Simba hii na Yanga hii sio zile

Muktasari:

Kila upande ni wazi unatamba kushinda kutokana na ubora wa kikosi chake, Yanga ikijivunia kikosi chenye kasi na kilichokaa pamoja muda mrefu wakati Simba ikijivunia usajili mkubwa iliyofanya msimu huu na hivyo kurejesha kasi ya timu hiyo.


Mechi ya Smba na Yanga itafanyika Jumamosi wiki hii huku homa ya pambano hilo ikizidi kupanda kila kona.

Kila upande ni wazi unatamba kushinda kutokana na ubora wa kikosi chake, Yanga ikijivunia kikosi chenye kasi na kilichokaa pamoja muda mrefu wakati Simba ikijivunia usajili mkubwa iliyofanya msimu huu na hivyo kurejesha kasi ya timu hiyo.

 

Simba

Msimu uliopita ulikuwa mchungu kwa timu hiyo kwani licha ya kutotwaa ubingwa, machungu zaidi yalikuja baada ya kupokea vipigo viwili kutoka kwa mahasimu wao hao.

Simba ilifungwa mechi zote mbili dhidi ya Yanga msimu uliopita, mechi ya mzunguko wa kwanza ikifungwa 2-0 na mzunguko wa pili ikifungwa tena mabao kama hayo.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa ubovu wa kikosi cha Simba msimu uliopita ilichangia kufanya vibaya kwenye ligi na hata kupokea vipigo viwili kutoka kwa watani zao Yanga.

Simba ya msimu uliopita ilionekana haina kasi na inacheza tu ili mradi ingawa msimu huu inaonekana kuja na nguvu kubwa hasa ikichagizwa na usajili wa kiwango kikubwa iliofanya.

Usajili iliofanya msimu huu umewaongezea nguvu Simba na kujikuta ikitamba kuwa italipiza kisasi kwa kuhakikisha inaifunga Yanga Jumamosi.

Simba imesajili wachezaji wengi msimu huu na baadhi yao ni Method Mwanjali kutoka Zimbabwe, Shiza Kichuya, Mohammed Ibrahim, Muzamil Yassin na Hamad Juma (Mtibwa Sugar), Laudit Mavugo (Vital’O, Burundi), Janvier Bukungu (TP Mazembe), Mussa Ndusha na Jamal Mnyate kutoka Mwadui.

Kuonyesha kuwa Simba imebadilika katika michezo mitano iliyocheza, mpaka sasa imeshinda michezo minne na kutoka sare mchezo mmoja.

 

Yanga.

Yanga haijafanya usajili wa kutisha msimu huu zaidi ya kumuongeza Hassan Kessy kutoka Simba, Juma Mahadhi (Coastal Union) na Beno Kakolanya kutoka Prisons.

Jambo hilo limedhihirisha kuwa Yanga bado ina kikosi bora ambacho kimeendelea kutikisa kwenye Ligi Kuu Bara na ambacho kinaweza kutikisa pia kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya Simba.

Kitu kinachoipa nafasi kubwa Yanga kutikisa katika mchezo wa Jumamosi ni ubora wa kikosi chao na jinsi timu ilivyokaa pamoja, hivyo kuifanya kuwa na maelewano mazuri kwa wachezaji wake uwanjani tofauti na Simba iliyo na wageni wengi.

Yanga iliyoifunga Simba katika mechi mbili msimu uliopita, ni ile ile hivyo bado ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo Jumamosi, ingawa mechi za watani huwa hazitabiriki.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Mayay anasema ni ngumu kutabiri nani ana nafasi kubwa ya kuibuka mshindi katika mchezo huo kutokana na timu zote kuwa katika kiwango kizuri cha soka kwa sasa.

“Yanga haijafanya usajili mkubwa na wachezaji wake wamekaa pamoja muda mrefu hivyo wana maelewano mazuri kuliko Simba ambayo imesajili wachezaji wengi wapya na bado ndiyo wanatafuta muunganiko lakini hilo halifanyi kutabiri nani ataibuka kidedea zaidi ya mwenzake.

“Ukiangalia Yanga, wachezaji wake wengi wamechoka kutokana na kutopumzika tangu kumalizika kwa ligi iliyopita, lakini hiyo haitawafanya kushindwa kung’ara katika mchezo huo kwani huwezi jua Pluijm atakuja na mbinu gani,lakini Simba nao wamebadilika hivi sasa, timu yao ina kasi,wanamiliki mpira na beki yao hivi sasa iko imara,” anasema Mayay.

Kocha Joseph Kanakamfumu anasema timu zote zina nafasi ya kushinda katika mchezo huo.

Yanga bado ina timu nzuri ingawa haina kikosi kipana kama wengi wanavyosema kwani ukiangalia wachezaji wanaoanza na walio benchi wanatofauti kubwa.

“Eneo la ulinzi pekee la Yanga ndio lina watu wa kazi kuanzia wanaoanza hadi wanaokuwa benchi lakini ukiangalia upande wa washambuliaji, ukimkamata Ngoma na Tambwe basi umemaliza kazi, hata eneo la kiungo hivi sasa kama hayupo Kamusoko timu haichezi,” anasema Kanakamfumu.

Anaongeza: “Katika mchezo ujao dhidi ya Simba, bado Yanga ina nafasi ya kufanya vizuri ila kitu kitakachowaathiri ni uchovu wa wachezaji wa kikosi hicho. Kwani baadhi ya wachezaji muhimu Yanga mfano Ngoma wametumika sana hivyo wamechoka.

“Kitu ambacho kitaibeba Yanga ni mbinu za kocha wao Hans Pluijm ambaye kwa kiasi kikubwa anazijua mbinu za timu nyingi hivyo anajua jinsi ya kuzikabili.”

Akiiongelea Simba Kanakamfumu anasema: “Simba nayo ina nafasi lakini tatizo kubwa linaloweza kuwagharimu ni kuwa na wachezaji wengi wapya. Huwezi kujua watachezaje kwani watakosa uzoefu wa kucheza mechi dhidi ya Yanga kwa sababu ni mechi yenye ushindani mkubwa na presha hiyo inaweza kuwa faida kwa Yanga, ingawa Simba hivi sasa ina morali kubwa hivyo inaweza kuwasaidia katika mchezo huo.”

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema Simba ya sasa imebadilika na inacheza soka zuri la kasi hivyo anaamini kuwa itapata ushindi dhidi ya Yanga Jumamosi.

“Usajili ilioufanya umewaongezea nguvu Simba kwani wachezaji wengi wanafanya vizuri, angalia kama Kichuya, Mwanjali, Muzamil wote wameonekana kuwa wameongeza kitu katika kikosi cha Simba,” anasema Pawasa.

Mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Ulimboka Mwakingwe anasema kwa kasi ya sasa ya Simba haoni jinsi Yanga itakavyopona Jumamosi. “Hii Simba ya sasa ya mwendo kasi, unaifurahia jinsi inavyocheza, kasi waliyonayo ni kubwa tofauti kabisa na msimu uliopita na kasi hii kama wakionyesha dhidi ya Yanga sioni jinsi watakavyopona,” anasema Ulimboka.