Soko la hisa lina mchango mkubwa Tanzania ya viwanda

Muktasari:

  • Mwaka 2017 kwa mfano, ni kampuni moja tu iliorodheshwa sokoni hapo. Licha ya Sheria ya Mawasiliano ya Electroniki na Posta (Epoca) kuzitaka kampuni zote za mawasiliano kujisajili kwenye soko hilo, ni Vodacom pekee ilitekeleza agizo hilo.

Mwitikio mdogo wa kampuni kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kunachelewesha kasi ya wananchi kumiliki na kuendesha uchumi kupitia taasisi mbalimbali zilizopo nchini.

Mwaka 2017 kwa mfano, ni kampuni moja tu iliorodheshwa sokoni hapo. Licha ya Sheria ya Mawasiliano ya Electroniki na Posta (Epoca) kuzitaka kampuni zote za mawasiliano kujisajili kwenye soko hilo, ni Vodacom pekee ilitekeleza agizo hilo.

Epoca inazitaka kampuni hizo kuorodhesha walau asilimia 25 ya hisa zao ili kuwapa Watanzania fursa ya kuwekeza kwenye sekta ya mawasiliano inayokua kila siku. Tangu kampuni hizo zianze kutoa huduma za fedha kwa mfano, takwimu zinaonyesha asilimia 65 ya wananchi wanafikiwa na kutumia huduma hizo.

Kati ya watumiaji hao, ni asilimia 17 tu wanazipata kutoka kwenye benki 58 zilizopo nchini na wanaobaki wakitegemea simu zao za mkononi. Takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha mpaka Septemba mwaka jana, takriban Watanzania milioni 22 walikuwa wanatumia huduma hizo.

Mwananchi limezungumza na Mkurugenzi Mkuu wa DSE, Moremi Marwa kuhusu mwenendo wa kampuni mpya kujiorodhesha katika soko hilo sanjari na ukuaji wa sekta ya masoko ya mitaji na hisa hapa nchini.

Anasema DSE inao mkakati wa kuinua uchumi wa nchi uwe wa hadhi ya masoko makubwa ya hisa ulimwenguni kupitia mpango wa maendeleo wa unaoanza mwaka huu hadi 2022 ambao soko hilo limejiwekea.

Endapo mwitikio wa kutekeleza matakwa ya Sheria ya Epoca ungekuwa mkubwa, anasema kampuni zilizoorodheshwa zingekuwa nyingi tofauti na 26 zilizopo sasa hivi.

Anasema pamoja na kuwa nje ya muda uliopangwa, kampuni hizo zinaendelea na mchakato wa kujiorodhesha kwani tayari zimewasilisha maombi ya kufanya hivyo. “Zipo katika mchakato wa utekelezaji wa sheria hiyo, zilizoleta maombi bado yanafanyiwa kazi. Si kwamba zimeshindwa ila bado zinalifanyia kazi suala hilo,” anasema.

Anafafanua kwanini Vodacom iliweza kumaliza mchakato huo mapema kuliko wengine pia. Anabainisha kwamba, kila kampuni ina changamoto zake hivyo huwezi kulinganisha kampuni moja na nyingine. Kuna changamoto za kiutawala, kisheria kiumiliki, utayari wa mambo ya utawala bora na uwazi.

Kampuni ya Tigo, kwa mfano, ina mgogoro wa umiliki unaoendelea. Ili isajiliwe sokoni hapo ni lazima iumalize kwanza ili kila kitu kieleweke na kufahamika mbele ya jamii kubwa ya wawekezaji watakaovutiwa na hisa zake.

Mwishoni mwa mwaka jana limeibuka sakata la umiliki wa hisa za Kampuni ya Airtel kati ya Serikali na Bharti Airtel ya India. Serikali inasema uuzaji wa hisa za iliyokuwa Celtel ulikiuka masharti na umiliki wote wa Airtel ni wa Serikali ambao unapaswa kuwekwa chini ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Mwaka 2017 Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria na kuibadili iliyokuwa Kampuni ya Mawasilino Tanzania kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania. Haya yamefanywa kabla TTCL haijatekeleza sharti la kuorodheshwa DSE.

Kwa kuzingatia hayo yote, Moremi kampuni zilizobaki zipo katika hatua tofauti za kujiorodhesha hivyo ni vigumu kusema kwa nini huyu ameweza na yule ameshindwa kwa sababu kila mmoja yupo katika changamoto zake ambazo zinaweza kuwa za kitaifa, kisekta au nyingine zinazoihusu kampuni husika.

Mkakati

Baada ya kutekeleza mpango mkakati wake wa mwaka 2012 hadi 2017, sasa DSE imeanza kuutekeleza mpya wa mwaka 2018 hadi 2022 kwa lengo la kuboresha zaidi mazingira ya biashara, sheria uongozi na utawala iliyonayo.

Ndani ya muda huo kumekuwa na mafanikio kadhaa ikiwamo kukua kwa mtaji wa soko na ongezeko la wawekezaji. Kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa mfano, takwimu zinaonyesha wawekezaji 40,000 wameongezeka kutoka 470,000 waliokuwapo mwaka 2016 mpaka 510,000 mwaka jana.

Pia, mkurugenzi huyo anasema wanatengeneza utaratibu wa kikanuni ambao utawezesha bidhaa mpya zaidi kuorodheshwa katika soko ikiwa ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha zaidi wafanyabiashara, taasisi na wananchi kulitumia soko la hisa kupata mtaji wa uwekezaji sanjari na kuongeza ukwasi.

Kutekeleza malengo hayo, anasema wanataka soko liwe kubwa zaidi kwa maana ya mtaji, ukwasi, idadi ya wawekezaji na kampuni zilizoorodheshwa ili kuongeza mchango wa sekta hii katika pato la nchi.

Bila kutaja kiwango, Moremi anasema wanakusudia kukuza mtaji wa soko kwa kipindi cha utekelezaji wa mpango huo. “Kiwango chochote kitakachoongezeka kwetu litakuwa jambo zuri. Katika miaka mitano iliyopita tulishuhudia ongezeko la takriban asilimia 30 ya ukubwa wa mtaji kutoka Sh17 trilioni hadi Sh21 trilioni na mchango wake kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20,” anasema.

Si mtaji pekee ulioimarika. Anasema wamefanya vizuri pia kwenye ukwasi wa soko kwani miaka mitano iliyopita, mauzo ya mwaka mzima yalikuwa yamefika Sh50 bilioni ambayo kwa sasa yameongezeka kwa mara 10 na kufika Sh500 bilioni.

“Wawekezaji sokoni walikuwa kama 200,000 lakini hizi sasa tunao zaidi ya 500,000,” anasema.

Kuongeza ushiriki zaidi wa wananchi na ufanisi wa soko, anasema miaka mitano ijayo wanatarajia ongezeko angalau sawa na hili walilolipata katika miaka mitano iliyopita. Anakumbusha: “Kimsingi soko linabaki kuwa soko na tathimini zake hazibadiliki, hata huu mpango wa sasa mategemeo ni yaleyale, kinachobadilika ni mikakati na namna ya utekelezaji wake.”

Anasema kusudi lililopo katika utekelezaji wa mpango huo mpya baada ya miaka mitatu au mitano ni kutajwa na kutambulika na mashirika makubwa ya kimataifa. Kwa vigezo hivyo vya kimataifa, Tanzania itambulike kama soko linalochipukia ili kuongeza wawekezaji wa kimataifa na kuwawezesha wajasiriamali nchini kukopa kiasi kikubwa zaidi na kufanikisha miradi yao.

“Masoko hayo mitaji yao inakuwa ni kuanzia asilimia 30 ya Pato la Taifa,” anasema Moremi.

Kufanikisha utekelezaji wa mkakati wake wa miaka mitano, mkuu huyo wa DSE anasema wanazitegemea sekta zenye mchango mkubwa katika uchumi hasa kipindi hiki Serikali inaposimamia mpango wa kuwa na uchumi wa viwanda ambao unahitaji mtaji mkubwa ambayo ni nafuu, ikiwezekana kutoka vyanzo vingine licha ya benki za biashara hasa soko hilo.

“Tunaitazama sekta ya kilimo pia kwa ukaribu kutokana na mchango wake kwenye ajira kwa vijana na umuhimu wake katika maisha ya wananchi kwa ujumla hivyo tukipata kampuni nyingi kutoka katika sekta hivyo tutapata mafanikio makubwa,” anasema Moremi.

Kadhalika sekta ya kibenki na miundombinu ni eneo jingine lenye fursa za kukuza uchumi wa Taifa kupitia soko la hisa kwani ili viwanda viweze kufanya kazi kwa ufanisi unaotakiwa ni lazima pawe na miundombinu imara.