TAKWIMU NA UCHUMI: Serikali iwekeze kimkakati kuwainua wanyonge, masikini

Serikali ya awamu ya tano ni ya wananchi wanyonge na masikini. Imewapa kipaumbele wao.

Kwa mtazamo wangu, hawa wanahitaji mambo makuu matano ili waweze kufurahia kutambuliwa na kuthaminiwa kwao na Serikali ya hii iliyoamua kuwapa kipaumbele katika uongozi wake.

Afya ni changamoto inayohitaji majibu ya uhakika kutoka kwa wahusika. Ni ukweli usiopingika kuwa kila mwananchi anahitaji kuwa na afya bora ili aweze kutimiza majukumu yake vyema. Binadamu yeyote asiye na afya bora hawezi kuzalisha ipasavyo.

Kero zilizopo kwenye sekta hii zinahitaji ufumbuzi ili kwani wenye kipato duni wanapozikosa kwa wakati hushindwa kupata mahitaji muhimu ikiwemo chakula, malazi, mavazi hivyo kuchochea ufukara.

Hivyo, ili mkulima, mfanyakazi au mtu mwingine yeyote aweze kufanya kazi kwa faida yake binafsi na taifa kwa ujumla anahitaji kuwa na afya bora. Serikali inapaswa kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha uwepo wa zahanati kwa kila kijiji, kituo cha afya kwa kila kata na hospitali kwa kila halmashauri.

Halikadhalika, hospitali teule kwa kila mkoa na hospitali ya rufaa kwa kila kanda. Vituo vya kutolea huduma za afya vinapaswa kuwa na dawa, vifaatiba, vitenganishi na wahudumu wenye weledi, maarifa na wanaoendana na mahitaji.

Uwezeshaji ni suala jingine muhimu ambalo Serikaliinapaswa kuliwekea mkazo. Ni jukumu la Serikali kuwezesha wananchi wake kiuchumi ili wawe na nguvu ya ununuzi bidhaa na huduma sokoni. Uwezeshaji unaweza kufanya kwa mambo mabadiliko kadhaa kwenye mfumo uliopo.

Mosi, kupunguza mfumuko wa bei. Takwimu zinaonesha tangu Januari mpaka Machi, 2017 mfumuko wa bei umekuwa ukipanda kila mwezi. Hali hii si kiashiria kizuri kwa ukuaji wa uchumi hasa kwa mwananchi wa kawaida.

Kupanda kwa bei hasa ya vyakula kunasababisha kuadimika kwa bidhaa husika hivyo kusababisha bei kupanda. Wenye kipato kidogo hushindwa kumudu gharama za ununuzi.

Vilevile ni muhimu kupunguza riba inayotozwa kwenye taasisi za fedha. Riba kubwa kwenye mikopo husababisha wakopaji kupungua hivyo uanzishwaji na uendelezaji wa biashara kudorora na mzunguko wa fedha kuwa mdogo.

Mjasiriamali husindwa kukuza mtaji hatimaye kuutumia kwenye shughuli za kawaida za kila siku. Mwisho wake ni kufa kwa biashara, kupungua kwa ajira, uchumi wa mwananchi kushuka na wa taifa kwa ujumla.

Tatu ni kuondolewa au kupunguzwa kwa utitiri wa kodi na tozo mbalimbali zilizopo. Pamoja na changamoto ya mtaji, mjasiriamali aliyepo sokoni anakabiliwa na kodi na tozo nyingi za kila aina.

Hii husababisha kiasi kidogo cha faida anachopata kurejeshwa serikalini, wakati mwingine hulazimika kukopa nje ya biashara ili kugharamia kodi na tozo hizi. Mfumo huu haumwezeshi mjasiriamali kukua bali kudumaa au kurudi nyuma.

Licha ya vingi vinavyofanywa na Serikali, maji ni kila kitu kwa maisha ya kila siku. Mwanachi mnyonge na masikini anahitaji kuwa na uhakika wa kupata maji ya kunywa, kunywesha mifugo au kumwagilia mazao yake.

Uwapo wa maji ya uhakika kwa wananchi wa mjini na vijijini ni kiashiria kizuri cha kutumia muda wao kuzalisha badala ya kutafuta maji kama ilivyo sasa.

Itakuwa busara, kwa nionavyo, badala ya kupeleka Sh50 milioni kwa kila kijiji kwa kupitia Saccos ni vyema zikatumika kujenga zaidi ya visima 1,500 kwa gharama ya Sh500 milioni kila kimoja na kuondoa kero iliyopo.

Ni wajibu wa Serikali kuwekeza nguvu nyingi kwenye ujenzi wa mabwawa ya kumwagilia na uvunaji wa maji ya mvua  ili wananchi wajikite kwenye kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua ambazo hazina uhakika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kila kitongoji kinapaswa kuwa na miundombinu ya kunyweshea mifugo ili kuepuka mwingiliano kwa wanyama na binadamu, wakulima na wafugaji pia.

Wananchi hasa vijana wanahitaji elimu itakayofanikisha masuala yao mbalimbali. Kila mmoja anatambua umuhimu wa elimu. Mwanachi mnyonge na masikini anahitaji, yeye na familia yake, kupata elimu bora.

Ni lazima Serikali iweke mazingira bora ya elimu ili wahitimu wawe na ubora unaohitajika sokoni. Mtoto wa mnyonge na masikini anatakiwa apewe kipaumbele kwenye mkopo akifanikiwa kufika elimu ya juu.

Vyuo vya kati vipewe rasilimali na elimu ya ujasiriamali ifundishwe katika hatua mbalimbali. Elimu bora na ya uhakika itamsadia mnyonge na masikini kuwa na uhakika kwa kipato ili kuinua uchumi wake na  wa taifa.

Kuna uhusiano wenye uthibitisho wa kisayansi kati ya uwapo wa nishati ya uhakika na maendeleo. Wananchi wanahitaji nshati ya uhakika kuanzisha viwanda vidogo vitakavyochakata mazao yao na kuongeza thamani sokoni.

Serikali ifahamu endapo itafanikiwa kuwekeza nguvu na rasilimali za kutosha kwenye maeneo afya, uwezeshaji, maji, elimu na nishati ambayo ni maeneo yanayomlenga mwananchi masikini na mnyonge itakuwa imefanikiwa kuboresha maisha na uchumi.

Mwandishi ni mtakwimu na ofisa mipango wa wilaya.

Maswali na majibu:
piga au sms kwa simu:  0685214949/0744782880
 [email protected].