Siasa katika filamu

Muktasari:

Wengine wakilalamika kuibiwa kazi zao, wapo wanaolalamika kuibiwa fedha kwa kununua kazi zisizo na ubora, huku wengine wakilalamika kuwa na filamu nyingi lakini soko limedorora.

Malalamiko katika sekta ya filamu yamekuwa mengi na yanazidi kuongezeka kila kukicha.

Wengine wakilalamika kuibiwa kazi zao, wapo wanaolalamika kuibiwa fedha kwa kununua kazi zisizo na ubora, huku wengine wakilalamika kuwa na filamu nyingi lakini soko limedorora.

Malalamiko haya yote yanayoumiza kichwa na kuchosha ni ya wasanii kudai wanafanya kazi, lakini hawapati faida kutoka na kuwapo kwa watu wanaodurufu kazi zao na wanaonufaika zaidi yao.

Alipofariki aliyekuwa mkali wa filamu, Steven Kanumba kuliibuka mambo mengi, ikiwamo kutokuwa na filamu yake mwenyewe licha ya kuigiza kwa miaka mingi.

Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff) Simon Mwakifwamba anasema waigizaji wanaopaswa kulalamika kuibiwa kazi zao ni asilimia 20 pekee.

Anasema asilimia 80 wanauza kazi zao kabla hazijatoka na miongoni mwa masharti wanayopewa na yanawaumiza bila kujua ni kuuza kazi zao, hati miliki na hati bunifu.

“Anayepaswa kulalamika kuibiwa ni wanayemuuzia kazi, siyo wao kwa sababu hawana mamlaka nazo, ndiyo maana ni ngumu kuwaona wakijitoa mhanga hata kuzikamata kwa sababu hawana kazi,” anasema Mwakifwamba.

Mwakifwamba anafafanua licha ya Taff kuwa na majukumu makubwa matatu, ikiwamo kufuatilia sera za nchi zinamsaidiaje msanii, zina faida gani kwake na hasara.

Analitaja jukumu lingine ni utetezi wa tasnia yenyewe na wanatasnia na kuwajengea uwezo kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali, kutunza fedha na masuala ya uchumi kwa ujumla.

Anasema licha ya kupata mafunzo hayo bado kuna waigizaji wanamuamini Muhindi (jina maarufu walilobatizwa wasambazaji wa filamu) kwa asilimia 100 kitu ambacho kinakwamisha kuwatoa katika kundi la wanaonyonywa.

“Wapo wanaoelewa taratibu, lakini wengine hawana uvumilivu wa njaa na wanaona ngumu kufanya kazi bila kuuza kwa Muhindi, ”anasema.

Mwakifwamba anasifia hamasa iliyokuwapo kwa wasanii kujiunga katika vikundi ambavyo vinajiunga na shirikisho hilo.

Anasema hadi sasa kuna vyama vya waigizaji tisa ambavyo vipo hai kwa wingi wa wanachama na kutambua nini kinatakiwa kufanyika vipo sita.

Mwigizaji Single Mtambalike “Rich” anasema kuiba ni kuiba haijalishi anaibiwa Mhindi au msanii.

Anafafanua kuwa masuala hayo ya wizi wa kazi za wasanii siyo madogo kama yanavyozungumzwa ni makubwa na inaonekana hata Serikali ni kama yamewashinda.

Nini kiini hasa?

Anasema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameziwekea kazi za wasanii wa ndani stika na kuziacha kazi za wasanii wa nje zikitamba mitaani bila kulipa ushuru.

Anafafanua: “Mtu ananunua filamu ya nje ina kila kigezo cha ubora tena inauzwa Sh1,000, atapata hamu ya kununua ya ndani yenye changamoto nyingi zikiwamo rangi hafifu, usikivu duni, maudhui yasiyokuwa na jipya kwa Sh2,500?”

“Nakuambia biashara hii inakufa, Serikali kupitia TRA walifunga maduka yanayouza kazi za nje kwa kuweka makufuli, tunavyozungumza hapa yametolewa na wamefunguliwa kesi ya kuhoji kukamatwa kwao, ”anasema Rich.

Rich anasema kama Serikali imeshindwa na haiwezi kulizungumzia hilo kwa sasa kwa sababu kesi ipo mahakamani msanii wa kawaida hataweza.

Anasema wasanii wa muziki wa kizazi kipya waliacha kutayarisha albamu, lakini wanapata fedha kidogo kwa shoo wa filamu wakiacha tasnia itakuwa imekufa kabisa.

Anafafanua kuwa hata hao wanaoitwa Wahindi watachoka kwa sababu ananunua masta ya filamu kwa Sh30 milioni halafu afanye matangazo auze bado wezi wa kazi wafanye yao. “Wataacha kwa sababu watauza wapi na watamuuzia nani, vita hii ifanywe kama ya dawa za kulevya kwa sababu ni kubwa, ”anasema.

Rich anasema Taff imejitahidi kuunganisha wasanii, lakini haina meno ya kushughulikia suala hili kwa sababu hawana meno ya kupambana na watu waliojikita na kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuibia wasanii.

Starehe imebaini suala hili linashughulikiwa na watu wasiofahamu huu mchezo wa wizi wa kazi ulivyo ndiyo maana maamuzi mengi yamekuwa adui kwa msanii badala ya kuwa msaada.

Akizungumzia wezi wa kazi za wasanii na jinsi ya kuwadhibiti Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kwa kushirikiana na Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni , Nape Nnauye watahakikisha kazi za sanaa kutoka nje zinalipa kodi kubwa kuliko za ndani.

Alisema kazi za nje zikitozwa kodi kubwa za ndani zitakuwa na soko hivyo kuwasaidia wasanii wa ndani kunufaika na kazi zao.

Suala hili halihitaji siasa

Starehe inaunga mkono juhudi hizo, lakini swali ni je? Kutoza kodi kubwa kazi za sanaa kutoka nje kutakuwa suluhisho?

Hakuwezi kuwa suluhisho zaidi ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya biashara na kupata faida kubwa wanaodurufu kazi za wasanii.

Kama kilio ni kazi za nje kulishika soko kutokana na kuuza kazi kwa bei ya chini huku zikiwa hazitozwi kodi na kazi za wasanii kuibwa kuna haja ya kushughulikia hivi vitu kwa pamoja.

Kumekuwa na maneno mengi kutoka kwa wahusika wakuu wa suala hili wakiwamo viongozi wa Wizara husika na waziri mwenye dhamana, wakuu wa mikoa, wilaya kuwa watawakamata, lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyefanikiwa hata kwa asilimia moja zaidi ya kurasimisha kazi na kutoza kodi.