Wednesday, March 15, 2017

Siku urais wa Trump zinahesabikaRais Donald Trump

Rais Donald Trump 

By Joster Mwangulumbi, Mwananchi jmwangulumbi@tz.nationmedia.com

Moshi mzito unafuka katika Ikulu ya White House nchini Marekani, lakini hakuna moto. Hali ilivyo haimpi utulivu Rais Donald Trump na njia pekee aliyoona bora kuitumia ni kumhusisha pia mtangulizi wake Barack Obama katika kashfa inayomkabili.

Maana tangu mashirika ya upelelezi yalipoeleza Oktoba mwaka jana kwamba mawakala wa Urusi waliingilia shughuli za uchaguzi wa rais wa Marekani, mlolongo wa ripoti na uvujaji wa habari umezua maswali mengi kuliko majibu. Hali hiyo imelazimu taasisi za kisheria – Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na Baraza la Congress – kufanyia uchunguzi nyaraka juu ya madai yaliyopo.

Taasisi hizo ndizo zitatoa majibu kama Mwanasheria Mkuu, Jeff Sessions alifanya mikutano miwili ambayo haijafichuliwa kilichozungumzwa na balozi wa Urusi nchini Marekani, Sergey Kislyak wakati wa kampeni za urais mwaka 2016.

Hizo ndizo zitabaini walioiba siri kutoka ofisi za Kamati ya Taifa ya Democratic (DNC), barua pepe za mgombea wao wa urais, Hillary Clinton na vikao kati ya maofisa wa utawala wa Trump na wa Urusi.

FBI kazini

Shirika la FBI linafanya kivyake aina tatu tofauti za uchunguzi kuhusu madai kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani na uwezekano wa uhusiano kati ya Urusi na-Trump kama vyombo vya habari vilivyoripoti mwezi uliopita, vikiwanukuu viongozi wa sasa wa Serikali na wa zamani ambao hawakutaka majina yao yatajwe.

•Ofisi ya FBI iliyoko Pittsburg, ambayo ni maalumu kwa uchunguzi wa masuala ya usalama wa kimtandao, inatafuta kutambua watu ambao waliiba na kuvujisha siri kutoka mfumo wa kompyuta za DNC mwaka jana.

•Ofisi ya FBI iliyoko San Francisco inachunguza kubaini watu wanaotuhumiwa kuwa nyuma “Guccifer 2” ambayo ilituma kwa John Podesta barua pepe zilizoibwa kutoka kwa meneja kampeni za mgombea urais wa Democratic.

•Mawakala wa FBI wa Washington wanafuatilia wapelelezi ambao kazi yao ni kufuatilia vyanzo vya watoa habari na nyaraka kwa mawasiliano ya nje.

Katika kile kinachoonekana kuwa uchunguzi wa nne wa FBI kuhusu sakata la Urusi na Trump, ofisi hii ilichunguza mfululizo wa mazungumzo aliyofanya mshauri za usalama wa kitaifa wa zamani, Michael Flynn na Kislyak, ingawa haikuweka wazi kwa Makamu wa Rais Mike Pence, ilisababisha Flynn kujiuzulu Februari 14 .

Kashfa nyingine

Kashfa kubwa ya kisiasa iliyoitwa Watergate ilianza hivi hivi baada ya watu wasiojulikana kuvunja ofisi za makao makuu ya Kamati ya Taifa ya Democratic (DNC) katika jengo la Watergate, Washington, D.C. mwaka 1972 na utawala wa Rais Richard Nixon kuhaha kuzuia uchunguzi.

Baada ya njama kufichuliwa uchunguzi ukafanywa na Baraza la Congress. Ukaidi wa utawala wa utawala wa Nixon ulichochea mgogoro wa kikatiba. FBI, CIA, na Mamlaka ya Mapato (IRS) waliingia kazini, ushahidi uliwekwa wazi kwamba Nixon alihusika kuweka mfuko wa kurekodi shughuli za wapinzani wao lakini alipotakiwa kuwasilisha mikanda hiyo alikataa. Suala hilo likapelekwa mahakama ya juu ambayo iliamuru Nixon aiwasilishe. Nixon alijiuzulu Agosti 9, 1974 na nafasi yake ilichukuliwa na Gerald Ford, Septemba 8, 1974.

Vipi Trump

Mei 2016 ilitolewa ripoti ya kwanza juu ya wadukuzi waliolenga chama cha Democratic. Miezi miwili baadaye, taarifa zilieleza kuwa mashirika ya ujasusi ya Marekani yalibaini uingiliaji wa taarifa uliofanywa na wadukuzi wa Urusi.

Julai, siku ya mkutano mkuu wa Democratic, mtandao wa Wikileaks ulichapisha barua pepe 20,000 kutoka chama hicho. Maofisa wa ujasusi wa Marekani walisema kuwa wanaamini kwa “kiwango cha juu” kwamba Urusi ilihusika katika udukuzi huo, lakini maofisa wa kampeni wa Trump walikana.

Baadaye Trump aliongeza utata aliposema anawakaribisha wadukuzi wa Urusi kulenga hifadhi ya barua pepe binafsi za mpinzani wake Clinton akisema: “Urusi, kama mnasikia, natumai mna uwezo wa kutafuta, ujumbe wa barua pepe 30,000 ambazo zimepotea”.

Taratibu sakata la kashfa ya udukuzi likawa linapata mashiko. Meneja wa kampeni za Trump wakati huo, Paul Manafort alishutumiwa kwa kukubali mamilioni ya dola taslimu kwa ajili ya kuwakilisha masilahi ya Urusi ndani ya Ukraine na Marekani, ikiwamo kuwasiliana na wafanyabiashara wakuu wenye ushawishi mkubwa na ambao wana uhusiano wa karibu na Vladimir Putin. Manafort alichunguzwa na FBI na akajiuzulu uenyekiti wa kampeni za Trump.

Oktoba, taasisi za ujasusi zilitoa ripoti ya pamoja ambayo iliishutumu Urusi kuhusika na udukuzi wa taarifa za DNC. Trump aliendelea kupinga matokeo ya taasisi hizo akidai katika mdahalo kuhusu uchaguzi wa urais kwamba, “Inawezekana ni Urusi, lakini inawezakana pia ulifanywa na China, wanaweza kuwa watu wengine wengi. Anaweza pia kuwa mtu fulani mwenye uzito wa pauni 400 aliyeketi kwenye kitanda chake”.

Mashirika hayo pia yalitoa ripoti iliyoitwa: “Udukuzi wa Hollywood” ambamo zilipatikana kauli zilizorekodiwa za matusi ya aibu alizozitoa Trump dhidi ya wanawake mwaka 2005.

Muda mfupi baadaye, mtandao wa Wikileaks ulianza kutuma zaidi maelfu ya barua pepe za Clinton. Trump aliendelea kukataa Urusi kuhusika katika udukuzi huo. Februari sakata dhidi ya Urusi liliibuka na kuwa kubwa. Ripoti ya gazeti la Washington Post ilisema Flynn alikutana na Kislyak na kujadili kilichodaiwa uwezekano wa Urusi kuondolewa vikwazo.

-->