Friday, September 15, 2017

AJIRA&KAZI: Sababu za watu kufanya uchaguzi mbaya wa kazi

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Uchaguzi wa kazi ni uamuzi anaofanya mtu tangu anapopata wazo la kazi anayotaka kuifanya hadi atakapostaafu.

Ndoto za kimaisha ndizo zinazoongoza uamuzi wa mtu katika kipindi chote cha masomo yake.

Anapoomba kazi kwa mara ya kwanza na kuipata; anapobadilisha na hata anapofikia umri wa kustaafu.

Uamuzi huo unaposhindwa kukidhi matarajio na kumfanya mtu asifurahie kazi yake, tunaweza kusema hapo anakuwa amefanya uchaguzi mbaya wa kazi.

Uchaguzi wa namna hii unaweza kusababisha mtu asitumie uwezo wake wote kazini, hali inayoweza kuleta kutokuridhika na kazi.

Kwa kuwa kutokuridhika na kazi kunaweza kusababisha mtu aache kazi, au aendelee kufanya kazi yake kwa manung’uniko, makala haya yanaangazia sababu tano kubwa zinazochangia watu kufanya uchaguzi mbaya wa kazi.

Kukidhi matakwa ya soko

Mwenendo wa soko ni sababu moja kubwa inayoathiri uamuzi wa kazi anayoyafanya mtu.

Kwa kawaida, kazi zinazohitajika kwenye soko la ajira ndizo zinazowavutia watu wenye ndoto za kuajiriwa.

Hata hivyo, changamoto ya kuongozwa na soko ni pale mahitaji ya soko yanapobadilika ghafla kutokana na sababu mbalimbali ikiwapo ya kisera.

Hivi sasa kwa mfano, karibu kila chuo kikuu hapa nchini kina programu za ualimu.

Hiyo ni kwa sababu ya mahitaji makubwa ya walimu shuleni.

Wanafunzi wengi huona ni afadhali wasomee ualimu ili kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo.

Huko tuendako tunaweza kujikuta tuna idadi kubwa ya wahitimu wa ualimu kuliko mahitaji halisi tutakayokuwa nayo wakati huo.

Ikitokea hivyo, wahitimu wengi wa ualimu watalazimika kutafuta ajira nyinginezo nje ya ualimu.

Hali hii inaweza kuleta changamoto kwa wanafunzi waliosoma kozi ya ualimu kwa lengo la kupata ajira mapema.

Kufurika kwa soko kunaathiri mustakabali wa wanafunzi wanaosomea ujuzi mahususi kwa ajili ya kazi fulani zinazopatikana hivi sasa kwenye soko la ajira.

Kazi hizo zinapojaa, wanafunzi wengi huaachwa wakitangatanga bila uelekeo unaoeleweka.

Kukidhi matarajio ya watu

Kuna kazi ambazo jamii huziheshimu kuliko nyingine.

Mfano, kazi zenye kuhitaji ujuzi na maarifa maalumu ambayo si watu wengi wanaweza kuwa nayo.

Huheshimika zaidi kuliko kazi zinazotegemea ujuzi wa jumla.

Aidha, mtu anayefanya kazi kama hizi huchukuliwa kama mwenye hadhi ya pekee kwenye jamii na watu humpa heshima kama mtu mwenye ujuzi maalumu.

Kwa kuwa binadamu kwa hulka yake anapenda heshima, ni rahisi kazi za namna hii kuwa chaguo la watu wengi hasa wasioutambua wito wao.

Mara nyingi watu hawa hujikuta wakitamani kukidhi matarajio ya jamii kwa kuchagua kazi wanazojua zinaheshimika. 

Hata hivyo, mara nyingine baada ya kufanya kazi hizi zisizoendana na wito, mtu huweza kubaini anafanya kitu kisichokidhi matarajio yake binafsi.

Hali ya kuchoka huweza kusababisha kuacha kazi na kutangatanga kutoka kwenye kazi moja kwenda nyingine.

Kuiga waliofanikiwa

Kuna kijana mmoja alivutiwa na kazi za wakili mmoja aliyekuwa maarufu mwishoni mwa miaka ya tisini.

Kwa sababu ya mafanikio makubwa aliyokuwa nayo wakili huyo, kijana yule aliamua kusomea sheria.

Baada ya kusomea sheria na hatimaye kufanya kazi za uhakimu kwa zaidi ya muongo mmoja, bado kijana yule anasema hajafikia mahali akajisikia ameridhika na kazi hiyo.

Juzi nilikutana naye akijaribu kufanya mipango ya kusomea kitu kingine kama jitihada za kutafuta utoshelevu.

Si jambo baya kuvutiwa na kujifunza kwa watu tunaofikiri wamefanikiwa kwenye kazi zao.

Hata hivyo, unapoiga uamuzi wa mtu mwingine unahitaji kuchukua tahadhari.

Mtu anaweza kufanya vizuri kwenye eneo fulani la utaalamu, lakini hiyo isimaanishe wewe ukifanya kitu hicho hicho utafanikiwa.

Kila mtu ana namna yake ya kufanikiwa.

Kupata kipato kikubwa

Upo ukweli kwamba moja wapo ya sababu kwa nini tunafanya kazi ni kutuwezesha kumudu maisha yetu.

Kwa sababu hiyo, kazi zenye uhakika wa kipato kikubwa, huwavutia watu wengi kuliko zenye heshima lakini hazina kipato kikubwa.

Si wakati wote suala la kipato huwa ni sababu iliyokamilika kueleza kwa nini tunafanya kazi.

Yapo mazingira ambayo kazi inaweza kuwa na kipato kikubwa lakini haimfanyi mtu atumie uwezo na ujuzi wake kikamilifu.

Inapotokea mtu analipwa vizuri lakini haoni namna gani kazi hiyo inakwenda sambamba na vipaji na haiba yake, ni rahisi mtu huyo kuanza kujisikia kudumaa na hivyo kukosa furaha ya kazi.

Ufaulu hafifu na uchumi duni

Katika mazingira yetu, kiwango cha ufaulu ndicho kinachoamua hatma ya mtu.

Mtu mwenye ufaulu mkubwa wa masomo kwa kidato cha nne au cha sita ndiye anayekuwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya uchaguzi unaokidhi ndoto zake kuliko mwingine mwenye ufaulu usioridhisha.

Zipo kazi ambazo ili mwanafunzi apate nafasi ya kuzisomea na kuzipata, anahitaji kuwa na ufaulu mkubwa.

Hizi ni zile kazi zenye kuchukuliwa kuwa nyeti mfano udaktari, sheria na uinjinia.

Ndiyo kusema, ufaulu dhaifu unaweza kuzima ndoto za mtu na kumfanya achague fani ambazo awali hakuwahi huzifikiria.

Pia, uwezo mdogo wa kiuchumi unaweza kuzima ndoto za maisha ya watu wengi.

Jitihada za kupata mkopo wa elimu ya juu huchangia wanafunzi wasio na uwezo  kufanya maamuzi yasiyozingatia matamanio yao.

Ingawa ni kweli uchaguzi mbaya wa kazi unaweza kumgharimu mtu, bado hata hivyo, kuna nafasi isiyo na kikomo ya kurekebisha uamuzi uliokwisha fanywa.

Lililo muhimu ni kujua kile unachokihitaji.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU).  0754870815

-->