi, kutengeneza mazingira ya wao kuzoea lugha lakini wengine wanaamua kuacha shule kwa madai kuwa hawaelewi.’’

Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Saidi Mohammed anasema wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha maendeleo ya watoto wao kielimu. Anasema wazazi ndiyo chanzo kwa mtoto kutomaliza masomo.

“Unakuta mtoto haendi shule lakini mzazi haulizi chochote na wengine wanaruhusu watoto wao kuingia kwenye biashara mbalimbali. Haiwezekani wanafunzi wanaanza wengi halafu mwisho wa safari wanabaki wachache, wazazi tuamke tusicheze na elimu,’’ anaeleza.

Kufeli mitihani

Sababu nyingine kubwa ya madaraja ya elimu kupungua wanafunzi, ni idadi kubwa ya wahitimu kufeli mitihani ya kumaliza madaraja husika.

Vijana wengi wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu hawafaulu mitihani yao ya mwisho. Wakati mwingine si makosa yao, shule nyingi hazina vitabu vya kutosha, na kwa hiyo inabidi wanafunzi kadhaa wachangie kitabu kimoja, inasema sehemu ya chapisho liitwalo Ujana Tanzania (2011).

Chapisho linaongeza: “Majumbani mwao hakuna umeme na hivyo hawawezi kujisomea usiku. Shule nyingi hazina walimu wa kutosha, na kwa maana hiyo madarasa yana wanafunzi wengi kuliko idadi inayotakiwa.’’

Sababu maalumu kwa wasichana

Wanafunzi wa kike wana sababu na mianya zaidi ya kuacha shule kuliko wanafunzi wa kiume. Tafiti na uzoefu vinaonyesha wanafunzi wa kike wanaacha shule kwa sababu ya kupata mimba au kuolewa mapema, wazazi kuwalazimisha kukaa nyumbani kwa minajili ya kusaidia kazi za nyumbani.

Sababu nyingine ni ukosefu wa vyumba vya stara wanapokuwa katika mzunguko wa damu wa mwezi, uhaba wa vyoo na wasiwasi wa kudhuriwa wakati wakienda ama kurudi shule.

‘’Hadi kufikia mwaka wa mwisho wa elimu ya sekondari idadi ya wavulana na wasichana wanaosoma huwa sawa, lakini idadi yao wote huwa ni ndogo sana. Ni vijana wanne tu kati ya 100 wanaomaliza miaka sita ya elimu ya sekondari,’’ linaongeza kusema chapisho hilo lililotolewa kwa uratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (Unicef).

Mkakati wa Serikali

Serikali inatambua kuwa mdondoko wa wanafunzi ni changamoto kubwa katika mfumo wa elimu. Mbinu, mipango na mikakati mbalimbali imekuwa ikibuniwa kuhakikisha tatizo hili linatafutiwa ufumbuzi.

Moja ya mikakati hiyo ni kuanzishwa kwa mpango wa elimu bila ada kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari. Tangu kuanza kwa mpango huo ambao ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, wanafunzi zaidi wanaandikishwa shuleni.

Kwa mfano, takwimu za Tamisemi zinaonyesha kuwa watoto walioandikishwa darasa la awali na la kwanza mwaka 2017 walikuwa 3,188,149. Uandikishwaji huu ni sawa na ongezeko la wanafunzi 319,849 ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi hao mwaka 2016.

Ili kuondokana na kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaofika elimu ya sekondari, Serikali imeanzisha mfumo mpya wa elimumsingi ambapo wanafunzi watasoma kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne. Ni mpango unaolenga kuwaokoa maelfu ya watoto waliokuwa wakidondoka katika mtihani wa kumaliza darasa la saba.

Mikakati mingine ni pamoja na programu za utoaji chakula cha mchana na ujenzi wa miundombinu hasa mabweni kwa ajili ya wasichana ili kuwakinga na vishawishi vya kupata mimba.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anasema hadi Mei 2017, wizara yake ilisharatibu uboreshaji wa miundombinu katika shule 274 katika halmashauri 119. Uboreshaji huo ulihusisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 1081, vyoo 2802 pamoja na mabweni 200.

Nusura kwa wasichana

Kwa kuwa waathirika wakubwa wa mdondoko wa wanafunzi shuleni ni wasichana, wadau wamekuwa wakishauri pamoja na mambo megine wanafunzi wa kike kusoma katika shule zilizo jirani na maeneo wanamoishi.

Hii inaweza kusaidia wakaepukana na vishawishi na vikwazo ambavyo mwishowe huwaingiza kwenye janga la mimba za utotoni.

Mikakati mingine maalumu kwa ajili ya watoto wa kike hasa waliopevuka ni pamoja na kupewa elimu ya uzazi na makuzi kwa uwazi zaidi; kupunguziwa kazi za nyumbani na kaya masikini kuwezeshwa kwa kupewa mitaji ili kukimu ugumu wa maisha.