MAONI YA MHARIRI: Siasa hizi Arusha hazina tija kwa wananchi, Taifa

Muktasari:

Kiini cha mvutano huo ambao sisi tunaamini ni wa kujitakia, ni sintofahamu iliyojitokeza Oktoba 18 wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa hospitali ya kinamama na watoto, mradi unaoelezwa kugharimu Sh9 bilioni.

Tangu juzi kumekuwapo na mvutano wa kisiasa kati ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Kiini cha mvutano huo ambao sisi tunaamini ni wa kujitakia, ni sintofahamu iliyojitokeza Oktoba 18 wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa hospitali ya kinamama na watoto, mradi unaoelezwa kugharimu Sh9 bilioni.

Gazeti hili liliandika kuwa siku hiyo Lema alionekana kukerwa na hotuba iliyokuwa ikitolewa na RC Gambo akimtuhumu kupotosha ukweli kuhusu mchakato wa ujenzi wa hospitali hiyo.

Hii siyo mara ya kwanza kwa watendaji wa Serikali jijini Arusha, hasa wateule wa Rais kukwaruzana na wanasiasa.

Wafuatiliaji wa mambo katika mkoa huo wanajua kuhusu uadui mkubwa uliopo kati ya madiwani wa Chadema na ofisi ya mkurugenzi wa jiji la Arusha kuhusu malipo ya posho.

Lakini, hata mafahari hao wa sasa wa siasa za Arusha, miezi michache iliyopita waliwahi kukwaruzana mbele ya Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo wakati huo Gambo akiwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Inawezekana kila upande una hoja zenye umadhubuti kuhusu inachokiamini katika msuguano huo, lakini tunajiuliza nini kinachokwamisha pande zote kukaa mezani na kujadili tofauti zao kwa busara kwa minajili ya kuchochea maendeleo na ustawi wa wananchi?

Kinachoendelea Arusha kati ya wanasiasa wa upinzani na watendaji wa Serikali ni kila upande kutunisha msuli, hali inayozidi kuchochea ukinzani usio na mantiki wala tija.

Mgogoro wa RC Gambo na Lema ambaye ni mwakilishi wa wananchi ambao sisi tunasema ni wa kujitakia, unadhihirisha kwa kiwango kikubwa namna mioyo ya Watanzania isivyo kuwa pamoja katika masuala ya maendeleo.

Aidha, ni mgogoro unaothibitisha kuwa pamoja na kutofautiana kwenye itikadi za kisiasa, bado hatujawa tayari kufanya kazi kwa pamoja kwa minajili ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Kinachoendelea mkoani Arusha, ni picha ya wajenzi wanaogombea fito ilhali wanajenga nyumba moja.

Tunawaomba na kuwashauri viongozi wa Arusha na maeneo mengine nchini kuziweka kando itikadi na tofauti zao binafsi, kwani wanachotaka wananchi ni maendeleo. Misuguano hii haina tija siyo kwa Arusha pekee bali nchi nzima kwa jumla.

Ndiyo maana, tunazisihi mamlaka za juu zijitokeze kukemea hali hii na kuandaa mazingira bora ya kuzizuia ili zisitokee tena si Arusha bali katika maeneo mengine.

Kwa mfano, ofisi ya Rais inaweza kuwa mamlaka ya kwanza kuingilia kati mgogoro huu, hasa kwa kuzingatia kuwa Rais John Magufuli amewahi kutamka kuwa hapendi kuona mtu yeyote akimchelewesha kutekeleza ahadi za kuwaletea wananchi maendeleo.

Huu ni wakati wa kila mtu kuwajibika, hasa tukikumbuka kuwa kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni ‘Hapa Kazi Tu’.

Misuguano hii iachwe, isiturudishe nyuma kwa kutumbua majeraha ya uchaguzi uliopita.

Tunashauri, kila mtu kwa nafasi yake, atumie kaulimbiu hiyo ya Rais Maguguli kuwajibika ipasavyo kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Tunawashauri viongozi hawa kuwajibika huku wakiongozwa zaidi na busara, siyo jazba zao binafsi ambazo wakati mwingine zinatia aibu nchi hii ambayo imejiainisha siku zote kuwa kisiwa cha amani, utulivu na mshikamano.

Tunawasihi, viongozi hao wawili, RC Gambo na Lema watoke hadharani, waombe radhi kwa aibu wanayoitia nchi.