Somo kutoka Ghana kwa Akufo, ‘wilaya moja kiwanda kimoja’

Muktasari:

  • Ni sawa ana ilivyokuwa Ghana. Katika Uchaguzi Mkuu Desemba 2016, Rais Nana Akufo-Addo kutoka NPP, aliomba ridhaa ili atawanye viwanda kila kona ya nchi hiyo, ahadi iliyobatizwa jina la “Wilaya Moja, Kiwanda Kimoja”.

Alipokuwa kwenye kampeni za urais mwaka 2015, Dk John Magufuli alijinadi kuwa anataka kuielekeza nchi kwenye uchumi wa viwanda. Ahadi hiyo ilipewa jina la “Tanzania ya Viwanda.”

Ni sawa ana ilivyokuwa Ghana. Katika Uchaguzi Mkuu Desemba 2016, Rais Nana Akufo-Addo kutoka NPP, aliomba ridhaa ili atawanye viwanda kila kona ya nchi hiyo, ahadi iliyobatizwa jina la “Wilaya Moja, Kiwanda Kimoja”.

Rais Magufuli aliapishwa Novemba 5, 2015 sasa ametimiza miaka miwili madarakani. Oktoba 2020, akitaka atarejea kwa wapigakura kuomba ridhaa ya kuongezwa kipindi cha pili.

Rais Akufo-Addo alikula kiapo cha kuiongoza Ghana kwa miaka minne Januari 17. Katika uchaguzi huo Akufo-Addo alimshinda Rais aliyekuwa madarakani, John Mahama.

Tanzania na Ghana ni nchi ambazo katika miaka ya 6, ziliweka mkazo mkubwa wa sera ya viwanda kwa lengo la kuyaelekeza mataifa hayo kwenye uchumi unaotokana na uzalishaji kuliko makusanyo ya kodi. Tanzania ilikuwa chini ya Mwalimu Nyerere, Ghana chini ya Kwame Nkrumah.

Kama ilivyotokea Ghana, sera ya viwanda kutofanikiwa na vilivyokuwepo kufa kwa sababu ya ukosefu wa uongozi sahihi, ndivyo na Tanzania ambavyo viwanda vingi viliingiza hasara badala ya faida, mwisho vikabinafsishwa kwa watu ambao baadhi wameshindwa kuviendeleza.

Tofauti na utekelezaji wa miaka ya sitini na sabini kwa nchi zote mbili kuwa chini ya Serikali, awamu ya sasa sekta ya viwanda siyo ya umma, bali watu binafsi, hivyo Serikali ina wajibu wa kuandaa mazingira yenye kuvutia na kuirahisishia sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda.

Kutokana na mkazo wa sera hiyo kwa nchi zote mbili na mafanikio ambayo Ghana imeanza kuyapata ndani ya muda mfupi wa utawala wa Akufo-Addo, inapendeza kuishauri Tanzania ione cha kujifunza.

Walichofanya Ghana

Akufo-Addo amebobea katika fani ya sheria, hivyo hajabobea sana katika uchumi. Hata hivyo, kwenye kutimiza malengo ya kiuchumi kwa nchi, anayo bahati ya kuwa na Dk Mahamudu Bawumia, mshirika wake ambaye ni makamu wa rais aliye nguli wa uchumi.

Buwamia ni bingwa wa uchumi ambaye shahada yake ya uzamivu inampambanua kama mbobezi wa uchumi kivitendo, kimuundo, kitabia na kiuamuzi. Pia ni mtaalamu asiyetiliwa shaka katika Uchumi wa Kimataifa, Uchumi wa Maendeleo na Sera ya Fedha.

Kabla ya NPP kumteua Buwamia kuwa mgombea mwenza wa Akufo-Addo, alikuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu Ghana, hivyo sera za kiuchumi na maendeleo ya kibenki kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa nchi, zimelala kwenye kichwa chake.

Hiyo ndiyo sababu masuala mengi ya kiuchumi yanasimamiwa moja kwa moja na Buwamia. Na kwa usimamizi huo, Serikali ya Akufo-Addo iliona umuhimu wa kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika biashara nyingi, ushuru, Kodi ya Ongezeko la Mtaji ili kuifanya sekta binafsi ipumue, ifanye biashara na ipate fedha.

Machi 12, mwaka huu, katika mkutano wa kutiliana saini makubaliano ya kutokutoza kodi mara mbili kwa bidhaa ziingiazo na kutoka kati ya Ghana na Mauritius, uliofanyika Mauritius, Buwamia alisema, bajeti mpya Ghana kwa mwaka 2017-2018, kodi nyingi zimefutwa ili kuipa uhai sekta binafsi.

“Lengo letu ni kuifanya Ghana kuwa nchi rafiki zaidi kibiashara na uchumi Afrika. Nchi rafiki kibiashara na uchumi wa watu Afrika. Ndiyo maana tumeondoa VAT kwenye uwekezaji wa biashara zisizohamishika. Tumefuta ushuru kwenye uingizaji wa mitambo yenye kutumika kutengeneza viwanda,” alisema Buwamia.

Alisema kuwa kodi nyingine zilizofutwa ni VAT katika usafiri wa ndani wa ndege, huduma za kifedha, ushuru wa uingizaji wa malighafi za viwandani na vipuri vya aina zote, vilevile wamepunguza VAT kwa wafanyabiashara wadogo kutoka asilimia 17 mpaka asilimia 3.

Msingi wa kuondoa kodi na ushuru kwa sehemu kubwa Ghana, upo kwenye maeneo makuu mawili, kwanza ni kuiondoa nchi kwenye uchumi wa kodi kisha kujielekeza kwenye uchumi wa uzalishaji. Ulimwengu wa leo, uzalishaji unafanywa na sekta binafsi, hivyo ni lazima ipewe nguvu.

Pili sera ya ‘wilaya moja, kiwanda kimoja’ ni ya Serikali lakini inatekelezwa na sekta binafsi kwa asilimia 100. Hivyo, Serikali inapaswa kuandaa, kutengeneza na kuboresha mazingira kwa wafanyabiashara, lakini muhimu zaidi ni kuwajengea vivutio ili wavutiwe kuwekeza kwenye viwanda.

Huwezi kuwa unataka mfanyabiashara awekeze kwenye viwanda wakati mazingira ya kibiashara ni magumu. Mfanyabiashara anabanwa hata kukuza mtaji, kwani anakatwa kodi kadiri anavyoongeza mtaji. Na viwanda vinahitaji mtaji mkubwa. Anafikaje huko?

Tanzania inaweza kujifunza kwanza kwa Ghana kutokana na mazingira ambayo Serikali imetengeneza kufanikisha sera yake ya ‘wilaya moja, kiwanda kimoja. Mazingira yenye kushawishi wafanyabiashara kuwekeza kutokana na unafuu mkubwa wa kodi ambao umewekwa.

Matokeo ya Ghana

Unadhani baada ya Ghana kufuta kodi maeneo mengi ili kuwarahisishia wafanyabiashara kuwekeza kwenye viwanda, mapato ya nchi yameporomoka? La! Ripoti ya Benki ya Dunia inaipata jeuri kuwa sera zake za kiuchumi kuelekea uchumi wa viwanda kila wilaya ni bora na ni mwafaka.

Ukuaji wa sekta ya viwanda ni wa kishindo, kwani imepanuka kwa asilimia 11.5, wakati ukuaji wake ulikuwa asilimia 1.8 mwaka jana. Katika eneo hilo, unaweza kuona kasi ya Ghana kuyafikia malengo ya uchumi wa viwanda kabla ya Serikali ya Akufo-Addo haijatimiza mwaka mmoja.

Sekta ya kilimo imekua kwa asilimia 7.6 kutoka asilimia 5. Hii inatokana na ukweli kwamba ukuaji wa viwanda siku zote huchochea kukua kwa kilimo kwa sababu uzalishaji wa bidhaa hutegemea malighafi ambazo nyingi hutoka shambani. Upande mwingine mfumuko wa bei umeshuka kufika asilimia 11.9 Julai mwaka huu, kutoka asilimia 12.4 Desemba mwaka jana.

Juni mwaka huu, mzani wa biashara kwa maana ya uwiano wa thamani ya fedha kati ya mauzo nje ya nchi na uagizaji wa bidhaa kutoka nje umekuwa chanya, kwa maana mauzo ya nje yamezidi kwa dola 1.43 bilioni (Sh3.2 trilioni), sawa na asilimia 3.1 ya Pato la Ndani la Taifa (GDP), wakati mwaka jana mzani ulikuwa na nakisi ya asilimia 3.3.

Matokeo hayo ya mzani wa biashara kuwa chanya, kwa maana ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi kuwa na thamani kubwa kuliko yale ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kufukia nakisi ya mwaka jana, kisha kuleta ziada ya Sh3.2 trilioni, ni kipimo chenye kuwasha taa ya kijani kuhusu mwanzo mzuri wa uchumi wa uzalishaji.

Matokeo mengine ni kuwa akiba ya fedha za kigeni imepanda kutoka dola 4.9 bilioni (Sh11 trilioni) Desemba mwaka jana mpaka kufikia dola 5.9 bilioni (Sh13.3 trilioni) Julai mwaka huu. Hiki ni kipimo kingine chenye kuashiria uimara wa nchi kibiashara.

Matokeo zaidi

Oktoba 3, mwaka huu, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Ghana, Robert Lindsay, alifanya mahojiano katika kipindi cha Citi Breakfast Show cha redio Citi Fm ya Accra, na kueleza uelekeo wa utekelezwaji wa sera ya ‘Wilaya moja, kiwanda kimoja’ kwamba mafanikio ni makubwa.

Lindsay alisema, mazingira bora ambayo Serikali ya Ghana imeyaweka kwa ajili kuirahisishia sekta binafsi kufanya biashara yamewezesha mpaka sasa kuwa na viwanda 173 ambavyo vinaendelea kujengwa, huku maombi mengi zaidi yakiendelea kufanyiwa kazi.

“Kwa muda sasa, tumeendelea kupokea maombi ya wafanyabiashara kujenga viwanda, wenye kuomba ni wafanyabiashara wa ndani na nje ya Ghana. Tumeshapokea maombi 600 ya kujenga viwanda na mipango ya biashara ya kuwekeza kwenye viwanda tuliyopokea mpaka sasa ni 457,” alisema Lindsay.

Alichokisema Lindsay kinaakisi moja kwa moja takwimu za Benki ya Dunia kuhusu matokeo ya ukuaji wa kiuchumi wa Ghana tangu kuingia kwa Serikali ya Akufo-Addo na makamu wake, Dk Buwamia. Inaonekana dhahiri kuwa wawekezaji wanakimbilia Ghana, kwani wanaona ni fursa iliyorahisishwa.

Ghana ina wilaya 216, hivyo kama viwanda vyote 173 alivyosema Lindsay vitakamilika ndani ya mwaka mmoja mpaka miwili, maana yake kutakuwa na upungufu wa viwanda 43 tu. Na ukifuata maombi na mipango ya uwekezaji, ni wazi inawezekana kufikisha hata viwanda vitatu kila wilaya.

Kizuri zaidi kwa Ghana ni kuwa mipango yao ya kujenga viwanda inafuata aina ya malighafi kwenye wilaya. Busara hiyo inasaidia kuchangamsha sekta nyingi, kwamba wakati nchi ikizalisha bidhaa, inawezesha maendeleo ya kibiashara kuwa makubwa na soko la wakulima kuwa la uhakika.

Hayo ndiyo mambo ambayo yanavutia kwa Ghana na yanaweza kuifaa Tanzania. Kutoa unafuu wa kodi na kuweka mazingira rahisi kwa wafanyabiashara ili kukuza mitaji yao na kuwekeza. Mazingira ya kibiashara yakiwa magumu ni vigumu mfanyabiashara kuvutiwa kujenga kiwanda. Na izingatiwe kwamba Serikali haijengi viwanda.