Shinikizo la juu la damu husababisha upofu, kifo

Muktasari:

Kila kukicha idadi ya maradhi haya ambayo yapo kwenye kundi la yasiyo ya kuambukiza huongezeka. Jinsi ulivyo baada ya kuathiri mfumo wa damu na husababisha madhara sehemu mbalimbali za mwili yakiwamo macho.

Shinikizo la juu la damu (hypertension) ni miongoni mwa maradhi yanayoendelea kuwapata watu wengi nchini na duniani kwa ujumla.

Kila kukicha idadi ya maradhi haya ambayo yapo kwenye kundi la yasiyo ya kuambukiza huongezeka. Jinsi ulivyo baada ya kuathiri mfumo wa damu na husababisha madhara sehemu mbalimbali za mwili yakiwamo macho.

Kwa vile huanzia kwenye mfumo wa damu madhara yake kwenye macho huhusisha mishipa ya damu iliyo ndani ya jicho hususan sehemu ya ndani ya ukuta wa nyuma inayoitwa retina.

Kazi kubwa ya retina ni kupokea mwanga wenye taswira na kuubadilisha kwenda kwenye mfumo utakaowezesha taswira kusafirishwa mpaka kwenye ubongo kwa ajili ya kutafsiriwa.

Shinikizo la juu la damu husababisha kuta za mishipa ya damu kutanuka ikiwamo iliyomo kwenye retina. Kadri kuta za mishipa ya damu inavyotanuka ili kukabiliana na ongezeko la msukumo wa damu kutoka kwenye moyo ndivyo inavyosababisha upenyo wa ndani ya mishipa hii ya damu kupungua.

Kupungua kwa upenyo huu hupunguza kiwango cha damu kinachoweza kupita kwenye mishipa hii. Upunguaji huu wa damu husababisha kiasi kidogo cha damu kufika kwenye retina.

Kukosekana huku kwa kiwango kinachostahili cha damu ambayo hubeba virutubisho na hewa safi na kuipeleka kwenye chembe hai hufanya uchukuaji wa uchafu kwa ajili ya kuusafirisha mpaka kwenye ogani ambazo hufanya kazi ya kuuondoa ushindikane.

Damu hii inavyopungua hupelekea ukosefu wa virubisho kwenye chembe hai zinazounda retina hivyo kusababisha retina kushindwa kufanya kazi yake sawasawa.

Retina inaposhindwa kufanya kazi vizuri husababisha mshipa maalumu wa fahamu unaosafirisha taswira kutoka kwenye retina kupeleka kwenye ubongo nao kushindwa kufanya kazi yake kama kawaida. Na matokeo yake kwa mgonjwa huwa ni kushindwa kuona vizuri.

Sababu kubwa ya kutokea kwa athari za shinikizo la juu la damu kwenye macho ni kupanda kwa shinikizo la damu kama nilivyoelezea hapo awali.

Unapaswa kufahamu kuwa madhara ya kwenye retina hutokea baada ya mgonjwa kuwa na shinikizo la juu la damu kwa muda mrefu, kwa kwa miaka kadhaa. Madhara haya kwenye retina hayatokei muda mfupi baada ya mtu kupata shinikizo la juu la damu.

Watu wenye maradhi haya kwa muda mrefu ndiyo wenye uwezekano mkubwa wa kupata madhara kwenye macho yao. Wengine wenye hatari ya kupata maradhi haya ni wale wenye shinikizo linalopanda kwa kasi na kwa kiwango cha juu sana yaani wanaopata aina ya shinikizo la juu la damu linaloitwa malignant hypertension.

Dalili

Kwa bahati mbaya, mgonjwa anapofikia hatua ya kuhisi tatizo kwenye uwezo wake wa kuona madhara huwa maradhi haya yanakuwa yameshakuwa makubwa.

Dalili ambazo wagonjwa wengi huzipata ni pamoja na kupungua kwa uwezo wa kuona, macho kuvimba na kichwa kuuma kuliko kawaida.

Nyingine ni mishipa midogo ya damu iliyopo kwenye macho kupasuka hivyo macho kuwa mekundu kama mishipa hiyo iliyopasuka ipo kwenye ukuta wa mbele wa jicho.

Baadhi ya wagonjwa huona taswira zaidi ya moja au kuona taswira kama nyota sehemu ambayo hakuna taswira hiyo kabisa.

Matibabu

Vipimo vya athari za shinikizo la damu machoni hupatikana kwenye hospitali kubwa zenye madaktari bingwa na kitengo maalumu cha macho. Ni ghali pia.

Baada ya vipimo vya daktari ambaye atatambua ukubwa wa tatizo atapendekeza tiba. Kwa kuwa maradhi husababishwa na shinikizo la damu hatua ya kwanza ni kuhakikisha mgonjwa anashushwa shinikizo hilo.

Hapa, namaanisha mgonjwa atalazimika kumuona daktari wa shinikizo la damu kwanza kabla hajatibiwa macho yaliyoathirika.

Kama madhara siyo makubwa, kushusha shinikizo kutasaidi kuokoa kutopotea kwa uwezo wa macho ya mgonjwa kuona.

Endapo madhara kwenye macho ni makubwa na chembehai za kwenye retina zimekufa, hakuna tiba ya kurejesha uwezo wa macho kuona tena. Kwa kifupi utakuwa umepoteza uwezo wa kuona vizuri au kutoona kabisa.

Madhara

Kupoteza kabisa uwezo wa kuona ni madhara makubwa ambayo mgonjwa anaweza kuyapata. Hii hutokea baada ya mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye retina kuziba kabisa.

Hali hii husababisha retina kukosa damu kabisa hivyo chembehai zinazotengeneza retina hufa kwa ukosefu wa virutubisho na hewa safi. Hali hii inapotokea mgonjwa hupoteza kabisa uwezo wake wa kuona kwa siku zote za maisha yake zilizosalia.

Utafiti unaonyesha watu wenye madhara haya huwa na uwezekano mkubwa wa kupata kiharusi ikilinganishwa na watu enye shinikizo la damu ambalo halijaathiri macho kwa mgonjwa husika.

Licha ya madhara hayo, utafiti unaonyesha wagonjwa walioathirika macho kutokana na shinikizo huwa kwenye hatari zaidi ya kupata mshtuko wa moyo.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba kutanuka kwa kuta za mishipa ya damu hutokea kwenye mishipa yote hata ile inayopeleka damu kwenye moyo suala linalomaanisha kuwa madhara yanayotokea kwenye retina huweza kutokea kwenye moyo na kuufanya ushindwe kufanya kazi.

Kinga

Namna pekee ya kujikinga na maradhi haya ni kuhakikisha unachukua tahadhari za kuepuka shinikizo la juu la damu kwa kubadili mfumo wa maisha hasa kwa kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta na chumvi nyingi.

Kufanya mazoezi maramara na kuwa makini na uzito wa mwili pamoja na kuepuka kitambi ni nyingine ambayo itakusaidia kujiondoa kwenye uwezekano wa kupata maambukizi ya shinikizo linaloweza kuua macho yako.

Kwa wenye shinikizo la damu, inashauriwa kumuona daktari bingwa wa macho kwa ajili ya vipimo mara kwa mara. Ni vyema kufanya hivi ili kugundua tatizo mapema kabla ya kupoteza uwezo wa kuona