Simba, Yanga zagawanya viwanja

Muktasari:

Ligi ya msimu huu inatarajia kuwa na upinzani mkali miongoni mwa timu shiriki kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa na klabu husika.

Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2016/17 itaanza mwishoni mwa juma hili kwa timu 16 kuanza kuwania taji linaloshikiliwa na Yanga.

Ligi ya msimu huu inatarajia kuwa na upinzani mkali miongoni mwa timu shiriki kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa na klabu husika.

Baadhi ya timu zimebadili makocha na kufanya usajili ambao zinaamini utazinufanisha. Hayo ni tisa, 10 ni viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya mashindano hayo msimu huu.

Spoti mikiki ilifanya mahojiano na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas kuzungumzia ubora wa viwanja na licha ya kukiri asilimia kubwa ya viwanja vitakavyotumika katika ligi hiyo vimeshafanyiwa uhakiki na kupitishwa alibainisha kuwa Uwanja wa Kaitaba utaendelea kukosa uhondo wa ligi hiyo kwa kuwa hauna sifa.

 

Kaitaba

Lucas anasema baada ya kufanyiwa tathimini juu ya Uwanja huo, Shirikisho la Soka nchini limejiridhisha kuwa uwanja huo hautatumika msimu ujao.

“Tulitarajia utakamilika mapema ikiwa ni pamoja na kutandika nyasi bandia, hayo bado hayajakamilika hivyo Kagera haitatumia uwanja huo na badala yake itatumia Uwanja wa Kambarage,” anasema

 

Sokoine

Uwanja huu ambao zamani ulijulikana kama Uwanja Mapinduzi, utatumiwa na Mbeya City na Tanzania Prisons katika michezo yake ya nyumbani. Lucas anasema uwanja huo umefanyiwa marekebisho kadhaa kwa ajili ya kuhimili vishindo vya Ligi Kuu msimu ujao.

“Sokoine umefanyiwa ukarabati ikiwa ni pamoja na kuweka sawa uzio ili kuzuia mashabiki kutoingia uwanjani, pia eneo la kuchezea limefanyiwa kazi na wamiliki wa uwanja,” anasema

 

Majimaji

Uwanja huu uliopo mkoani Ruvuma, utatumiwa na Majimaji na katika kuhakikisha unakuwa tayari kuhimili mikikimikiki,” anasema Lucas na kuongeza:

“Majimaji umeshakaguliwa na kuthibitishwa kuwa utatumika msimu ujao, tunashirikiana na meneja wa uwanja ili kuhakikisha maeneo ya vyoo na kwingineko yanafanyiwa kazi kabla ya kuanza kwa ligi.”

 

Azam Complex

Uwanja huu una uwezo wa kuchukua watazamaji 5,000, hauna tatizo na kinachosubiriwa ni kuanza kwa ligi.

“Azam ni moja ya viwanja bora tulivyonavyo, uwanja huu unahudumiwa na uongozi na kamati iliyopitia imejiridhisha kuwa uwanja huo hauna matatizo yoyote,” anasema

 

Kambarage

Ni uwanja uliopo mjini Shinyanga na utatumiwa na klabu za Stand United na Mwadui FC.

Lucas anasema uwanja huu wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000 umekaguliwa na kupitishwa kutumika msimu ujao.

“Nao umekamilika, kimsingi hakukuwa na shida katika uwanja huo na ndiyo maana kamati imejiridhisha kuwa uko tayari kwa ajili ya mikikimikiki ya ligi,” anasema

 

Nangwanda Sijaona

Uwanja huu uliojengwa mwaka 1982 Lucas anasema: “Nangwanda ulikuwa na changamoto kidogo hasa katika eneo la kuchezea lakini kamati iliyopita kufanya uhakiki ilijiridhisha kuwa uwanja huo utakuwa tayari kabla ya kuanza kwa msimu huu.”

 

Uwanja wa Taifa

Huu ni uwanja utakaotumiwa na klabu za Simba na Yanga katika michezo ya nyumbani. Kuhusu uwanja huu, Lucas anasema: “Uwanja wa Taifa hauna shida kutokana na ubora wa miundombinu yake, kimsingi la kusisitiza mashabiki watakaokwenda uwanjani hapo kutokujihusisha na uharibifu wa miundombinu.”

 

Jamhuri Morogoro

Uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Morogoro utatumiwa na Mtibwa Sugar katika michezo dhidi ya Simba na Yanga. Lucas anasema pamoja na kwamba uwanja huo utatumika kwa michezo michache, kamati ilipita na kujiridhisha kuwa uwanja uko katika hali nzuri. “Uwanja huu umekuwa na tatizo katika eneo la kuchezea, hivyo kamati iliuomba uongozi wa uwanja kuyafanyia kazi mapungufu hayo,” anasema.

 

CCM Kirumba

Uwanja huu upo katikati ya Jiji la Mwanza na una uwezo wa kuchukua watazamaji 35,000. Kuhusu utayari wa uwanja huu, Lucas anasema: “CCM Kirumba ulikuwa na changamoto ya uchakavu wa baadhi ya miundombinu kama vyooni. Hata hivyo , kamati ilipita kukagua na kujiridhisha kuwa maeoneo ya vyooni yamefanyiwa marekebisho.”

 

Mwadui Complex

Lucas anasema: “Uwanja huo uko tayari,kamati iliyopitia katika uwanja huo imejiridhisha kuwa nao uko tayari kwa mikikimikiki ya Ligi Kuu,”

 

Mabatini

Uwanja huu uko mkoani Pwani na utatumiwa na klabu za JKT Ruvu na Ruvu Shooting. Kuhusu ubora wake, Lucas anasema: “Nao uko tayari ni matumaini yetu uongozi wa uwanja wamefanyia kazi marekebisho waliyoambiwa ikiwamo eneo ya kuchezea.”

 

Karume

Uwanja huu utatumiwa na African Lyon iliyopanda Ligi Kuu. Lucas anasema: “Uwanja wa Karume hauna matatizo hasa eneo la kuchezea. Hata hivyo, African Lyon italazimika kucheza Uwanja wa Taifa kwa mechi za Simba na Yanga.”

 

Manungu Complex

Uwanja unaomilikiwa na Mtibwa Sugar. Lucas anasema: “Manungu bado una shida kwenye majukwaa lakini kiujumla uwanja uko vizuri na Mtibwa itaendelea kutumia. Mechi za Simba na Yanga bado zitaendelea kuchezwa katika uwanja wa Jamhuri kwa kuwa Manungu ni mdogo.”