Safari ya miaka 35 ya Mukoba katika ualimu

Muktasari:

  • Haikuwa kazi rahisi kufika hapa alipo. Maisha ya ualimu wa Gratian Mukoba aliyestaafu hivi karibuni yalianza mwaka 1982 katika Shule ya Msingi Mwavile, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Alianza kama mwalimu wa shule ya msingi, akastaafu akiwa na kumbukumbu ya kuwa kiongozi wa juu wa wa shirikisho la wafanyakazi nchini.

Haikuwa kazi rahisi kufika hapa alipo. Maisha ya ualimu wa Gratian Mukoba aliyestaafu hivi karibuni yalianza mwaka 1982 katika Shule ya Msingi Mwavile, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Alijipambanua kama mtetezi wa haki na hata kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Walimu nchini(CWT) na baadaye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Katika maisha yake ya kazi Mukoba, amefundisha jumla ya shule saba katika mikoa ya Mwanza, Kagera na safari yake kuishia katika Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa ya jijini Dar es Salaam.

Mwandishi wetu Phinias Bashaya, amefanya mahojiano naye kuhusu safari yake ya miaka 35 akiwa mwalimu na kiongozi wa walimu nchini.

Swali: Kipi umejifunza kama mwalimu miaka yote ya utumishi wako?

Jibu: Nimejifunza kuwa elimu haithaminiwi kwa kiwango kinachotakiwa. Mazingira ya kujifunzia na kufundishia yamekuwa sio rafiki kwa watoto na walimu wao. Walimu wanakabiliwa na ukosefu wa nyumba, vifaa vya kutolea elimu, kutopandishwa vyeo, kutopandishwa mshahara, kutorekebishiwa mshahara mara wanapopanda madaraja, kutolipwa madeni yao kwa wakati na mengineyo.

Swali: unaridhika na hadhi waliyonayo walimu wa Tanzania?

Jibu: Siridhiki na hadhi ya walimu kwa sababu miaka ya 1960, walimu waliheshimika. Walilipwa mishahara mizuri hivyo walimiliki magari, wakajenga nyumba bora na kusomesha watoto wao. Wananchi au jamii ilikuwa ikiwaheshimu walimu. Na wao walitumikia wito wao kwa moyo mmoja huku wakijibeba na kujielewa. Waliendelea kujinoa ili wawe imara kitaaluma, lakini kwa sasa ualimu umepoteza heshima yake.

Swali.Walimu wanachukuliwa kama kundi la watumishi waoga wanaolalamika tu badala ya kuchukua hatua; jambo hilo lina uhalisia wowote?

Jibu.Hili lina ukweli fulani kwani hata pale tulipofuata sheria zote za nchi tukafikia hatua ya kufanya mgomo baada ya milango ya mazungumzo kufungwa, bado wanachama wengi waliogopa vitisho vya mwajiri wakaenda kazini. Bado kunatakiwa kujengwa moyo wa kujiamini kwa walimu na hili litatokana na kiwango cha kujielewa na kujua thamani halisi ya kazi yao.

Swali. Ni kitu gani kilikusukuma kuwania nafasi za uongozi kwenye Chama cha Walimu

Jibu. Tangu utoto wangu nachukia uonevu au haki kupotea. Msukumo huu umo ndani yangu, nahisi ndio umekuwa nguvu nyuma ya harakati zangu za kuipigania kila siku.

Swali. Walimu walikuamini na kukuchagua kuwa Rais wao, unadhani matarajio yao kwako yametimia?

Jibu. Kuongoza walimu kulitokana na jinsi nilivyojipambanua kupigania haki kuanzia shuleni Kahororo wilaya ya Bukoba na shule nyinginezo. Baada ya kuongoza sehemu hizo, walimu wa nchi nzima waliniamini na kunichagua kwa mara ya kwanza mwaka 2002 kuwa makamu wa Rais wa CWT na 2007 kuniamini zaidi na kunichagua kuwa Rais wa CWT na 2014 wafanyakazi wote kunichagua kuwa Rais wa TUCTA (Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania).

Swali.Ni mambo gani mapya yamefanyika katika uongozi wako ambayo ungependa yakumbukwe na kuendelezwa?

Jibu. Katika uongozi wangu yamefanyika mengi. Siwezi kusema kuwa ni mimi mwenyewe kwani taasisi huongozwa na timu. Nishukuru Mungu kwa kunikutanisha na timu nzuri niliyofanya nayo kazi na kuweza kupata mafanikio yaliyoipambanua CWT kama chama kikubwa na chenye nguvu kulinganisha na vingine.

Mambo makubwa ni ujenzi wa ofisi za mikoa na wilaya, ujenzi wa jengo la uwekezaji la Mwalimu House, ununuzi wa vifaa vya kutendea kazi kama magari na samani za ofisi. Pia, nimeacha wigo wa madaraja ya walimu umepanuliwa kwa madaraja mawili zaidi kwa kila ngazi.

Swali.Umewahi kuongoza mgomo wa walimu nchi nzima kudai masilahi yao, unadhani ulifanikiwa kushinikiza kile mlichokidai?

Jibu. Niliongoza migomo miwili mwaka 2008 na 2012, tulifanikiwa kiasi kwani kila mgomo ulipoisha walioshiriki kikamilifu waliongeza ujasiri na wale walioogopa kushiriki waliona kuwa inawezekana.

Hatukupata kile tulichokidai kwa ukamilifu, kwani mwajiri mara zote aliumaliza mgomo wetu kwa kutumia mahakama ambayo haikutupatia kile tulichokuwa tunadai, hivyo kuacha hali isiyo njema kwa upande wetu.

Swali. Mliwezaje kukaa meza moja na Serikali kumaliza mgomo?

Jibu. Hatujawahi kukaa mezani na Serikali kumaliza mgomo, migomo mitatu ya 1993, 2008 na 2012 yote iliisha kwa vitisho na walimu kurudi kazini huku wameinamisha vichwa chini.

Swali. Nini chanzo cha kuwapo kwa makundi yenye mtizamo tofauti kwenye chama yaliyokuwa yanashinikiza kujitenga na kuanzisha chama kipya cha walimu?

Jibu. Chanzo cha makundi ndani ya chama ni sheria inayoruhusu uanzishwaji wa vyama, vingine ni yale niliyoyaeleza hapo juu ya kuwa na waajiri tofauti. Pia, ipo hali ya ubinadamu; kuna mtu anaona akianzisha chama atapata uongozi hasa baada ya kugombea na kushindwa.

Swali. Hadi unaondoka kwenye uongozi wa CWT, kundi linalotaka kujitenga bado lipo au changamoto hiyo imetatuliwa?

Jibu. Bado lipo na linajinasibu kwa kueleza kuwa nchi nyingine zina vyama vinane hata zaidi. Mimi nimekwenda nchi nyingi, pale penye utitiri wa vyama na mashirikisho sikuwahi kusikia faida kwa wafanyakazi zaidi ya malalamiko na sehemu nyingi vyama vimekuwa vikiungana na kuacha kugawana nguvu ili viweze kumkabili mwajiri kwa nguvu moja na sauti moja.

Swali. Kwa nini CWT iliamua kuanzisha benki ya walimu?

Jibu. Katika dira yetu mwanzoni tulijiwekea malengo makuu matano likiwamo la kupigania hali bora ya uchumi wa wanachama hao

Sasa uanzishwaji wa benki ni kutekeleza lengo hili la kuwaimarisha wanachama kiuchumi. Hii inatatua pia tatizo la riba zisizo rafiki zinazotolewa na taasisi za fedha ambazo kwa kiwango kikubwa zimejinufaisha kwa kuwakopesha walimu na kuwatoza riba kubwa hadi asilimia 300.

Swali. Unalizungumziaje suala la elimu bure kwa wanafunzi na mazingira ya walimu kufundisha nchini?

Jibu. Suala la elimu bure kwa wanafunzi ni zuri, linaondoa kumfungia milango mtoto aliyezaliwa kwenye familia masikini ambazo zingeshindwa kumudu karo na mahitaji mengine ya shule. Hata hivyo, utaratibu huu umeleta changamoto kwani madarasa mengi yanajaa mno, huku ni kumweka majaribuni mwalimu ambaye kwanza hana motisha.

Labda nieleze hapa kuwa siku zinavyokwenda ndivyo binadamu anavyopaswa kutayarishwa kwa ubora zaidi. Kinachobeba uzito siyo idadi ya watu waliopo duniani kwa wakati fulani bali ubora wao. Uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa unatokana na upungufu wa watu bora unakwenda kuleta madhara makubwa mno.

Ni bahati mbaya kwamba gharama ya vita duniani kwa mwaka ni mara nane ya gharama ya kutolea elimu. Kama mataifa na Tanzania ikiwamo yatashindwa kubadilisha mizani hiyo hapo juu, dunia itaendelea kujiandalia angamizo lake.

Swali: Ni mambo gani katika elimu ungetamani yawe na msingi wa kudumu badala ya kutegemea utashi na matamko ya wanasiasa?

Jibu: Ningetamani kuufanya ualimu uwe kazi ya heshima namba moja kama ilivyo katika za Ujerumani na Finland. Kwa kufanya hivyo ualimu utavutia vijana wenye uwezo wa kutayarisha watoto kwa ubora unaotakikikana.

Ningetamani mazingira ya kufanyia kazi ya ualimu yaboreshwe ili wote wafundishaji na wajifunzaji waweze kutimiza kwa ukamilifu malengo ya kuelimisha na kuelimika.