Sifa ya chuo kikuu ni kuwekeza katika jamii

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Profesa Joe Lugala.Picha Anthony Siame

Muktasari:

  • Chuo Kikuu cha Aga Khan kupitia taasisi ya kuendeleza elimu Afrika Mashariki, siyo tu imejikita kutoa elimu bora, bali pia kuishirikisha jamii katika utoaji wa elimu hiyo.

Lengo la taasisi yoyote ya elimu hasa chuo kikuu, ni kuisaidia jamii husika. Jamii iliyoelimika hutokana na jumuiya ya wasomi waliomo na matokeo yake huonekana katika maendeleo.

Chuo Kikuu cha Aga Khan kupitia taasisi ya kuendeleza elimu Afrika Mashariki, siyo tu imejikita kutoa elimu bora, bali pia kuishirikisha jamii katika utoaji wa elimu hiyo.

Akihojiwa na gazeti hili, Mkurugenzi wa taasisi hiyo na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Profesa Joe Lugala anajivunia ubora wa elimu inayotolewa na jinsi wanavyoishirikisha jamii katika elimu.

Swali: Tueleze kuhusu wajibu wa vyuo vikuu?

Jibu: Ulimwengu mzima, chuo kikuu ni lazima kiwe kimebobea katika maeneo matatu. Lazima kiwe kimebobea kwenye ufundishaji, kuwe na wahadhiri wazuri walioelimika. Kufundisha siyo kuropoka tu, ni suala la kuhamisha ujuzi, ni lazima kuwe na uhusiano wa mwanafunzi wa walimu.

Walimu wanapaswa pia kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wanafunzi, kuna walimu wanadhani wanajua kila kitu. Wanafunzi wa vyuo vikuu ni watu wazima, wanakuja na ujuzi na uzoefu fulani. Elimu unaipata darasani na inaweza kukupotosha, lakini ujuzi ni kitu unachokipata kutoka kwenye mazoea ya jamii.

Sifa ya pili ya chuo kikuu kuwa ni kubobea katika utafiti na uandishi ili kuyatumia majibu mnayopata kuboresha mambo.

Sifa ya tatu ni lazima chuo kikuu kiwe mahiri kuhusisha jamii katika mafunzo yake. Elimu isiyo na uhusiano na jamii haina thamani. Tunataka elimu inayoangalia changamoto za jamii na iliyo tayari kubadilisha mfumo wa maisha ya wananchi.

Swali: Je, Aga Khan mnazo sifa hizo zote?

Jibu: Ndiyo. Kwa mfano sasa tuna kituo kinachoitwa Centre for Education Long Learning ambacho huifikia jamii kwa kuwafikia walimu walioko kazini.

Sasa hivi kuna watu walioko Nachingwea au Lindi wanafanya kazi na walimu walioko tayari shuleni. Tunafanya kazi na vyuo vya walimu kama vile Kitangali TTC, Nachingwea Tanzania na Rodonga na Arua kule Uganda Kaskazini.

Tunashirikiana pia na taasisi kama Kilifi na Kwale Mombasa. Tunafanya kazi eneo zima za Afrika Mashariki na hiyo ndiyo sifa ya taasisi ya elimu na maendeleo yake.

Swali: Je, shule yenu ya elimu ina jumla ya wanafunzi wangapi na mnawapataje?

Jibu: Hapa tunatoa shahada ya uzamili ambayo huchukua wanafunzi 60 tu kutoka nchi za Afrika Mashariki yaani Tanzania, Kenya, Uganda kwa mchujo maalumu.

Shahada hiyo imegawanyika katika matawi mbalimbali. Kuna wanaosoma elimu ya awali, kuna wale wanaosoma ufundishaji bora wa masuala ya sayansi na elimu, kuna wanaosoma ufundishaji wa Hisabati, uongozi na utawala kwenye elimu na kuna wale wanaosoma upimaji, tathmini na mchanganuo; lakini yote ni shahada moja ya uzamili.

Swali: Mmejipangaje kwa upande wa wahadhiri?

Jibu: Kuna walimu kati ya 15 hadi 20 ambao kimsingi hufundisha uwiano wa wanafunzi watatu au wanne, hivyo kuongeza ubora katika ufundishaji tofauti na vyuo vyenye wanafunzi wengi.

Tuna wanafunzi kutoka Kenya, Uganda na Tanzania ambao ni walimu. Wengine ni maofisa elimu huko Kenya, Uganda na wengine ni walimu wakuu wa vyuo na shule za msingi.

Swali: Taratibu za kuwapata wanafunzi zikoje?

Jibu: Hapa taratibu zetu ni ngumu. Unaweza ukawa umepata daraja la kwanza kwenye shahada ya kwanza na mwingine daraja la pili, lakini huyo wa daraja la pili akaingia.

Kwanza kabisa tunaangalia vyeti kisha tunaviwekea alama. Kama una daraja la kwanza pengine alama 15, daraja la chini una alama 10, una daraja la pili una alama pengine 5.

Halafu kuna mtihani wa Kiingereza, tunataka kujua kama una uwezo wa kuwasiliana. Hiyo inawaengua wengi. Halafu kuna uandishi wa insha, kabla ya kufanya mahojiano ya ana kwa ana.

Kwa mwaka huu waliomba wanafunzi 350, Watanzania walikuwa 180 na wengine walikuwa kutoka Kenya na Uganda.

Huwa tunaweka vituo katika miji ya nchi husika na kuwapeleka walimu wao wakiwa pia na maofisa wa wizara za elimu ili kuwahakiki.

Kwa hiyo kuna vitu vinne, unaweza kuwa na daraja la kwanza kwenye vyeti lakini Kiingereza ukakwama, ikaja kwenye mahojiano ukakwama, kwenye insha ukapata sifuri.

Akaingia mwenye daraja la pili wewe wa kwanza ukatupwa nje.

Unapokuwa na mazingira yaliyotawanyika kama hivi unayafanya kuwa ya utajiri wa elimu hasa katika utoaji wa elimu na teknolojia. Kwa sababu unakuta hapa kuna wanafunzi kutoka Kenya, Uganda, kuna Wahehe kama mimi, Wakikuyu, Baganda, wote wako pamoja.

Kwa hiyo unashirikisha huo uzoefu. Ukija kwa walimu nako kuna Wakenya, kuna Profesa wa utafiti hapa kutoka Zimbabwe, kuna Wazungu, kulikuwa na mmoja kutoka Pakistan, Ireland, Canada wengine wameondoka.

Swali: Kuna changamoto zozote zinazowakabili?

Jibu: Kuna changamoto nyingi; unajua unapofanya kazi katika nchi tofauti kuna sera tofauti hivyo inabidi uangalie jinsi ya kupita.

Kenya na Uganda wana taratibu zao. Tunajua jinsi ya kwenda nao, nimekwambia kuwa wanakuja hata kwenye usaili wetu, wanaijua miradi yetu yote. Watu wa Kenya wameshakwenda mpaka Mtwara, Watanzania wameshakwenda Mombasa.

Kama nilivyosema kuwa kuna walimu hapa kutoka nje ya nchi, hivyo kuna changamoto ya kupata vibali vya kazi, inaweza kuchukua hata miezi sita ndiyo unapata.

Swali: Unauonaje mfumo wa elimu nchini?

Jibu: Moja kabisa tangu tulipopata uhuru, sera za nchi kuhusu elimu zimekuwa zikibadilika. Kwa hiyo kwa miaka 50 au 60 tangu tupate uhuru, kumekuwa na mabadiliko mengi ya sera kiasi kwamba hata wafundishaji, walimu, wanachanganyikiwa, hawaelewi.

Tukitaka kuendelea, lazima tukubaliane, tunataka elimu ya namna gani na tutaipata kwa njia ipi.

Sera nyingine za elimu zimekuwa na utata, kwa mfano suala la lugha mpaka leo halijapatiwa ufumbuzi. Darasa la kwanza mpaka la saba Kiswahili.

Sawa ni lugha ya Taifa, tuna haki kuiendeleza na tumefanya vizuri kuiendeleza. Lakini unaanza kidato cha kwanza Kiingereza, huko shule ya msingi kinafundishwa kama lugha ya kigeni.

Huo utaratibu hauna ubaya, lakini kinachotakiwa kama unajua Kiingereza kinaanzia kidato cha kwanza, ni lazima uzalishe walimu wazuri wa kufundisha Kiingereza ili uelewa wa Kiingereza na Kiswahili viende sambamba.

Changamoto nyingine ni walimu; ni lazima wapewe motisha, walipwe vizuri ili kuboresha elimu. Lazima tuwe na mitalaa inayoakisi jamii, inayowasaidia watu kuelewa matatizo ya nchi na namna ya kuisaidia nchi itoke kwenye matatizo hayo.

Unapozungumzia kuboresha elimu, uwekezaji ni muhimu na ni lazima kila mtu achangie. Serikali itoe mchango wake na wananchi pia. Ukitegemea Serikali peke yake, hufiki popote.