Shule zinazotumia Kiingereza ziboreshe ufundishaji wa Kiswahili

Muktasari:

  • Katika ngazi ya vyuo vikuu, wale wanaoamua kuchukua kozi za Kiswahili au zinazohusiana na Kiswahili, huendelea na somo hilo.

Kwa mujibu wa miongozo ya elimu inayotumiwa nchini, Kiswahili kinapaswa kufundishwa katika viwango mbalimbali vya elimu kama somo hususan katika shule za msingi na sekondari.

Katika ngazi ya vyuo vikuu, wale wanaoamua kuchukua kozi za Kiswahili au zinazohusiana na Kiswahili, huendelea na somo hilo.

Katika makala haya, lengo letu ni kuangazia ufundishaji wa Kiswahili katika shule za msingi zinazotumia mfumo wa Kiingereza katika ufundishaji.

Shule hizi hutumia lugha ya Kiingereza katika ufundishaji wa masomo yote na Kiswahili hufundishwa kama somo.

Hata hivyo, kwa kuwa katika shule hizo msisitizo mkubwa ni kuwawezesha wanafunzi kujua Kiingereza, Kiswahili hupigwa vita kwa namna mbalimbali. Mosi, wanafunzi huzuiwa kukiongea katika mazingira ya shule na ikiwezekana wawapo nyumbani kwao ikiwa shule wanazosoma ni za kutwa. Pamoja na namna nyingine za kukipiga vita Kiswahili, namna mbaya zaidi ni ile ya kutokipa kipaumbele katika jambo lolote katika shule hizo.

Mathalani, ni utaratibu kwamba mwalimu anayefundisha somo fulani hana budi kuwa na ujuzi wa kitaaluma katika somo husika.

Ujuzi huo kwa kawaida unathibitishwa na cheti cha mwalimu huyo kwamba alisoma somo hilo na kufuzu vizuri katika somo lenyewe na methodolojia au mbinu a ufundishaji wake.

Katika shule nyingi zinazotumia mfumo huo wa Kiingereza, uzoefu unaonyesha kwamba mambo ni tofauti katika ufundishaji wa somo la Kiswahili. Mwalimu yeyote anayejua kuongea Kiswahili hupewa jukumu la kufundisha.

Kwa sababu hiyo, ufundishaji huo hufanyika bila kuzingatia weledi. Matokeo yake mwalimu husika hufundisha Kiswahili kwa mazoea. Aidha, kwa kuwa somo hilo si fani ya mwalimu huyo, ufundishaji hufanyika bila kuwekewa msisitizo na mbaya zaidi wanafunzi hushindwa kumuelewa mwalimu kama huyo.

Matokeo ya kutolielewa somo hilo ni kutolipenda na kuliona kuwa gumu. Kwa uzoefu wetu, wanafunzi wengi wanaojiunga na sekondari wakiwa wametokea katika shule za msingi zinazofundisha kwa mfumo wa Kiingereza, huwa hawakimudu Kiswahili ipasavyo. Pamoja na hilo wanafunzi hao huwa na kasumba dhidi ya Kiswahili. Huliona somo hilo kuwa halina manufaa yoyote kwao.

Bahati mbaya iliyoje, pamoja na kukidharau Kiswahili miongoni mwao hata Kiingereza huwa hawakimudu. Kwa sababu hiyo huwa hawakijui Kiingereza wala Kiswahili. Katika hilo ni nani wa kulaumiwa? Ni wazi kwamba uongozi wa shule unapaswa kulaumiwa.

Kwa kuwa lengo la kufundisha ni kutoa elimu, ipo haja ya shule hizo kuyapa uzito masomo yote. Walimu wanaopangiwa kufundisha Kiswahili wawe wenye weledi na waliofuzu vizuri katika somo hilo.

Mwalimu ambaye hakusomea kufundisha Kiswahili asipewe jukumu la kufundisha Kiswahili. Halikadhalika, wanafunzi wapewe msisitizo wa kukazania masomo yote. Vilevile, ile dhana ya kuwaaminisha watu kwamba kujua Kiingereza ndiyo kuelimika haina budi kuepukwa. Linalotakiwa ni kwamba, wanafunzi wakazaniwe kuyaelewa masomo yote vizuri. Wakuu wa shule na wamiliki wa shule wanapaswa kulimakinikia jambo hili.

Mamlaka husika za Serikali zinapofanya ukaguzi shuleni, ziangalie pia jambo hili. Walimu wanaofundisha masomo mbalimbali wawe na weledi na masomo hayo.