Skendo hazileti pesa isipokuwa kinyume chake

Nimekutana na wasanii wengi wa kike nchini wanaomzimia staa wa vipindi vya televisheni wa Marekani, Kim Kardashian na kwa kiasi fulani wamejaribu kuigiza aina ya maisha ya mwanamke huyo.

Kwa kifupi Kim na familia yake wanaingiza fedha kwa kuanika maisha yao. Kuanzia kwenye televisheni, majarida, magazeti na mitandao ya kijamii.

Familia hiyo imejipatia utajiri kwa kazi hiyo...kujianika. Wapo wanaowabeza kwa aina hiyo ya maisha, lakini wamefanikiwa kujipatia umaarufu na mali. Pia, wamejizolea umaarufu kuliko baadhi ya mastaa wakubwa wa muziki, filamu, soka na michezo mingine.

Kwa mfano Kim anachuana kwa karibu na mwimbaji Beyonce katika mitandao ya kijamii kwa kuwa na ufuasi mkubwa. Wakati Beyonce akiwa na wafuasi milioni 108 katika mtandao wa instagram, Kim anao milioni 104.

Mwanamuziki Rihanna ana wafuasi milioni 58, Christian Ronaldo milioni 115, Nicki Minaj wafuasi milioni 84.1. Kama ulikuwa hujui fahamu kuwa Kim ana utajiri wa dola za Marekani 150 ni wastani wa Sh301.5 bilioni.

Kwa hesabu hizi unaweza kuiona nguvu ya Kim katika kuvuta ufuasi. Ikumbukwe kuwa ufuasi ni mtaji kwa sababu unakuwezesha kupata matangazo ya biashara. Kama hapa kwetu ufuasi wa watu laki tano mpaka milioni moja unawafanya waishi vizuri, je huyu mwenye watu milioni 100? Huyu ndiye mwanamke anayeweza kukubali malipo ili afanye chochote na siyo kufanya chochote ili atengeneze fedha. Yaani fedha kwanza mambo mengine yanafuata.

Labda turudi nyuma miaka 12 iliyopita. Mwanamke huyu alikuwa na mkanda wa ngono aliojirekodi akiwa na na mwanamuziki Ray J. Aligundua kuwa ile ni fedha na kuamua kuuza.

Wakati dunia ikimtukana kwa kuanika mambo yake ya faragha, inadaiwa kuwa alikuwa tayari ametia kibindoni dola laki tano sawa na Sh1.2 bilioni. Fedha kwanza halafu skendo baadaye. Upuuzi mwingi anaoufanya Kim Kardashian upo katika vipindi vyao vya Keeping up With the Kardashian. Anakuwa amelipwa kufanya hivyo. Inaelezwa kuwa kwa kila kipindi anavuta dola laki moja na nusu ambazo ni wastani wa Sh301 milioni.

Ajabu ni kwamba hapa kwetu mtu anataka afanye skendo halafu fedha ije baadaye. Ndiyo maana wanasema eti ukiandikwa kwa matendo mabaya unajulikana na kupata dili mbalimbali.

Siyo kweli. Skendo hizi zimewashusha wasanii wengi na waliobaki wananing’inia katika mstari mwembamba wakielekea kutupwa nje ya gemu. Mfuatulieni vizuri Kim mtagundua kitu cha kujifunza. Najua Calisah alikubali kuvaa viatu vya kike kwa kuwa mpunga ulishafika mezani kwake.