Simulizi ya maisha ya ghetto kwa wanafunzi wa kike Bahi

Muktasari:

  • Katika safari hiyo, nimeambatana na msichana aitwaye Veronica Tito. Huyu ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hii. Lengo la safari yangu ni kuona anakoishi Vero (kama anavyoitwa na marafiki zake).
  • “Karibu sana, hiki ndicho chumba changu,”ananikaribisha katika chumba kimoja kati ya vinne vilivyoko kwenye nyumba yenye mwonekano duni kwa anayeitazama.

Jua la adhuhuri linawaka barabara, lakini halizuiii safari yangu ya dakika kama 20 kutoka Shule ya Sekondari Chikopelo kwenda kijiji cha Bwawani kilichopo katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Katika safari hiyo, nimeambatana na msichana aitwaye Veronica Tito. Huyu ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hii. Lengo la safari yangu ni kuona anakoishi Vero (kama anavyoitwa na marafiki zake).

“Karibu sana, hiki ndicho chumba changu,”ananikaribisha katika chumba kimoja kati ya vinne vilivyoko kwenye nyumba yenye mwonekano duni kwa anayeitazama.

Haina madirisha, milango na chini sakafu ni vumbi, lakini humo ndimo wanamoishi kina Vero; wenyewe wanapaita ‘geto’

Nimeingia ndani ya geto hili na sasa nakaribishwa katika chumba cha Vero na mwenzake Anastazia Mselemia ambaye pia ni mwanafunzi wa shule ya Chikopelo.

Chumba hiki hakina mlango, isipokuwa pazia jeupe ambalo likipeperushwa na upepo, kila kilichomo ndani kinaonekana.

Hata vyumba vingine vitatu ambavyo wapangaji wake ni wanafunzi wa kike na wa kiume, havina milango.

Mbele ya nyumba hii naona mkusanyiko wa vijana wa kiume, wakazi wa Bwawani. Shughuli za ufundi baiskeli zinaendelea. Wengine wanapiga soga. Wengine wanacheza ‘draft’.

Veronica anasema bei ya chumba chake ni Sh5,000 kwa mwezi. Ni bei ambayo wazazi wake wanaweza kuimudu. Anaishi hapa kutokana na umbali uliopo kutoka kwao hadi shuleni.

“Kwetu ni mbali sana. Nikisema nitembee kutoka huko, shule itanishinda,”anaeleza..

Wanafunzi wanaosoma kwenye shule ya Chikopelo wanatoka katika vijiji vya Chali Igonga, Chali Isanga, Chali Makulu, Bwawani, Zegere na Nondwa.

Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa baadhi ya vijiji hivyo viko umbali wa zaidi ya kilometa 30 kutoka ilipo shule.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, inataja umbali mrefu wa kutembea kwenda shuleni na kurudi, ujauzito, umasikini na ndoa za utotoni, kuwa miongoni mwa sababu za watoto wengi wa kike kuacha shule.

Baadhi ya wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Magaga wakiwa nje ya vyumba walivyopanga mtaani, maarufu kwa jina la magheto. Picha na Tumaini Msowoya

Maisha ya ‘geto’

Baada ya kuitika makaribisho ya Vero, naangaza macho nikitafuta mahali pa kukaa. Kwa haraka nabaini hakuna meza, kiti wala kitanda. Naweka begi langu chini kisha naamua kukaa kwenye turubai jeusi ambalo limetandikwa kwenye sakafu.

Baadaye Vero anasema turubai hili ndicho kitanda chake. Nikiwa nimeketi naona kibatari kwenye moja ya pembe za chumba hiki. Akilini mwangu nawaza kwamba hiki ndicho huwapa mwanga usiku, iwe kwa kusoma au kazi nyinginezo.

Vero hana wasiwasi. Kwa haraka anabadilisha nguo, akachukua chungu na sufuria yenye masizi, akatoka nje na kuanza kukoka moto wa kuni kwa ajili ya kuandaa chakula. Anafanya hivyo juani, jasho likimtoka.

Kwa sababu moto unasumbua kuwaka, nainuka nilipoketi, nakung’uka vumbi ambalo limechafua nguo niliyoivaa, nakwenda kumsaidia. Moto unakolea, kisha tunaanza kusaidiana kupika.

“Dada utaweza kula hiki chakula kweli? Sisi ndio chakula chetu kila siku, hatuna mboga nyingine ya kubadilisha,”anauliza Vero wakati tukiendelea kupika. Mboga anayoizungumzia inaitwa ‘Segulasegula’. Haya ni majani ya kunde yaliyokaushwa.

Namtoa hofu Veronica kwa kumwambia kwamba hata mimi wakati nasoma sekondari kama yeye, nilizoea kutumia aina hiyo ya mboga. Wakati tunakaribia kuhitimisha mapishi haya, mara wanaingia wasichana watatu. Mmoja wao ni Anastazia anayeishi pamoja na Vero.

Sasa chakula tayari; mboga kwenye chungu, ugali kwenye sufuria. Hakuna sahani wala kijiko hapa. Chungu na sufuria vinaingizwa ndani, tunaanza kula wote kwa pamoja.

Veronica anasema huwa anapata mlo mmoja kwa siku, kutokana na bajeti ndogo anayopewa na wazazi wake na kwamba Ijumaa huwa ni siku ya wanafunzi waliopanga kwenda makwao kuchukua vyakula.

“Nikifika napewa unga ‘lita’ (kilo) moja au zaidi na mboga ya segulasegula ambayo lazima nitumie wiki nzima. Kwa siku tunakula mlo mmoja tu,”anasema.

Maisha haya ya Vero na mwenzake Anastazia yanaakisi maisha ya mamia ya wanafunzi wa kike wanaosoma shule za msingi na sekondari, wakiishi kwenye ‘mageto’ bila uangalizi wa wazazi au walezi wao. Maisha haya yana madhara makubwa, ikiwamo kuwa kichocheo kikubwa cha ujauzito.

Mazingira si salama

Mwenyekiti wa kijiji cha Sokoni-Bahi, Nacheti Mlyanzoka anasema wasichana wanapopanga mitaani, kunawafanya wajiingize kwenye vitendo vya ngono kwani hawana uangalizi wa karibu.

“Niiombe Serikali ipunguze gharama za hosteli kwenye shule za kata ili wazazi wote wamudu gharama za kuwapeleka watoto huko. Pia wajenge mabweni kwenye zile zisizo na mabweni, hii italeta ahueni kwa watoto wetu,”anasema.

Wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule ya Sekondari ya Magaga wanakiri kuwa mazingira wanayoishi ni magumu na yanahatarisha maisha yao.

“Siku nyingine unataka kwenda kuoga, hapo uwanjani ukakutana na wavulana wengi wanaongea kwenye kijiwe chao, inabidi tu ukae ndani,” anasema Asha Abdalah ambaye mwanafunzi wa kidato cha kwanza.

Asha anabinisha kuwa wapo wanaume wakware ambao wamekuwa wakiwatongoza kila kukicha kwa sababu wana uhakika kwamba hawana uangalizi.

Mwingine ni Mlekwa Matonya anayesoma kidato cha nne ambaye anaishi katika chumba ambacho kinapakana na klabu ya pombe. Ifikapo saa kumi jioni, klabu hiyo huanza kupigwa muziki kwa ajili ya wateja wake.

Kadhalika anapakana na saluni ya kunyolea nywele ambayo pia hupiga muziki wakati wote inapokuwa wazi. Mlekwa anasema kelele hizo humfanya ashindwe kusoma na wakati mwingine hubaki amejifungia na kushindwa hata kwenda kujisaidia, akiogopa watu.

Ndani ya chumba chake lipo godoro dogo na nguo zake ambazo huzitundika kwenye misumari aliyoipigilia ukutani. Hata hivyo analalamika akisema wakati wa kupika, chumba hujaa moshi.

“Kama unavyoona nyumba hii ina vyumba vitatu, kimoja tunatumia kama jiko, sio sisi tu hata wenye nyumba hupikia humu. Moshi ukijaa huwa hatuwezi kusoma wala kufanya chochote. Tunatoka nje kusubiri hadi uishe,”anasema.

Anasema mara kadhaa wameshuhudia wenzao wakikatiswa masomo kwa kupata mimba, kurubuniwa na wanaume au kutokana na ugumu wa maisha.

“Namshukuru Mungu katika mazingira haya magumu natarajia kumaliza kidato cha nne…naamini nitafaulu,”anasema Mlekwa.

Chanzo cha mimba

Msaidizi wa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Magaga, Daudi Gingi anakiri kuwa mazingira magumu wanayoishi wanafunzi hao ni chanzo cha mimba na utoro.

“Sisi kama walimu huwa tunawapitia huko mitaani walikopanga, hata hivyo sio rahisi kuwalinda,”anasema.

Mwalimu mlezi wa watoto wa kike wa shule hiyo, Wende Mbuna anasema ujenzi wa hosteli unaweza kupunguza mimba na utoro. “Nyumba nyingine walizopanga zinauzwa pombe unadhani wanaweza kukwepa vishawishi? Ni vigumu,”anasema.

Hata hivyo Mkuu wa Shule ya Sekondari Chikopelo, Juma Idosa anasema hosteli ipo, lakini kutokana na ugumu wa maisha wazazi wanashindwa kumudu gharama zake.

“Tumepunguza gharama, kila mwanafunzi anatakiwa kuchangia Sh17,000 kwa miezi mitatu na debe moja la chakula, lakini bado watoto wengi wamepangiwa mitaani,”anasema.

Mkuu wa shule ya Sekondari ya Bahi, Stellah Selemani anasema: “…sisi tuna hosteli, lakini wasichana 20 tu kati ya 180 waliopo ndio wanaoishi hapa wengine wamepanga”.

Harakati za uongozi

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chifutuka, Gasper Mhembono anasema wameamua kuanza ufatuaji wa tofali 5,000 kila kijiji ili kuwanusuru wanafunzi na upangaji kwenye geto.

“Tunawashirikisha wananchi kwenye ujenzi wa hosteli, itasaidia watoto wetu wasipange,”anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu anasema kuwa wapo kwenye mkakati wa kuhakikisha kuwa kila shule inajengwa hosteli ili wasichana hao waondokane na maisha ya kupanga mitaani.

Hata hivyo anawataka wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwahahakikishia usalama watoto ikiwamo kuwapa chakula jambo litakalopunguza mimba na utoro.

“Tumekubaliana kwamba kila shule ianze kutoa chakula cha mchana, kitasaidia watoto wasipoteze muda kwenda kupika,” anasema.