Serikali, wasanii wawasaidie Mama Kanumba, Lulu

Aprili 7, 2012 ni siku iliyobeba kumbukumbu nzito kwa msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael (Lulu). Ni siku aliyojikuta akiingia kwenye tuhuma za mauaji ya msanii mwenzie maarufu barani Afrika, Steven Kanumba. Lulu alifikishwa mahakamani na ilijiridhisha kuwa msanii huyo alikuwa na kesi ya kujibu.
Lulu alikiri mahakamani kuwa ni kweli alikuwa na uhusiano wa mapenzi na Kanumba na kwamba siku ya tukio kulikuwa na ugomvi wa kimapenzi dakika kadhaa kabla ya kifo cha Kanumba. Alisema kuwa ilikuwa ni kawaida yake kumtembelea mpenziwe nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.
Habari hii imepokelewa kwa simanzi kubwa miongoni mwa wapenda sanaa, familia yake na watanzania kwa ujumla ukizingatia kuwa Lulu bado ni msichana mdogo aliyekuwa na mvuto wa aina yake kwenye tasnia.
Kama ilivyokuwa kwa wadau wengi wa sanaa, nimekuwa nikiifuatilia habari hii kwenye vyombo vya habari kuanzia tukio lilipotokea hadi hukumu ilipopitishwa. Mahakama ni moja ya mihimili mikuu mitatu ya Serikali, hivyo basi hatuna shaka kabisa na busara ilizotumia kufikia hukumu hiyo.
Kwangu yote mawili; kufa kwa msanii na kufungwa kwa msanii ni mapigo makubwa. La kwanza ni kumpoteza moja kwa moja msanii Steven aliyefanya mapinduzi makubwa kuiweka Tanzania kwenye ramani ya sanaa kimataifa. Lakini la pili pia naliona kuwa pigo kwa sababu tutamkosa msanii Lulu kwa muda mrefu. Kumkosa huku kunagubikwa na wasiwasi iwapo msanii huyu atarudi uraiani kama alivyoingia gerezani.
Hakuna asiyejua kuwa maisha ya jela si rafiki. Ni maisha mapya yenye sheria na kanuni zake zilizo tofauti kabisa na ya uraiani. Kwa kawaida mfungwa anakosa uhuru wa kujichagulia aina yake ya maisha kama chakula, mavazi, vinywaji, mawasiliano, burudani na kadhalika.
Huku anaanza akiwa na marafiki wapya kabisa. Ingawaje si wote walio gerezani walifanya makosa, lakini wapo wahalifu sugu ambao haiwezekani kujitenga nao kwani mtakula na kulala pamoja. Ni maisha yanayohitaji tahadhari kubwa na usaidizi wa karibu kwa watoto wadogo kama Lulu.
Baadhi ya watafiti wanaamini kuwa miezi minane ya mwanzo wa kutumikia kifungo ndio wakati mgumu zaidi kwa mfungwa. Wakati huu ndio ambao mtu anahisi kupoteza ndoto zake za mafanikio alizoota tangu utotoni. Ni wakati ambao kama hatakuwa makini anaweza kumezwa na makundi mabaya.
Yawezekana Lulu na jamii wakadhani kuwa huo ndio mwanzo wa mwisho wa msanii huyo mdogo wa umri. Binafsi nadhani yeye mwenyewe ndiye mwenye kuibeba hatima yake. Anaweza kujiweka sawa kisaikolojia akakubaliana na hiki kilichotokea sasa. Bado maisha yanaendelea.
Lakini kwa upande mwingine, jela si jehanamu. Ni chuo cha mafunzo chenye kazi ya kurekebisha tabia. Tunaona watu wengi maarufu wakienda jela kwa makosa mbalimbali lakini bado wakiishi na fani zao katika kipindi chote cha adhabu. Pia kuna baadhi waliorudi uraiani na kufanya vizuri zaidi ya vile walivyoingia.
Mwaka 2005, Kimberly Denise Jones aliyejulikana kama Lil’ Kim alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani pamoja na kupigwa faini ya dola za Marekani 50,000 baada ya kuzidanganya mamlaka ili kuwaokoa marafiki waliofanya uhalifu. Hata hivyo mdada huyo alipunguziwa adhabu baada ya kuonesha utiifu akiwa kifungoni.
Mnamo mwaka 2013, mwimbaji na mwigizaji maarufu Lauryn Hill naye alitumikia kifungo baada ya kukutwa na hatia ya kushindwa kulipa kodi ya mapato kiasi cha dola za Marekani 1.8 milioni. Historia inaonyesha kuwa wadada hawa walifanya mapinduzi makubwa sana kisanii baada ya kutoka kifungoni.
Bado tunaamini kuwa Lulu angali na nafasi ya kufanya vizuri akiwa gerezani na hata baadaye. Kwa vyovyote vile  alikuwa na ndoto za kuleta mageuzi makubwa katika sanaa nchini. Mmoja wa walimu wangu wa uandishi alifanya kazi nzuri wakati akitumikia kifungo gerezani. Kwa maneno yake aliniambia kuwa yalikuwa ni matokeo ya kusimamia ndoto zake.
Kwa upande huu wanasaikolojia wanasema kuwa ukitaka kuzishinda sononi zako zigeuze kuwa mzaha. Zione kuwa changamoto inayokukumbusha jambo, na ukishalikumbuka yenyewe inapita zake. Nadhani hili linawezekana iwapo utakumbuka kuwa si kila mfungwa ametenda dhambi.
Ingawaje si rahisi kulisimamia hilo hasa kwa binti mdogo kama Lulu, lakini hayo yanawezekana kujijenga baada ya kukubaliana na hali halisi, baada ya kipindi kigumu cha mwanzoni. Ni muhimu kumtanguliza Mungu na kujipa moyo bila kusahau kudumisha nidhamu na utii kwa mamlaka.
Wito wangu kwa familia na wote walioguswa kwa karibu na matukio hayo ni kumshukuru Mungu kwa kila jambo. Kila analolipanga huwa na makusudi kwetu. Moja kati ya makusudi ni kutupa mafundisho juu ya maisha yetu ya kila siku. Lakini lingine ni kutupima jinsi tunavyoweza kukabiliana na changamoto kama hizi.