UCHAMBUZI: Sioni mantiki wala tija ya mahafali

Muktasari:

Taifa lolote duniani lenye kunuia kupiga hatua za kimaendeleo, huhakikisha watu wake wanapata elimu bora tena kwa gharama rahisi kwa kila mzazi.

Mwanafalsafa wa Ugiriki, Plato alisema: “Maisha yasiyotafakariwa hayafai kuishi.”

Taifa lolote duniani lenye kunuia kupiga hatua za kimaendeleo, huhakikisha watu wake wanapata elimu bora tena kwa gharama rahisi kwa kila mzazi.

Mwanafunzi kwa upande wake, anatazamiwa kufanya jitihada za kusoma kwa bidii ili kufikia maagano kati yake na wazazi ikiwa ni pamoja na kuwa mtiifu wa nidhamu.

Mzazi mwenye mawazo chanya, daima atafurahi na kuridhia amuonapo mwanawe amehitimu shule akiwa na ufaulu wa kumwezesha kusonga mbele kimasomo.

Nashawishika kusema hali ipo tofauti hapa nchini, kwani wazazi wengi wanapenda kufanya sherehe za kuhitimu watoto wao kabla ya kufanya mitihani ya mwisho, badala ya kusherehekea ufaulu wa vijana wao baada ya matokeo.

Imekuwa hulka na utamaduni kuona wazazi kwa kushirikiana na wakuu wa shule wakithamini sherehe za mahafali kwa kuchangia na kutumia gharama kubwa.

Ina maana gani kwa mwanafunzi wa kidato cha nne au cha sita kufanya sherehe za mahafali kabla ya kupata matokeo yake? Pengine sherehe hizi zingekuwa na maana kwa mtoto mdogo wa awali ambaye amehitimu darasa la awali kwa kuwa alikuwa hajui kusoma na kuandika sasa walau anajua kusoma.

Huyu ana haki ya kupongezwa na wazazi, lakini sio kwa kufanya mahafali (sherehe), kwani elimu si suala la kulifanyia sherehe, elimu ni suala la msingi kama ilivyo chakula na mavazi.

Kwa nini ufanye sherehe kabla ya kula, kuvaa nguo au kabla ya kulala? Haya ni mahitaji ya msingi ya binadamu; tujiulize kama taifa, sherehe hizi zina mantiki na tija ipi?

Historia inatuambia kwamba sherehe za kuhitimu masomo kwa wanafunzi zilianza huko bara la Ulaya katika karne ya 12.

Vazi maalumu wakati wa sherehe hizi ilikuwa ni magauni ambayo baadaye yalirasimishwa kuwa vazi rasmi la kuvaa wakati wa mahafali.

Karne ya 14 na 15 ilibuniwa kofia maalumu ya kuvaliwa, ikiwa na maana ya uwezo wa juu kiakili.

Katika ngazi ya vikuu, mahafali hizi hufanyika baada ya chuo husika kutoa matokeo ya wanafunzi wake na vyeti vya kuhalalisha kuhitimu masomo yao. Kwa taratibu zilivyo, chuo kinahusika kutunuku ngazi ya elimu kwa mhitimu siku hiyo ya mahafali, haiwi jukumu la chuo kumfanyia sherehe mhitimu.

Leo, tunashuhudia wahitimu wakikodi kumbi kufanya sherehe wakiwa wamevaa majoho na kofia. Huenda wanamaanisha kuhitimu masomo.

Kwa nini mwanafunzi wa chini naye afanye sherehe kabla hajafanya mitihani? Hii ni sawa na kusherehekea ndoto!

Huenda ukawa ni utaratibu mzuri wa kufanya sherehe lakini ikumbukwe kuwa sherehe ni gharama kubwa kwa shule, mzazi na zaidi inaharibu tu saikolojia ya mwanafunzi, kwani kwa utafiti mdogo niloufanya nimebaini wanafunzi wengi hujikuta wakitumia muda mwingi kuifanya siku hiyo ya mahafali kuwa ya kipekee.

Wengi hupoteza muda katika kubuni mavazi na kujiandaa kwa siku hiyo.

Najua thamani ya kutambua na kuwapongeza wanafunzi wanaofanya vyema katika masomo yao, lakini sidhani kama vyeti vya utambuzi wao au zawadi zao lazima zitolewe kwa kuitisha sherehe za mahafali.

Sherehe ya mwanafunzi huyu ni kumjengea mazingira ya usikivu na utulivu katika akili yake na ajue mbele yake kuna mtihani ambao ni sawa na mapambano.

Sikumbuki kuona au kusikia askari wakifanya sherehe kabla ya kwenda vitani, mara kadhaa hufanya sherehe baada ya ushindi mwishoni kabisa.

Frank Chalamila ni mwalimu na mtunzi wa kitabu Fedheha ya Mwajifriwa. 0717-707187