NDANI YA BOKSI: Siyo sanaa tu... mpaka mapenzi kama Big G

Muktasari:

Hata serikali yetu pia inafurahishwa na mafanikio ya wanamuziki, na inachukizwa wanapokosea na kwenda kinyume na maadili yanayostahili.

Mtu mwenye upeo mkubwa, si tu atawapenda adui zake wakifanya vizuri, bali pia atawachukia marafiki zake wakikosea.

Hata serikali yetu pia inafurahishwa na mafanikio ya wanamuziki, na inachukizwa wanapokosea na kwenda kinyume na maadili yanayostahili.

Tuachane na hayo bana. Maana tukiamua kuzama sana hatutamaliza. Na hizi ‘stress’ katikati ya mwezi tukisubiri mabosi wateme mzigo. Tutaishia kurushiana maneno kisha ngumi.

Sasa sikia. Unajua hizi totoz hapo kabla hazikuwa lolote wala chochote. Ni vile tu wamekutana na hawa mabishoo wa sasa watoto wa mama.

Enzi hizo kuna maneno yaliwaponza watoto wazuri na walishituka wakiwa wamechelewa sana. Silaha kuu ilikuwa maneno siyo “siksi paki’ na pesa kama sasa.

Ukitazama kwa jicho la haki kwa maana ya haki. Zamani kulikuwa na masela vichwa sana kuliko mabishoo wa sasa. Madogo wa sasa wamerahisishiwa sana.

Mizuka ya zamani ili ukamatie mtoto mzuri wakati huo ufundi ulihitajika. Ufundi wa kucheza na maneno.

Watoto wa mjini walikuwa mafundi wa maneno bana. Siyo kulamba lips kama hawa wa kizazi hiki. Wakati huo mtoto anabanwa kwenye kona dakika sifuri anaelekea kibra.

Siongelei ‘bushi’ na mitama yao. Kule maneno machache vitendo vingi. Yaani dem anasubiri akatwe mtama badala ya kusubri udambwi udambwi wa maneno.

‘Bushi’ ilikuwa mizinguo sana. Kifupi usijivunie historia ya mapenzi kwa tabia za watu wa Sitimbi huko. Walikuwa wanazingua. Naongelea watoto wa mjini.

Siwezi kujivunia kitu cha kale kama kumtokea demu kupitia rafiki yake ndo akulainishie njia. Ule ulikuwa ubwege kama ubwege mwingine.

Eti baada ya kuonana mara mbili mnapanga siku. Yaani aje kichakani. Au kama vipi chini ya Mwembe fulani hivi amazing hapo kijijini.

Akifika tu swali bila salamu: “Ester alikupa ujumbe wangu?” Naye anajibu “Ndiyo” badala ya kuuliza angekuwa hajaniambia ningekuja hapa?

Anaona aibu. Akijisugua mguu juu ya mguu mwingine. Anang’ata vidole na macho yake yakijenga undugu wa ghafla na ardhi.

Wakati huo naye mwanaume kama bwege utasikia. “Basi ndo hivyo si upo tayari mpenzi wangu... mwenzio nipo hoi juu yako.”

Msichana naye alijikuta “Mi sijui ila nyie wanaume nyie mnajifanya mnatupenda kumbe mnatuchezea tu. Mi naogopa bwana.”

Mpaka hapo kwa sisi wanaume kutoka Tarime. Hatukuchelewesha. Hapo ndo kakubali tayari. Ni kata funua miguu juu. Mtama wa hatari.

Usianze kurudia maneno.

Watoto wa town ndo kuna maneno yalikuwa yanawaponza sana. Utasikia: “Unajua Salome nilipokuona tu moyo ulilia paaaah! nikajiukiza huyu malaika kashuka lini duniani?”

Toka siku hiyo silali kwa ajili yako. Naweweseka juu ya penzi lako Salome. Nalala nikikuota nikishituka usingizini napapasa pembeni sikuoni mpenzi.

Nagundua niko peke yangu kitandani. Sononeko la moyo linaingia na kukaa eneo la usingizi. Matokeo yake mpaka kunakucha nakuwaza wewe tu Salome.

Basi ni vile sina pesa. Lakini wewe Salome ulistahili kununuliwa bahari yote. Coco Beach (Ndege beach ilikuwa maarufu sana wakati huo) iwe yako. Nakupenda Salome.

Yaani hata nikinywa maji nakuona kwenye glasi. Tabasamu lako tamu kama noti mpya ya Nyerere. Niko radhi kufa kwa ajili yako Salome. Naomba unipe nafasi kwenye uvungu wa moyo wako.

Hata kama uvungu umejaa. Niweke kwenye kibaraza. Kama napo hakuna nafasi nitafutie hata banda la uwani nipange kwa muda nikisubiri uniweke ndani ya moyo rasmi. Salome nafsi yangu inateketea kikatili kama siyo kindava juu ya penzi lako. Kuna miale ya moto inachoma kifuani kwangu kila upitapo.

Napenda unavyotabasamu. Unavyocheka. Ukitembea mimi hoi. Hata ukinuna navutiwa na uso wako. Wewe ni malaika unayeishi kimakosa duniani. Tena Tanzania badala ya Ulaya.

Nakupenda sana Salome. Haki ya nani tena. Eh eh eh eh (Kidume unalamba ulimi unapangusa mchanga kisha unalamba tena ulimi), kama mimi muongo nife hapa hapa. (Eti ndo umekula kiapo).

Mpaka hapo mtoto Salome utamuona anazungusha shingo. Miguu ikichora maroroso chini. Tayari hamna kitu tena. Yaani umechukua jimbo bila kusubiri sauti ile ya Jaji Lubuva.

Kama umemwandikia barua unakakikisha ndani umenyunyizia na poda. Umemchorea ua na mkuki umepenya kwenye alama ya kopa (moyo).

Wakati madem wa sasa watakuuliza “Kwani shingapi?”

Zamani ungeambiwa ngoja afikirie kwanza. Hapo masela wa kitambo tulijua tayari. Mtoto kaelewa. Kishatafunwa.

Miluzi mingi hata kama siyo ya mdomoni basi ya kwenye bandama, figo, mapafu na kongosho. Lazima zipige makofi. Humuachii aondoke unakaza zaidi ili zigo upewe siku za karibuni.

Siku hizi bana siyo poa hata kidogo. Siku ya kwanza mnakutana baa mitungi mingi michemsho na stori kadhaa. Jiwe mbili mezani anajikataa. Ndo tayari hivyo.

Totoz za kitambo kile maneno matamu yaliwavua nguo. Siku hizi pesa mezani ndo inawavua nguo. Kifupi wanaingiza pesa kila mwisho wa wiki kama kina Ronaldo.

Mtoto hotelini haangalii runinga wala sura yako. Yeye macho kayaelekeza kwenye pesa mezani akikadiria ziko ngapi na yeye utampa ngapi.

Unadhani hapo atafika Kibo au Mawenzi? Hawezi. Wanaishia kusema wanaume wa Dar hamna kitu. Kumbe wao ndiyo matango pori kutoka Ikwiriri.

Unampa pesa. Unamlisha na kumnywesha na bado anataka akupe adhabu ya kumfikisha Kibo au Mawenzi. Zamani dem ukimpa hela anakataa kwa kuogopa kwao ataulizwa kaitoa wapi. Siku hizi sijui pesa zenyewe wanafanyia nini maana hawaendelei na zaidi wanachoka nyuso zao kama kuta za selo za polisi.

Mkikutana iwe njiani, kwenye starehe au katika magroup ya whatsApp. Mnapeana namba. Mnachati, mnaalikana. Tayari wapenzi na wivu juu.

Kuna siku nilileta za kizamani. Nikaanza maneno yangu dem ananikodolea macho tu. Mwisho nikaambiwa nimekusikia andaa changu kesho nakuja kwako.

Duh...

Magufuli kaweka watu sawa kabisa. Warembo waliokuwa wanategemea kuwekwa mjini na wanaume siku hizi wamefulia. Wengine ‘bize’ na matangazo ya Waganga mitandaoni wapate pesa za saluni.

Demu ambaye umetumia nguvu nyingi na muda mrefu kumpiga ‘saundi’ anavutia sana, kuliko wa kumnyakua kaa bando la chuo.

Siyo muziki tu pia mapenzi ya sasa yanakinai upesi. Yaani watu hawadumu kwenye uhusiano kama zamani. Nyakati za sasa na mazingira yake yanahatarisha neno upendo.

Kinachotokea ni kwamba wanaume wanatongoza kirahisi wasichana. Na wasichana wanakubali kirahisi sana. Sasa kwa nini mwisho wa mapenzi uwe mgumu? Lazima uwe rahisi tu.

Ndani ya mwaka jana tu. Aslay alitoa nyimbo nyingi sana. Wasafi na bosi wao Diamond walitoa nyimbo nyingi sana ndani ya mwaka mmoja. Kama “Bigi Jii’ vile. Nyimbo zilibamba ghafla na kutoweka ghafla.

Muziki wa sasa unaisha utamu haraka kama ambavyo uhusiano wa sasa unavyoisha haraka kwa wapendanao. Utandawazi umekuja na faida kubwa sambamba na ukubwa wa matatizo.

Zari ‘The Boss lady’. Alikutana kwenye ndege na mzazi mwenzake na kuanza penzi ghafla. Mimba ghafla. Mimba ya pili ghafla. Kisha wameachana ghafla kupitia Instagram.

Siyo sanaa tu. Ukifuatilia sana kila kitu hakidumu dunia ya sasa. Kanumba kaondoka 2012 bila kuijua whatsApp. Kaacha BBM na Facebook. Leo hii ndani ya miaka sita tu kuna mpaka Snapchat.