MAONI YA MHARIRI: Sheria izingatiwe mgogoro wenyeviti wa mitaa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene

Muktasari:

Hatua ya waziri kusitisha agizo hilo la Novemba mwaka jana, imekuja baada ya viongozi hao wa ngazi ya msingi katika Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza kujiuzulu nyadhifa zao wakipinga uamuzi huo.

Juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alitangaza kusitisha agizo la kuwataka wenyeviti wa Serikali za Mitaa nchini kukabidhi mihuri kwa maofisa watendaji mpaka pale utaratibu mzuri utakapotolewa.

Hatua ya waziri kusitisha agizo hilo la Novemba mwaka jana, imekuja baada ya viongozi hao wa ngazi ya msingi katika Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza kujiuzulu nyadhifa zao wakipinga uamuzi huo.

Walisema kitendo cha kurejesha mihuri hiyo kilikuwa na athari kubwa kwa wananchi hasa wale ambao wanahitaji huduma kama ya kupata hati za dhamana mahakamani, vibali vya misiba, mikopo na barua za misamaha ya matibabu kwa wazee.

Serikali, kwa mujibu wa Waziri Simbachawene ilifikia uamuzi huo kutokana na matumizi mabaya ya mihuri kwa baadhi ya wenyeviti wa vijiji na mitaa akisema baadhi ya migogoro ya ardhi vijijini na mijini imechangiwa na kutumiwa vibaya na viongozi hao. Alitoa mfano akisema ardhi ya vijiji zinasimamiwa na Sheria namba 4 na 5 ya mwaka 1999 inayoeleza kwamba mwisho wa mwenyekiti wa kijiji kutoa eneo kwa mwekezaji ni ekari 50 lakini wapo wanaotoa ekari 100 hadi 1,000.

Katika hili, Serikali ilikuwa na hoja ya msingi lakini tunadhani ilichokosea ni kutowashirikisha wahusika tangu mwanzo wa mchakato huo na pia kujenga msingi imara wa utendaji wa watendaji wa mitaa na vijiji. Kama Simbachawene alivyobainisha, Tangazo la Serikali namba 3 la Mei 9, 1994 limeweka bayana vitendea kazi vya mwenyekiti wa mitaa na kijiji kuwa ni bendera yenye nembo ya halmashauri, orodha ya wakazi wa mtaa na daftari la muhtasari wa vikao.

Kadhalika, majukumu ya mwenyekiti wa mtaa wajibu wake yameanishwa kisheria kwamba ni pamoja na kuongoza mikutano yote ya kamati ya mtaa na mkutano mkuu wa mtaa; kusuluhisha migogoro midogomidogo ambayo haistahili kuitisha mkutano wa kamati ya mtaa au kupelekwa kwenye baraza la kata au Mahakama na kuwa msemaji wa mtaa.

Mengine ni kuwaongoza na kuwahimiza wakazi wa mtaa kushiriki shughuli za maendeleo, sherehe za Taifa, mikutano ya hadhara itakayoandaliwa na mtaa, halmashauri ya mji manispaa au jiji na Serikali; kuwakilisha mtaa kwenye kamati ya maendeleo ya kata; kutekeleza kazi atakazopewa na kamati ya mtaa na mkutano wa mtaa na kamati ya maendeleo ya kata; kusimamia utekelezaji wa kazi na majukumu ya kamati ya mtaa; kusimamia utunzaji wa rejesta ya wakazi wote wa mtaa.

Katika majukumu yote hayo, hilo la mihuri halimo na ndiyo maana Simbachawene alikaririwa akisema, “Mamlaka ya mwenyekiti na kijiji hayapo katika mihuri, bali kwenye uamuzi na kutokutumia muhuri hakushushi hadhi ya cheo alichonacho.” Huku akiwataka kutotumia kigezo cha mihuri kuingia kwenye mgogoro.

Idadi kubwa ya wenyeviti wa Serikali za Mitaa wamekuwa wakiitumia mihuri hiyo kupiga dili, huduma ambazo wamekuwa wakitoa kwa wananchi, wamekuwa wakizitoza kinyume cha utaratibu.

Hivyo tunadhani kwamba umefika wakati sasa kwa kila kiongozi kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Kama ni suala la kutoa huduma zinazolalamikiwa, watendaji ambao haswa ndiyo jukumu lao, wapewe miongozo na wahimizwe kuifuata na wenyeviti wakiwa ndiyo wasimamizi wao wahakikishe wananchi wao wanahudumiwa inavyostahili.