Samatta aipa heshima Cecafa

Mbwana Samatta

Muktasari:

  • Nahodha huyo wa Taifa Stars anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji kwa sasa, aliisaidia TP Mazembe kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa 2015 akifunga mabao saba na kuibuka mfungaji bora.

Tuzo ya mchezaji bora wa ndani ya Afrika aliyopata Mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta mwaka 2015, imefungua milango ya heshima kwa Ukanda unaosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati, Cecafa.

Samatta aliyekuwa anachezea klabu ya DR Congo na mabingwa Afrika wakati huo, TP Mazembe alipata kura 127 na kuwazidi kipa wa TP Mazembe, Robert Muteba Kidiaba na mchezaji wa Algeria, Baghdad Bounedjah aliyekuwa wa tatu.

Nahodha huyo wa Taifa Stars anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji kwa sasa, aliisaidia TP Mazembe kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa 2015 akifunga mabao saba na kuibuka mfungaji bora.

Heshima Cecafa

Heshima kwa Cecafa aliyoiweka Samatta imeendelezwa na kipa wa Uganda, Dennis Onyango ambaye ameteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika, ndani ya Afrika kwa 2016 akimrithi Samatta.

Onyango alikuwa katika ‘list’ ya wachezaji watatu waliotajwa kuwania Tuzo ya Glo-Caf 2016 pamoja na mchezaji mwenzake wa Mamelodi Sundowns, Khama Billiat na Rainford Kalaba wa TP Mazembe ya DR Congo na Zambia.

Mafanikio

Mafanikio ya kipa huyo yanahitimisha furaha kwa mwaka 2016,  kwani timu yake imetwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa, Ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini ABSA, kuiongoza  Cranes kukata tiketi ya Afcon 2017 na kuchaguliwa katika kikosi bora cha Afrika 2016.

Kama ilivyokuwa kwa Samatta, kipa huyo wa zamani wa SC Villa, amecheza mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia ya Fifa akiwa na Mamelodi na bado Uganda inawania kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2018, Onyango anaweza kuwa na rekodi ya mbali zaidi.

Kikosi cha Afrika

Katika kikosi cha Caf African XI, Onyango anaunganishwa na mastaa wa Ligi Kuu ya England, Riyad Mahrez (Leicester City) ambaye ndiye mchezaji bora Afrika 2016, Sadio Mane (Liverpool) na Eric Bailly wa Manchester United.

Pia, yumo mshambuliaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang anayechezea Borussia Dortmund.