Serikali inatumia mabilioni kutibu magonjwa yasiyoambukiza

Muktasari:

Maradhi ya moyo na maambukizi ya figo ni miongoni mwa magonjwa hayo ambayo yanakuwa tishio kwa wananchi wengi huku matibabu yake ambayo mara nyingi hufanyika nje ya nchi yakiigharimu Serikali zaidi ya Sh36.6 bilioni kati ya mwaka 2013 na 2016 kama zinavyobainisha takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Maambukizi na athari za magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuongezeka nchini huku yakizigharimu familia na taifa fedha nyingi kukabiliana nayo.

Maradhi ya moyo na maambukizi ya figo ni miongoni mwa magonjwa hayo ambayo yanakuwa tishio kwa wananchi wengi huku matibabu yake ambayo mara nyingi hufanyika nje ya nchi yakiigharimu Serikali zaidi ya Sh36.6 bilioni kati ya mwaka 2013 na 2016 kama zinavyobainisha takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Taarifa za wizara hiyo zinaeleza kuwa ndani ya muda huo jumla ya wagonjwa 590 waliosafirishwa na Serikali kwenda kutibiwa nje, 430 walikuwa na magonjwa ya moyo na 160 walihitaji kupandikizwa figo.

Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja anasema magonjwa ya moyo huwaathiri zaidi watu wazima kuliko watoto na kushauri kuzingatia mazoezi ili kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi hayo.

Anasema ndani ya muda huo, watoto 186 waliopelekwa nchini India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji

wakilinganishwa na watu wazima 244 waliokuwa na matatizo ya moyo hivyo kuhitaji huduma za madaktari kuokoa maisha yao.

Kama ilivyo kwa magonjwa ya moyo, Mwamaja anasema ndani ya miaka hiyo mitatu, maambukizi ya figo yamejitokeza zaidi kwa watu wazima huku kukiwa hakuna mtoto aliyekwenda nje ya nchi kwa matibabu ya maradhi hayo.

Akifafanua taarifa zilizopo za waliopandikizwa figo anasema: “Kati ya Julai 2013 na Juni 2014 kulikuwa na wagonjwa 51; Julai 2014 mpaka Juni 2015 walikuwapo 59; na Julai 2015 mpaka Juni 2016 Watanzania 50 walipata matibabu hayo. Gharama zao zinahusisha ndugu wanaokwenda kuwatolewa figo.”

Ni dhahiri, kuanzia Julai 2013 mpaka Juni 2016, Watanzania 160 wakiambatana na ndugu zao 160 walikwenda nchini India kwa ajili ya kupandikizwa figo kwa gharamma za Serikali.

“Naamini kitengo cha kupandikiza figo kikianzishwa Muhimbili gharama hizi zitapungua,” anasema Mwamaja.

Kuhusu matibabu ya magonjwa ya moyo na gharama zake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi anasema kumtibu mgonjwa mmoja ambaye atapelekwa nje ya nchi kufanyiwa upasuaji ni Dola za Marekani 27,500 ambazo ni zaidi ya Sh55 milioni.

“Gharama huwa zikitofautiana kulingana na anachotibiwa mgonjwa. Mara nyingi inaanzia Dola 15,000 mpaka 27,500 endapo mgonjwa atawekewa betri maalumu ya kumsaidia kupumua kwenye moyo (Pecemaker),” anasema Profesa Janabi.

Daktari Bingwa wa Figo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Jacqueline Shoo anasema utaratibu wa kusafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi umekuwa ukiratibiwa na Wizara ya Afya huku ukiigharimu Serikali kati ya Dola 15,000 (zaidi ya Sh30 milioni) na 35,000 (zaidi ya Sh70 milioni) za Marekani kupandikiza figo moja.

Kwa utaratibu uliopo, wizara hufanya hivyo kwa wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka hospitali zinazotambulika nchini na zenye ruhusa ya Serikali kutoa kibali hicho baada ya kuthibitika kutowezekana kwa matibabu hayo nchini.

Dk Shoo anasema MNH imekuwa ikisafirisha mgonjwa na mchangiaji wake wa figo kwa gharama za Serikali, lakini mara nyingi huwa zinaongezeka kutokana na masuala mengine kama vile malazi, chakula na usafiri.

“Kwa utaratibu uliopo, mgonjwa na mchangiaji hugharamiwa kukaa kwa wiki mbili ikijumuisha vipimo, upasuaji na maabara au ICU itakapobidi,” anasema.

Utafiti uliofanywa nchini na Shirika la Afya Duniani (WHO) ujulikanao kama Tanzania Steps Survey kati ya Februari na Oktoba mwaka 2012 ulibainisha asilimia 92.6 ya washiriki 5,680 waliopimwa na kukutwa na shinikizo la damu walikuwa hawajaanza matibabu hali inayowaweka kwenye hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Utafiti huo unatoa mwanga wa ongozeko la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza nchini yakiwemo kisukari, moyo, saratani na mapafu.

Matokeo ya awali ya utafiti huo uliofanyika kwa awamu tatu yanaonyesha watu wanaokabiliwa na shinikizo la damu wapo kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya magonjwa mengine yasiyoambukiza kuliko wasionao.

Mwenyekiti wa Chama cha Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (Tancda), Dk Tatizo Waane anasema utafiti huo ulilenga kuangalia ukubwa wa magonjwa hayo nchini yanayosababishwa na mfumo wa maisha mfano kutokufanya mazoezi, ulaji holela wa vyakula, utumiaji wa tumbaku na unywaji wa pombe kupita kiasi.

Anasema kati ya washiriki hao waliotoka kwenye mikoa 20; asilimia 14.1 walikuwa wanavuta sigara, huku asilimia tano tu wanatumia matunda kwenye milo yao. Asilimia 4.5 wanakula mboga za majani wakati asilimia 30 hawafanyi mazoezi.

Asilimia 26 walibainika kuwa na uzito unaoongezeka, asilimia 8.7 wana uzito uliopitiliza na asilimia 30 wanaongezeka lehemu.

Akielezea athari za magonjwa hayo, Makamu Mwenyekiti wa Tancda, Profesa Andrew Swai anasema zaidi ya vifo milioni 56 vinavyotokea duniani kila mwaka husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza ikilinganishwa na vifo milioni 38 vitokanavyo na magonjwa ya kuambukiza. Anasema kwa mujibu wa kikao cha Halmshauri ya Umoja wa Mataifa (UN) kilichofanyika mwaka 2011 na mkutano wa pili mwaka 2014, mpaka mwaka 2018, Tanzania inatakiwa kupunguza magonjwa yasiyoambukiza kwa asilimia 25.

“Magonjwa yasiyoambukiza hayapewi kipaumbele kwani bajeti yake, mara nyingi, huelekezwa kwenye magonjwa ya kuambukiza kama vile Ukimwi, Malaria na kifua kikuu,” anasema Profesa Swai.

Mmoja wa wagonjwa wanaoishi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Ramadhani Mongi anasema: “Serikali inatakiwa kuweka sera na sheria za kuangalia watu ambao tayari wameathirika na magonjwa haya na kuweka mikakati ya kulinda wale ambao bado hawajakumbwa na magonjwa haya, lakini pia kudhibiti matangazo na biashara chochezi za magonjwa haya.”