Sifa kuu tatu anazopaswa kuwa nazo mwanaume

Muktasari:

  • Moja miongoni mwa mambo mengi yanayounda mwanaume ni tabia au uwezo wa kujibu; kujibu haina maana kwamba kutoa majibu wakati wa mazungumzo. Hapana. Kujibu huku ni kunamaanisha kuwa na jawabu la kila linalokuja mbele yako kama mwanaume — tena jawabu lenye manufaa kwa anayestahili kunufaika, jawabu lenye kujenga.

Ukiweka pembeni suala la jinsia, kuna vitu vingi vinavyounga mkono mtu kuwa mwanaume. Kila mwenye jinsia ya kiume anaweza kuwa mwanaume, lakini sio wote wenye uwezo wa kuwa wanaume wanaostahili kuitwa wanaume.

Tunachokifanya leo sio kukupa maana ya mwanaume! Hapana. Hiyo ipo ambayo haitabadilika miaka nenda rudi. Tunachokifanya hapa ni kuipa changamoto akili yako kama binadamu mwenye jinsia ya kiume, ili utengeneze tafsiri ya neno mwanaume ambayo kwanza itakuwa inaendana na nyakati tulizonazo lakini pia ambayo hata mwenyewe ukijiambia peke yako utaona namna inavyokuingia na kukubaliwa na nafsi yako na ikiwezekana hata ilingane na mitazamo ya wengi.

Moja miongoni mwa mambo mengi yanayounda mwanaume ni tabia au uwezo wa kujibu; kujibu haina maana kwamba kutoa majibu wakati wa mazungumzo. Hapana. Kujibu huku ni kunamaanisha kuwa na jawabu la kila linalokuja mbele yako kama mwanaume — tena jawabu lenye manufaa kwa anayestahili kunufaika, jawabu lenye kujenga.

‘Mama anaumwa’ unatakiwa uwe na jawabu, ‘binti yako kapata ujauzito akiwa shule’ unatakiwa uwe na jawabu, mkeo kasimamishwa kazi lazima uwe na jawabu na kila kitu kingine kinachotokea kwenye maisha ya wanaokutazama kama mwanaume wa kutegemewa— yaani watoto, mke, mama, wakwe, dada, kaka, bosi na zaidi.

Sifa nyingine inayounda mwanaume ni kutazama ndani. Kutazama ndani maana yake ni kwamba, kabla mwanaume hajashughulika pointi namba moja, yaani hajajibu kile alicholetewa au kilichotokea kwake, huanza kwa kushughulikia na kuangalia undani kinapotokea kile alichotupiwa. Mtoto akisema ‘baba nataka nihamishe shule’, baba hamuamishi mtoto tu wala hazuii kutokumhamisha, badala anatazama ndani ya mtoto, ili kuona kilichomsukuma mtoto kutaka kuhama shule.

Je, ni kwa sababu hakuna marafiki anaowapenda, shule haifundishi vizuri au ni mtoto tu hataki kusoma tu. Vyote vinawezekana, na vinapatikana tu ikiwa mwanaume ataamua kuingia ndani.

Hii ndiyo inawasukuma hata wanaume wengine kuwa na uwezo mkubwa wa kusuluhisha shida zinapotokea kati yake na mkewe; yaani mfano mwanamke kakuta meseji ambazo hakutakiwa kuzisoma, na akauliza Joyce ndiyo nani.

Wanaume wanaotazama ndani hawajibu tu, wanaingia kwanza ndani ya mke na kuelewa nini kinachoendelea, na wanapotoka wanakuja na jibu ambali linakuwa una uwezo wa kupunguza ‘ngori’ hata kwa asilimia 50.

Kingine, wanaume wanachukua hatua, mwanaume hasimami tu, wanafanya jambo. Akishajua mke anataka kuacha kazi kwa sababu labda anashindwa kumudu majukumu ya kazini na nyumbani, mwanaume huchukua hatua kulingana na mtazamo wake na uwezo aliokuwa nao. Yaani aidha apatikane dada wa kazi na mke aendelee na kibarua au mke aachane na ajira aelee familia.

Mwanaume anajengwa na mambo mengi sana, na sifa kuu ya mwisho ni kutafuta kuwa mwanaume wa ukweli. Kuchunguza viwango gani unatakiwa uwe navyo ili tukuite mwanaume. Unaweza kuanza hili kuanzia sasa hivi.