Sheria, kanuni ununuzi wa umma zizingatiwe kuongeza tija

Muktasari:

  • Tathmini ya matumizi, inakadiriwa zaidi ya asilimia 40 yaliyopitishwa yameangukia upande wa ununuzi. Hii inamaanisha mwaka wa fedha ulioanzia Julai mpaka Juni mwakani zaidi ya Sh12.7 trilioni zitatumika kununua bidhaa, huduma, ujenzi na ushauri elekezi wa miradi mbalimbali.

Robo ya pili ya mwaka huu wa fedha inakaribia kwisha na matarajio ni kwamba bajeti iliyopitishwa, Sh31.7 trilioni kwa matumizi mbalimbali, itakuwa imeanza kutumika kwa ajili ya utekelezaji kati ya Julai hadi Septemba.

Tathmini ya matumizi, inakadiriwa zaidi ya asilimia 40 yaliyopitishwa yameangukia upande wa ununuzi. Hii inamaanisha mwaka wa fedha ulioanzia Julai mpaka Juni mwakani zaidi ya Sh12.7 trilioni zitatumika kununua bidhaa, huduma, ujenzi na ushauri elekezi wa miradi mbalimbali.

Kwa muktadha huu, idara ya ununuzi inahitaji kufanya kazi kwa weledi mkubwa hasa maofisa wanaohusika pamoja na wanasiasa, wakurugenzi, wajumbe wa bodi za zabuni, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wakaguzi wa hesabu na wahasibu.

Lengo ni kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo kuwapunguzia wananchi umasikini kama Rais John Magufuli inavyosisitiza mara kwa mara kwamba tunachokipata ni lazima kitumike kwa uaminifu na uadilifu. Kanuni namba 2(a)(b), 4(1) na 5(1) ya ununuzi ya umma ya mwaka 2013 inaagiza hilo.

Kumekuwa na upotevu wa fedha za umma kutokana na uzembe, udanganyifu na mambo kadha wa kadha yanayofanywa na sekta ya ununuzi. Ripoti ya CAG kwa mwaka 2015/16 inaonesha kati ya halmashauri 171 zilizokaguliwa; 138 zilipata hati za kuridhisha, 32 zilipata hati za mashaka na moja hati isiyoridhisha. Hati hizi zinatokana na kutozingatia sheria na kanuni za ununuzi pamoja na sheria za fedha na kanuni zake.

Iwapo sheria za ununuzi ya umma ya mwaka 2011 na mabadiliko yake ya mwaka 2016 bila kusahau kanuni za mwaka 2013 na mabadiliko yaliyofanywa mwaka 2016 na sheria za fedha za mwaka 2004 zitawekewa mkazo na kufuatwa, kutakuwa na mafanikio makubwa kwa Taifa.

Hii pia itawasaidia watumishi wa umma wanaohusika na ununuzi kufanya kazi zao kwa weledi hivyo kuepuka matumizi mabaya ya fedha za Serikali ama kwa makusudi au kwa kutojua.

Kutokana na Serikali kutilia mkazo eneo hili ili kuongeza mchango wake kwenye maendeleo ya nchi, ni vyema wadau wa ununuzi wakazingatia sheria, kanuni na taratibu kama zilivyoainishwa. Hili linaweza kutekelezeka kwa kuwakumbusha maofisa ugavi kuzingatia mambo ya msingi yaliyo katika sheria na kanuni husika.

Kwa ujumla zipo sheria 108 na kanuni 380 zinazotakiwa kuzingatiw akufanikisha ununuzi usiotia mashaka kwenye idara na ofisi zote za Serikali lakini makala haya yatazingatia vifungu vichache ambavyo vitajenga uwezo na kuongeza chachu kwa wahusika.

Ushindani

Kifungu cha 163 na 164 cha kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013 zinaelekeza kushindanisha watoa huduma wengi iwezekanavyo ili kupata thamani ya fedha kwenye kila kinachonunuliwa au mradi unaojengwa.

Kwa mfano, Juni 23, 2006; Tanesco ilisaini mkataba na Kampuni ya Richmond Development wenye thamani ya Dola 179 milioni wakati kampuni hiyo haikuwa na sifa stahiki kupata zabuni hiyo hivyo kuisababishia Serikali hasara kwa kutokufanya ununuzi kwa njia shindanishi.

Aidha ripoti ya CAG ya mwaka 2015/16 inabainisha zaidi ya Sh23.98 bilioni zilitumika bila kushindanisha angalau watoa huduma watatu.

Ukaguzi

Kukagua bidhaa au mradi kabla ya kuupokea ni maelekezo ya kifungu namba 244 cha kanuni za sheria za ununuzi wa umma ya mwaka 2013 na mabadilko ya mwaka 2016. Kanuni hii inamtaka kila ofisa masuhuli kuhakikisha kila bidhaa inayopokelewa imekaguliwa kulingana na vigezo vilivyotajwa katika mkataba na iliyo chini ya viwango isipokelewe.

Aidha, kifungu namba 245 cha kanuni hiyo kinataka kila ofisa katika mamlaka yake kuteua kamati ya ukaguzi wa kila bidhaa inayopokelewa kulingana na mkataba. Taarifa ya CAG ya mwaka 2015/16 inaonyesha vifaa vya Sh2.315 bilioni vilipokelewa na taasisi tisa bila kukaguliwa hivyo basi thamani halisi kutopatikana.

Taarifa

Kifungu namba 86(1)(2) cha kanuni za ununuzi kinamtaka kila mkaguzi wa ndani kuwasilisha taarifa ya robo mwaka kwa mkuu wa taasisi husika ambayo itaonyesha kama sheria na taratibu za ununuzi zimefuatwa au la na ndani ya siku 14 mkuu huyo wa taasisi aiwasilishe Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Aidha kifungu namba 87(2)(c ) kinataka kila taasisi kuwasilisha PPRA taarifa za ununuzi ndani ya siku saba baada ya mwezi kwisha au robo ya mwaka.

Vilevile kifungu namba 232 kinamtaka ofisa masuhuli kuwasilisha nakala ya barua za mikataba yote iliyoingiwa baina ya taasisi yake na wazabuni PPRA, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), CAG, mhakiki wa mali na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndani ya kipindi cha mkataba kilichokubaliwa.

Mkataba

Mikataba ni lazima ifanyiwe uhakiki na wanasheria wa taasisi husika kabla ya kusainiwa kama kiwango cha fedha hakizidi Shilingi bilioni moja vinginevyo upelekwe kwa AG kama kiwango ni zaidi ya Shilingi bilioni moja. Kifungu namba 59 cha kanuni za mwaka 2013 kinaelekeza hivyo.

Katika taarifa ya CAG ya mwaka 2015/16 inaonyesha msajili wa vyama vya siasa aliingia mkataba wa zaidi ya Sh668 milioni kipindi ambacho kiwango cha kupeleka mkataba kwa AG kilikua kuanzia Sh50 milioni.

Makubaliano

Kazi yoyote inayofanywa mtu binafsi au mzabuni kwa niaba ya Serikali ni lazima kuwe na mkataba ambao utazibana pande zote mbili; taasisi husika kwa upande mmoja na mzabuni kwa upande mwingine.

Hili ni takwa la kifungu namba 233 za kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013 na marekebisho yake ya 2016. Katika taarifa ya CAG mwaka 2015/16 inabainisha kuwa taasisi za umma zilitumia Sh11.253 bilionia bila kuwapo mkataba au makubaliano yanayokubalika kati yao na wazabuni au watoa huduma.

Dhamana

Katika kila zabuni iliyoingiwa kati ya taasisi ya umma na mzabuni lazima kuwe na hati ya dhamana kwa kipindi maalum kilichokubaliwa ili kazi husika iweze kufanywa kwa uaminifu ikiwa pamoja na kuwalipa vibarua, mafundi na watoa huduma kama wapo.

Haya ni matakwa ya kifungu namba 29 cha kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013.

Mambo haya machache yakitiliwa mkazo, thamani ya fedha itaonekana kwenye ununuzi wa Serikali kwa kiasi kikubwa idara husika kufanya kazi kwa weledi na ufanisi hivyo kuepuka matatizo ambayo yanaweza kuwapata watumishi husika.

Watumishi wote wanaohusika na mchakato huu wanapaswa kupewa elimu ili wawe na ufahamu wa kutosha na fedha inayotolewa kwa ajili ya kununua huduma, ujenzi, vifaa na ushauri inatumika ipasavyo.

Mwandishi ni mkaguzi wa ndani wa hesabu za kampuni na mwajiriwa wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. Anapatikana kwa namba 0715073996