MAONI YA MHARIRI: Serikali ifuatilie kadhia ya wanaofukuzwa Msumbiji

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Suzan Kolimba

Muktasari:

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo hata gazeti hili lilichapisha jana zinaonyesha kuwapo kwa hali tete zaidi, kwani raia hao mbali ya wengi kuwekwa mahabusu nchini humo, baadhi yao wameanza kurudishwa nyumbani.

Kwa siku kadhaa vyombo va habari nchini vimekuwa vikiripoti taarifa za matukio ya unyanyasaji na hata ukatili wanaofanyiwa raia wa Tanzania wanaoishi katika baadhi ya maeneo nchini Msumbiji.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo hata gazeti hili lilichapisha jana zinaonyesha kuwapo kwa hali tete zaidi, kwani raia hao mbali ya wengi kuwekwa mahabusu nchini humo, baadhi yao wameanza kurudishwa nyumbani.

Hadi jana, Watanzania wapatao 180 walishafukuzwa na kurudishwa nyumbani. Idadi hiyo ni kwa mujibu wa Ofisi ya Uhamiaji mkoani Mtwara ambayo hata hivyo inakinzana na idadi ya watu 132 iliyotolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Suzan Kolimba.

Tangu kuanza kwa kadhia hii kumekuwapo sintofahamu kuhusu sababu hasa ya raia hao wa Tanzania kufukuzwa kutoka katika maeneo kama Mtepweshi na Nanyupu.

Serikali kupitia Waziri Kolimba inaamini hiyo ni operesheni maalumu ya kuwarudisha nyumbani wahamiaji haramu wa mataifa mbalimbali inayoendeshwa na serikali ya Msumbiji. Lakini kwetu sisi hatua hiyo inaacha maswali lukuki.

Tukikopa maneno ya Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Mtwara, Rose Mhagama, operesheni hiyo hata kama ni zoezi rasmi, bado inaleta sintofahamu na maswali kama vile kwa nini wahusika wafikie hatua ya kuwachania Watanzania hati zao za kusafiria na kunyang’anywa mali zao?

Sintofahamu hii ndiyo inayotukusukuma kuamini huenda kuna tatizo la msingi ambalo mamlaka zetu bado hazijaliweka bayana.

Kimsingi, zipo taratibu zinazotumika kuwarudisha wahamiaji haramu makwao ambazo hata sisi Tanzania tumekuwa tukizitumia tukiwa ni moja ya nchi zinazosumbuliwa kwa kiwango kikubwa na tatizo la wahamiaji haramu.

Kwa Tanzania, hakuna rekodi za wahamiaji hawa kufanyiwa ukatili au kunyang’anywa mali zao wakiwa katika ardhi yetu. Tunajiuliza cha mno nini walichofanya raia wa Tanzania huko Msumbiji?

Aidha, tangu kuanza kwa madhila haya yanayowapata raia wa Tanzania, kunaonekana kuwapo kwa mkono mfupi wa ushiriki wa ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji, licha ya Wizara ya Mambo ya Nje kusema ubalozi wetu unashirikiana na serikali ya Msumbiji kuhakikisha Watanzania hawapati matatizo katika operesheni hiyo.

Wakati wizara ikiamini hivyo, wananchi hao wanalalamika kufanyiwa vitendo vya kikatili, jambo linalotusukuma kujiuliza ni kwa namna gani mamlaka zetu zinathamini raia wa Tanzania hasa wanaopatwa na madhila mbalimbali nje ya nchi?

Kwa vyovyote itakavyokuwa, Watanzania hawa ambao wanafukuzwa Msumbiji wanastahili haki ya utu wao, kupata heshima na si kudhalilishwa kwa namna yoyote ile.

Inatia moyo kuwa Waziri Kolimba ameshasema kuwa wanafuatilia tuhuma hizo za baadhi ya Watanzania kufanyiwa ukatili. Tunaomba ufuatiliaji huo ufanywe haraka ili kunusuru maisha ya raia hawa.

Kama ambavyo nchi yetu inavyowakirimu wageni na kutumia taratibu kushughulika na wale wanaovunja sheria, tungependa hali hii pia iwakute Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania.

Tungeshauri mambo haya yanapotokea kuwe kuna uharaka wa kushughulikia, kwa sababu inavyoelekea kumekuwa na mkanganyiko wa sababu za kufukuzwa kwa Watanzania hao kwa maofisa wa serikali kupishana kuelezea sababu za kufukuzwa kwao.