YOUNG D: Sikuingia kwenye unga kwa bahati mbaya

Mwanamuziki Young D

Muktasari:

Hatimaye Young D ameamua kuutua mzigo huo na kukiri kuwa kwa zaidi ya mwaka mmoja amekuwa akitumia dawa za kulevya pamoja na kukiri kilichomwingiza huko.

Waswahili husema: “lisemwalo lipo kama halipo laja’. Usemi huu umedhihirika baada ya kuwepo tuhuma siku nyingi kuwa Rapa David Genzi maarufu Young D kuwa anatumia dawa za kulevya naye kuzikanusha kila mara.

Hatimaye Young D ameamua kuutua mzigo huo na kukiri kuwa kwa zaidi ya mwaka mmoja amekuwa akitumia dawa za kulevya pamoja na kukiri kilichomwingiza huko.

Kama ulifikiria rapa Young Dee alitumbukia kwa bahati mbaya katika matumizi ya dawa za kulevya, mwenyewe ameiambia Starehe kuwa alifahamu fika kwamba anaingia kwenye unga tofauti na wengine wanapoanza kutumia kwa mara ya kwanza.

Wasanii wengi waliokiri kutumia dawa za kulevya wamekuwa wakitoa ushuhuda kuwa walianza bila kujua. Wengi hueleza kuwa walianza kwa kuwekewa katika bangi au sigara na marafiki, wapenzi au wafanyabiashara.

Young Dee ameyasema hayo wiki moja baada ya kutangaza rasmi mbele ya vyombo vya habari kuwa amekuwa akitumia unga kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuamua kuacha na kupatiwa matibabu na wanasaikolojia.

Akizungumza mapema wiki hii alisema kitu kilichomvuta kutumia dawa za kulevya ni kundi la marafiki ambalo alikuwa akiambatana nalo kipindi alipolegalega katika kazi zake za muziki.

“Washkaji ndiyo walionishawishi kwani walikuwa wanavuta mbele yangu kwa kipindi kirefu, kila nikiwacheki niliona wapo fresh yaani hawana shida yoyote, na mimi nikaanza kuvuta kama mtu anavyoanza kujifunza kunywa pombe na kuvuta sigara,” alisema Young Dee.

Kutokana na aina ya dawa alizokuwa akitumia alikuwa anajua haitakuwa na madhara kwake jambo ambalo halikuwa sahihi.

Hata hivyo, anasema kinachowatumbukiza wasanii wengi katika matumizi ya vilevi hivyo ni mazingira na watu wanaokutana nao kila siku.

“Siyo kwamba niliwekewa kwenye kitu, bali ni mazingira yenyewe ya kazi yalivyo sisi wasanii tunakutana na watu kama hao wengi, wakati mwingine katika mazingira ya kazi, studio, kwenye mikusanyiko na hata nyumbani wanakuja kukusalimia;”

“Kwa mfano walikuwa washkaji zangu wa karibu na wala siyo wasanii. Walikuwa wanakuja kwangu kunisalimia niliona kawaida sana sikudhani kama ingeleta madhara maana wao walikuwa washatumia na hauwadhuru.”

Anasema sasa ameamua kuacha kwa kuwa ameona anakoelekea siyo kuzuri ukilinganisha na ukweli kwamba yeye ni msanii mkali.

“Kwa kiasi fulani nimegundua kuwa nimeyumba kwenye gemu ndio maana sikutaka nisubiri nifike walipofika wenzangu,” anasema Young D.

Akizungumzia project yake mpya, Young Dee anasema ameachia kazi yake mpya na itakuwa kazi ya kwanza tangu kurudi katika kampuni ya MDB inayomsimamia kazi zake.

“Alhamisi ya wiki hii nitaachia wimbo wangu mpya ‘Hands Up’ ni project ya kwanza kabisa tangu nimerudi MDB ni kazi ya kwanza ambayo tumepanga kuanza nayo na baada ya hapo kutakuwa na project zingine ambazo zitakuwa zinafuata.”

Hata hivyo, anafafanua kuwa video ya wimbo huo itafuatia wiki ijayo: “Utakuwa ni wimbo pekee na video itakuja baada ya wiki moja, tunataka video ije kivingine kabisa.”