Siku 10 hifadhini, changamoto gharama za utalii nchini

Muktasari:

  • Nilisafiri salama mpaka Dar es Salaam na kufika kwa wakati. Saa 12:45 ya siku iliyofuata nilichukua usafiri kutoka Sinza nilikofikia kuelekea Mbezi Goigi ambako tulipanga kukutana na wenzangu kabla ya kuelekea Bagamoyo mkoani Pwani  ambako tungemkuta Mussa Mandia, kiongozi wa msafara wetu. Kwa usafiri teksi, nililipa Sh15,000.

Nilianza safari ya kutoka Songea mkoani Ruvuma kuelekea Dar es Salaam kuungana na waandishi wenzagu kwa ajili ya kutembelea hifadhi za Taifa zilizo chini ya Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa).
Nilisafiri salama mpaka Dar es Salaam na kufika kwa wakati. Saa 12:45 ya siku iliyofuata nilichukua usafiri kutoka Sinza nilikofikia kuelekea Mbezi Goigi ambako tulipanga kukutana na wenzangu kabla ya kuelekea Bagamoyo mkoani Pwani  ambako tungemkuta Mussa Mandia, kiongozi wa msafara wetu. Kwa usafiri teksi, nililipa Sh15,000.
Saa 1:30 asubuhi nilikuwa nimefika na tukaanza safari ya kuelekea Bagamoyo kwa kutumia usafiri binafsi wa mwanahabari mwenzetu, Irene Mark. Tulipofika Bunju tulimchukua Esther Macha ambaye alikuwa mkuu wa msafara na kuwasili Bagamoyo saa 3:47.
Tulifikia Hoteli ya  DZ ambako tulipata kifungua kinywa wakati tukiwasubiri waandishi wengine kutoka mkoani Kigoma. Ilipotimu saa tano asubuhi safari  yetu ilianza rasmi kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Saadan, umbali wa kilomita 60 tukitumia magari mawili ya Tanapa.
Tuliwasili salama Saadan na kupokelewa na mhudumu mcheshi na aliyevaa nadhifu. Alijitambulisha kuwa ni Apaikunda Mungule, mhifadhi utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Saadan.
Alitutembeza kwenye vyumba vya wageni na kuhifadhi mizigo yetu na kurudi kwenye ukumbi wa chakula ambako tulipata mlo  kisha kutawanyika kuelekea kwenye hifadhi kujionea wanyama waliopo.
Utalii
Hifadhini tulikuwa na mwongozaji watalii kijana Richard, mkarimu kama  alivyokuwa dereva, Mussa.Ukarimu ni sifa ya wahudumu wa hifadhi hii. Ulitufanya tuwe huru kuuliza maswali na kujifunza zaidi: Richard alitueleza sifa za kila mnyama tuliyekutana naye kama vile simba na kwamba simba dume huchagua jike kutoka kwenye kundi la zaidi ya majike 20  na kupumzika naye kwa siku saba mfululizo.

Ikitokea dume hilo limempenda jike mwenye watoto huwaua na kuanzisha kizazi chake.Hufanya hivyo kwa kuhofia uhusiano wake kupungua kutokana na kuwapo kwa watoto hao.

Tulijifunza tabia za wanyama mbalimbali na kushuhudia makundi ya swala, twiga, ngiri, pundamilia na nyati. Tulibahatika kuwaona korongo, nyoka wa aina tofauti, mbawala na misitu mizuri yenye ndege wa rangi za kuvutia bila kusahau miti mikubwa ya mibuyu na ukwaju inayopamba hifadhi hiyo.

Saa nane mchana tulirejea kambini. Tukiwa hapo, nyani wakirandaranda. Baada ya chakula cha mchana tulikwenda kupunga upepo mwanana wa Bahari ya Hindi.

Siku ya pili, tulielekea Bahari ya Hindi kilomita 10 kutoka kambini hapo. Njiani tuliendelea kuona wanyama na mara kadhaa tulikutana na watalii kutoka mataifa mbalimbali.

Ufukweni mwa bahari hiyo, Apaikunda alituonyesha Mto Wami unapomwaga maji yake. Tuliona misitu ya mikoko, nyani na ndege wa majini bila kusahau makutano ya mto na bahari; maji chumvi na baridi yanapochanganyika.

Tukiwa baharini tuliona makundi ya viboko na mamba baadhi wakiwa majini na wengine nchi kavu. Niliogopa kwani walikuwa wakizama na kuibuka mara kwa mara na kusababisha waandishi wote tukae kimya.

Apaikunda alibaini hilo hivyo alitutoa hofu na kueleza kuwa, tupo salama na viboko wala mamba hawawezi kutufanya kitu chochote. Alitueleza kwamba kiboko anakula nyasi na ngozi yake haipatani na jua, ndiyo maana muda mwingi hasa kukiwa na jua kali huzama ndani ya maji au kwenye matope.

“Viboko wanaishi katika familia na huwezi kukuta wamechanganyika na familia nyingine,” anasema Apaikunda.

Baada ya mzunguko baharini, tuliporejea kambini ambako Mhifadhi wa Ikolojia na Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Saadan, Lomi ole Meikasi anatupokea na kutupa historia fupi ya hifadhi hiyo.

“Hii ni moja kati ya hifadhi 16 za taifa yenye vivutio vingi. Imejaliwa kasa zaidi ya 3,000 wa rangi ya kijani, ambao hutaga mayai kwenye ufukwe wa Madete wenye eneo la kilomita nane za mraba,” anasema.

Anatueleza jina la hifadhi hiyo kuwa limetokana na Kijiji cha Saadan ambacho kilikuwa eneo la kihistoria lililoanzishwa na wavuvi wa pwani hiyo kwenye karne ya 19, kila walipokuwa wanapumzika baada au kabla ya kwenda kuvua.

Tulifahamishwa kwamba hifadhi hiyo imepakana na mikoa ya Pwani na Tanga ikipita kwenye wilaya za Bagamoyo, Pangani na Handeni ambazo zinanufaika na mapato yatokanayo na ongezeko la watalii kila mwaka.

Iridhihirishwa kwamba idadi ya watalii hasa kutoka Marekani, imekuwa ikiongezeka kutoka 3,758 mwaka 2005 hadi 490,000 mwaka 2015.

Saadan ilipandishwa hadhi kutoka pori la akiba na kuwa hifadhi kamili mwaka 2005, ni pekee inayopakana na Bahari ya Hindi nchini. Watalii wanaweza kufika kwa kutumia barabara au baharini kwa maboti na usafiri mwingine.

Kati ya wanyama watano maarufu big five; simba, tembo, twiga, nyati anakosekana faru pekee hifadhini humo. “Saadan ni hifadhi nzuri ambayo inawavutia kasa kutoka India kuja kutaga mayai yao katika ufukwe wetu,” anasema Meikasi.

Kutokana na kuimarika kwa watalii na mapato yanayopatikana, hifadhi imetoa zaidi ya Sh722.83 milioni katika miradi 22 ya maendeleo ya kujenga ujirani mwema katika vijiji vinavyoizunguka.

Miradi hiyo ni ujenzi wa zahanati, madarasa na mchango wa madawati 150,000 katika shule za misingi za vijiji vya mikoa inayopitiwa na Saadan. Katika miradi 22 iliyotekelezwa kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2015; Wilaya ya Pangani imepata miradi saba, Handeni mitatu, Chalinze minne na Bagamoyo minane.

Hifadhi ya Mikumi

Baada ya kutalii Saadan tulielekea Hifadhi ya Mikumi ambako tuliwasili saa nne asubuhi na kupokelewa na Mkuu wa Hifadhi hiyo, Donat Mnyagatwa ambaye tulizungumza naye.

Anasema hifadhi hiyo inakabiliwa na changamoto ya wanyama kugongwa na magari mara kwa mara kwenye Barabara ya Iringa iliyopita ndani ya hifadhi hiyo ikitokea Dar es Salaam.

“Kwa wastani kila siku, mnyama mmoja hugongwa,” anasema Mnyagatwa.

Barabara hiyo inaiunganisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Dar es Salaam ambalo ni jiji la biashara na nchi zinazopakana na Tanzania, zilizopo kusini-magharibi huku ikipitisha wastani wa magari 2,000 kwa siku.

Kutokana na changamoto zinazotokana na uwapo wa barabara hiyo, baadhi ya wanyama adimu wanatishiwa kutoweka katika hifadhi. Takwimu zinaonyesha kwa miaka mitano iliyopita hadi mwaka 2015 zaidi ya wanyama 3,000 walikufa baada ya kugongwa na magari binafsi, mabasi ya abiria au malori.

Kudhihirisha kukithiri kwa matukio hayo, Mnyagatwa analinganisha kipindi hicho na miaka iliyopita kwamba 1992 wanyama 72 waligongwa idadi ambayo imekuwa ikiongezeka kila mwaka na 2015, wanyama 237 walikufa kwa kugongwa.

“Kilomita 50 kati ya 3,230 za barabara hii kutoka Tanzania mpaka Zambia imepita hifadhini. Urefu huu unaweza kuonekana ni jambo dogo, lakini unapoteza baadhi ya aina ya wanyama,” anasema Mnyagatwa.

Licha ya kupoteza wanyama hao, uchafuzi wa mazingira kutoka kwa abiria wa kwenye magari yanayopita hifadhini humo, anasema: “Utalii wa bure unaofanywa nao unapoteza mapato mengi ya Serikali.”

Yapo masuala mengine yanayojitokeza kutokana na vitendo vya abiria wanaokuwamo kwenye magari yanayopita Mikumi.

Licha ya ujangili na kuzuka kwa moto, tabia za baadhi ya wanyama zimekuwa zikibadilika kutokana na kurushiwa matunda au vyakula vya binadamu na kuota kwa mazao yanayomwagika yakisafirishwa kupitia barabara hiyo.

Baada ya kumaliza mahojiano, tulitembezwa kwenye vyumba vya kulala wageni na hotelini. Kilichonifurahisha zaidi ni kuona vyote vikiwa na hali nzuri licha ya kutofautiana gharama. Vya hadhi ya juu bei yake ilikuwa Sh100,000 wakati vile vya kati ni 50,000, huku vikiwapo vya kati ni Sh20,000 na 30,000. Ili kuepuka udanganyifu, vyumba vya kati na chini kila kichwa kinatakiwa kulipia hata kama ni mtu na mwenzi wake.

Licha ya Saadan na Mikumi tulikotalii kwa siku mbili mbili, tulikwenda Udzungwa kisha Ruaha tulikotumia siku tatu kila moja. Kote tulipokelewa vizuri na watu wakarimu na wenye upendo kwa wageni.

Gharama

Uzoefu wangu kwenye ziara hiyo unaonyesha watu wengi wanaotembelea hifadhi nchini, wanatumia ama usafiri binafsi au magari ya kutembeza watalii ambayo gharama zake zipo juu kidogo.

Wakati Serikali ikiweka mkakati wa kuvutia watalii zaidi ya milioni tatu kwa mwaka kuanzia mwakani kutoka zaidi ya milioni 1.2 waliokuja nchini mwaka 2015, ipo haja ya kuimarisha miundombinu ya usafiri inayokwenda kwenye vivutio vilivyopo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi anasema Serikali imepunguza bei kwa watalii wa ndani na inaendelea kuboresha miundombinu hiyo.

“Upo mpango wa kutumia reli ya Tazara kwenda Hifadhi ya Selous na kuongeza safari za promosheni za kutembelea vivutio vilivyopo kutoka kwenye miji mikubwa,” anasema Jenerali Milanzi.

Pamoja na hayo yote, anashauri Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea na kufahamu vivutio vilivyopo nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri amewahi kushauri ujenzi wa reli kwenda kwenye mbuga, hifadhi na uanzishaji wa mabasi yatakayokuwa yakifanya safari zake kutoka miji mbalimbali kwenda kwenye vivutio.

“Ni gharama kubwa kwa Mtanzania kufanya utalii nchini. Licha ya kushusha kiingilio, miundombinu isiporahisishwa haitasaidia. Reli na mabasi ni suluhu ya kudumu,” anasema Erick.