Sifa na faida za darasa linaloongea

Muktasari:

Ni darasa  linaloongeza thamani, mtazamo chanya, furaha na amani ya akili ya mwanafunzi.

Darasa linaloongea ni lile lenye uwezo wa kumfanya mwanafunzi ajifunze kulingana na mahitaji yake hata asipokuwapo mwalimu.

Ni darasa  linaloongeza thamani, mtazamo chanya, furaha na amani ya akili ya mwanafunzi.

Zana mbalimbali zilizowekwa katika kona za darasa hilo na zilizobandikwa, humfanya mwanafunzi apende kujifunza zaidi na kuhudhuria shuleni bila kukosa.

Mkufunzi na mwezeshaji  kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Aisha Gguhiya anaeleza kuwa darasa linaloongea ni darasa  lililosheheni zana za kujifunzia na kufundishia.

Darasa hilo linaweza kutofautiana kulingana na muundo wa darasa na ubunifu wa walimu husika.

Zana zilizomo katika darasa hilo zinaweza kuwa katika mfumo wa picha za kuchorwa, picha za kubandikwa mbegu za nafaka, vitambaa, majani ya mimea mbalimbali au mchanga.

Zikiandaliwa hubandikwa katika kuta za darasa ili wanafunzi waweze kuona. Wakati mwingine hubandikwa hata juu ya dari kulingana na ubunifu wa walimu.

Darasa linaloongea huwa na kona mbalimbali za kujifunzia. Kwa mfano, kona za ujifunzaji,  kona ya hisabati (kuhesabu), kona ya uchoraji, kona ya kuandika, kona ya kusoma na kona ya baadhi ya vitu halisi ambavyo pia husababisha mvuto kwa watoto au wanafunzi.

Pia, kunaweza kuwa na kona ya toyi midoli inayotumika kulingana na uchaguzi wa mwanafunzi mwenyewe.

Katika hili mwalimu hawachagulii wanafunzi kona ya kujifunza, bali yeye atakuwa akisimamia namna kila mwanafunzi anavyojiamulia kona anayoipenda.

Darasa hili hutoa fursa kwa mwalimu kubaini vipaji mbalimbali vya wanafunzi wake na vitu wanavyopendelea.

Darasa hili huwa na mvuto na mara nyingi imezoeleka kutumiwa na walimu wanaofundisha hususani katika darasa la kwanza, la pili na la tatu.

Walimu wengi wamekiri kuwa darasa linaloongea limewasaidia kwa kiwango cha juu kuwawezesha wanafunzi wao kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa urahisi.

 

Faida za darasa hili

Darasa linaloongea huwa na faida nyingi kwa wanafunzi, walimu na shule. Baadhi ya faida hizi ni kama ifuatavyo:

Moja, huchangia kupunguza idadi kubwa ya utoro shuleni. Mvuto wa shule na madarasa huchangia kwa kiasi kikubwa  kuwafanya wanafunzi wapende kwenda shuleni bila shuruti.

Mazingira ya kuvutia ya darasani pia huongeza thamani ya shule na wanafunzi katika jamii.

Mbili, huhamasisha elimu jumuishi. Kwa sababu watoto wenye mahitaji mbambali huweza kulitumia darasa linaloongea bila ubaguzi.

Kwa mfano, wanafunzi wenye mahitaji maalumu wasioona na wasiosikia wote huweza kulitumia na kushirikiana na wanafunzi wengine.

Tatu, humfanya mwanafunzi kuwa mbunifu. Wanafunzi wanajengwa stadi za ubunifu na kujiamini kwa sababu hupewa fursa ya kwenda wenyewe kwa hiari yao kucheza au kujifunza katika kona ya ujifunzaji.

Nne, huleta ari ya kujifunza kwa mwanafunzi. Hamasa ya mwanafunzi kujifunza huchangiwa na namna walimu wanavyoweza kufanya madarasa yao kuwa yenye mvuto.

Darasa linaloongea humfanya mwanafunzi aweze kuhusianisha anayojifunza shuleni au darasani na maisha yake halisi.

Tano, humrahisishia mwalimu kazi ya ufundishaji na ujifunzaji kwa sababu kwa kiwango kikubwa hupunguza vurugu na kelele darasani. Darasa lenye wanafunzi watulivu na wasikivu husababisha mada kueleweka vizuri.

Pia, darasa hili ambalo limeandaliwa kwa kuwekwa zana bora za kufundishia na kujifunzia, lina uwezo wa kumshawishi mtoto kutaka kujifunza zaidi.

Sita, humfanya mwanafunzi kuwa mdadisi. Mwanafunzi anapokuwa mdadisi hii, anakuwa na tabia ya kutaka kujifunza  kutoka kwa wanafunzi wenzake.

Kuna wakati wanafunzi huulizana maswali juu ya picha zilizobandikwa katika darasa lao. Kwa kufanya hivyo hukuza kumbukumbu na kuendelea na tendo la kujifunza pasipo uwepo wa mwalimu.

Mwalimu Jackline Chaula wa Shule ya Msingi Chadulu iliyoko Dodoma Mjini, anaeleza kuwa mwanafunzi huendelea kujifunza kwa ziada.

Kwa mfano, inawezekana  mwalimu anayefundisha wanafunzi wa darasa la kwanza akawa amefundisha tarakimu mpaka namba tano katika kitabu, lakini katika kuta za darasani humo akawa amebandika picha zenye vitu kulingana na namba mpaka tarakimu ya namba 10 au 20.

 

Saba, hurahisisha upimaji wa mtoto katika hatua zake za kielimu darasani. Kwa mfano, ni jambo rahisi kwa  mwalimu kupata majibu ya haraka ya aina zote za upimaji kwa kumhoji mwanafunzi kulingana na picha anazoziona darasani kila siku.

Nane, humjengea mwanafunzi hali ya uzalendo. Mwanafunzi anayesomea katika darasa lenye sifa za kuwa darasa linaloongea, hujifunza pia moyo wa kulipenda, kulithamini, kulitunza na kulilinda darasa lake.

Mwanafunzi huyu anapokuwa amejengwa moyo na ufahamu wa kutunza vitu vyake binafsi, kutunza mali za shule, kutunza mali za wenzake, akiwa mkubwa atakuwa na uwezo wa kutunza, kulinda na kupigania maliasili za taifa lake popote pale.

Kwa hiyo, faida za kuwa na darasa linaloongea ni nyingi kwa mwanafunzi, mwalimu, wazazi, shule na taifa kwa jumla. Ni wajibu wa walimu hususani wanaoweka msingi wa elimu kwa watoto na vijana, kujitoa kutimiza wajibu wao sawasawa kiuweledi ili kuwapatia wanafunzi stahiki zao.

Walimu wanasisitizwa kuongoza vitendo vya ujifunzaji na ufundishaji kwa kutumia zana mbalimbali, ili kuweza kufikia malengo ya elimu.

Walimu wanaohisi hawana uwezo wa kufanya hivyo, ni vema wakachukua hatua ya kutembelea shule mbalimbali zilizo jirani kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu.