Suma JKT yajipanga kuchimba madini, kumjengea nyumba kila askari

Thursday November 9 2017

Mkurugenzi mtendaji wa Suma JKT, Brigedia

Mkurugenzi mtendaji wa Suma JKT, Brigedia Jenerali Charo Yateri akiwa ofisini kwake jijini Dar es Salaam alikozungumza na gazeti hili na kubainisha mipango ambayo shirika hilo linapanga kuitekeleza siku zijazo. Picha na Julius Mnganga. 

By Julius Mnganga, Mwananchi; [email protected]

Hakuna taifa linaloendelea kwa kuwategemea watu wa nchi nyingine. Maendeleo ya uhakika huletwa na wazawa.

Uwapo wa rasilimali za aina tofauti kuanzia madini, mbuga, ardhi safi, wanyamapori, nguvukazi ya uhakika na viumbetiba, uendelezaji makini usipofanywa taifa haliwezi kuendelea.

Taifa lenye uchumi makini linatokana na wananchi wanaojiweza. Mabadiliko ya sheria na sera za rasilimali za taifa yaliyofanywa hivi karibuni inalenga kuinufaisha zaidi Tanzania na wananchi wake.

Katika juhudi hizi, serikali imeanza kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na ufanyaji biashara sambamba na kukaribisha uwekezaji zaidi kutoka nje. Yote haya yanafanywa ili kuijengea uwezo sekta binafsi ili kuongeza mchango wake kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuongeza ubunifu wa sayansi na teknolojia pamoja na kuongeza ajira.

Mkakati wa maendeleo uliopo ni kuongeza mchango wa sekta ya viwanda mpaka asilimia 40 kwenye Pato la Taifa (GDP) na kuajiri zaidi ili kupunguza uhaba wa ajira uliopo kwa zaidiya wahitimu 800,000 wanaoingia sokoni kila mwaka.

Sekta ya madini pia ina fursa nyingi za kufanikisha malengo ya serikali. Kwa kutambua hilo, Shirika la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) linakusudia kuanza uchimbaji wa madini ya aina tofauti.

Mkurugenzi mtendaji wa Suma JKT, Brigedia Jenerali Charo Yateri anasema katika mkakati wa miaka mitano wa shirika hilo, uchimbaji wa madini ni miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele.

“Tuna mipango mingi inayohitaji kutekelezwa. Mwaka wa fedha 2020/21 tutaanza uchimbaji wa madini,” anasema brigedia huyo anayejivunia nguvukazi ya kutosha aliyonayo kwenye shirika hilo kufanikisha mipango iliyopo.

Mipango hii inabainishwa wakati serikali ikilalamika udanganyifu unaofanywa na wawekezaji, wengi wa kimataifa kwenye sekta hiyo hivyo kutolipa kodi kama inavyotakiwa.

Hivi karibuni, Mamlaka ya Mapato (TRA) iliipiga faini ya Dola 190 bilioni (zaidi ya Sh424 trilioni) kampuni ya Acacia ambazo zilijumuisha kodi, faini na riba kwa udanganyifu ilioufanya kwa zaidi ya miaka 20 ya kuchimba madini nchini.

Licha ya udanganyifu huo, baadhi ya wawekezaji wamekuwa na migogoro na jamii zinazozunguka migodi suala ambalo Suma JKT imejipanga kuliepuka.

“Tutashirikiana na wachimbaji wadogo waliopo kwa kuwapa mafunzo yanyohitajika kama tunavyofanya maeneo mengine,” anasema akibainisha mikakati mingi iliyopo.

Licha ya uchimbaji, shirika hilo linatarajia kuanza uvuvi katika bahari kuu na kujenga kiwanda cha kusindika samaki, kiwanda cha vifaa vya umemejua, kufungua duka la silaha na risasi pamoja na kufungua vituo vya mafuta kwenye kanda saba nchini.

Biashara

Lengo la kuanzishwa kwa shirika hilo, kamnda huyu anasema ni kuipunguzia serikali gharama za uendeshaji za JKT na kuongeza mchango wake kwenye pato la serikali.

Katika kufaniisha hili, anasema miradi na mipango mbalimbali inatekelezwa. Anasema maandalizi yamekamilika na mwezi ujao watazindua kiwanda cha maji ya kunywa ambayo yatatumika kwanza jeshini kabla ya kusambazwa kwenye vikosi vyote vya ulinzi na usalama.

“Maji yetu yataitwa Uhuru Peak. Tumewekeza Sh1.4 bilioni kuagiza mitambo yenye uwezo wa kuzalisha chupa 4,800 za ujazo wa nusu lita kwa saa moja. Kitakuwa Mgulani. Ndani ya miaka miwili tunatarajia gharama za uwekezaji zitakuwa zimerudi na tutaanza kupata faida,” anasema brigedia jenerali huyo.

Akijivunia zaidi ya ajira 5,000 zilizotolewa kwa vijana ndnai ya shirika hilo, Yateri anasema mtazamo wa shirika hilo lililoanzishwa likiwa na mashamba mengi yaliyokuwa yanatumika kuzalisha chakula kwa ajili ya askari.

Anasema shirika lina hekta 2,000 lakini mtazamo wake umebadilika hivi sasa na linajipanga kuendesha kilimo cha kisasa kitakachotumia zana na mitambo ya kisasa kuzalisha chakula kingi kitakachochangia kwenye hifadhi ya serikali pia.

Anasema kutokana na mabadiliko hayo, wamepunguza mashamba waliyonayo na kubakiwa na matatu ambayo ni Chite lililopo Morogoro linalozalisha mpunga, Mlundikwa lililopo mkoani Rukwa na jingine wilayani Tanganyika yanyozalisha mahindi na mpunga.

Wakati ikijipanga kwa namna hiyo, anasema inaanzisha viwanda vingi kwa ajili ya kuongeza thamani za mazao ya kilimo, mbolea na mbegu bora ambazo kwa muda mrefu imekuwa ni changamoto inayowakabiri wakulima.

“Mwaka huu wa fedha tumepanga kujenga maghala ya nafaka na kiwanda cha majitiba ambayo yatauzwa nchini hata nje. Kuna kumbi mbili zinaendelea kujengwa Mwenge, mmoja utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 1,500 na nyingine 1,000,” anasema.

Nyumba za askari

Wakati benki za biashara na taasisi za fedha kwa ujumla zikijikita kutoa mikopo ya nyumba kwa riba ya soko, Jenerali Yateri anasema upo mpango kama huo kwenye shirika lake.

Kwa kutambua changamoto hasa za makazi zinazowakabili wastaafu, anasema mmwaka shirika lake litaanza kuwajengea askari wote nyumba za bei nafuu kwa mkopo unaolipika.

“Mwakani ujenzi huo utaanza. Utakuwa ni ubia kati yetu na benki za biashara. askari ataruhusiwa kuomba mkopo na kujengewa nyumba aitakayo. Tutajenga kuanzia nyumba ya Sh30 milioni mpaka Sh200 milioni kulingana na uwezo wa askari,” anasema.

Tangu kuanzishwa kwa Shirika la Mikopo ya Nyumba (TMRC) takriban miaka minane iliyopita, tayari zaidi ya benki 20 zimejiunga nalo ili kutoa mikopo nafuu ya nyumba kwa madhumuni ya kuboresha makazi ya Watanzania.

Kama kutakuwa na wadau wa kutosha, mkurugenzi huyu anasema wataangalia namna ya kuongeza wigo kwa watumishi wengine wa umma ili kuinua hali zao na kuwaondoa kwenye nyumba duni baada ya kustaafu utumishi serikalini.

Mikataba mibovu

Kwa muda mrefu, suala la mikataba mibovu baina ya taasisi za serikali na wawekezaji wa kimataifa limekuwa likilalamikiwa kutokana na kutoinufaisha Tanzania.

Mara kadhaa wabunge wamesimama na kueleza juu ya hilo wakitaja baadhi ya taasisi za umma. Kwa nyakati tofauti, mawaziri wamekiri hilo. Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliwahi kusema mikataba mingi ya sekta ya madinini mibovu.

Hivi karibuni, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesitisha vibali vyote vya uwindaji vilivyotolewa mwaka huu akisema vilikiuka taratibu hivyo kuwa na dalili za kutolinufaisha taifa.

Hata jeshini mambo haya yapo lakini Brigedia Jenerali Yateri anasema hatua za makusudi zimechukuliwa kwa kuandaa viwango vitakavyohakikisha shirika hilo linanufaika zaidi kwenye kila ubia linaloingia.

Anasema Suma JKT imejipanga kukabiliana vilivyo. “Hawa wenzetu ni wajanja sana. Wanatorosha fedha na kupandisha bei ya mitambo na malighafi wanazonunua kutoka kwao hivyo kujinufaisha zaidi,” anasema.

Kama serikali inavyochukua hatua kushughulika mikataba yake, anasema wamebadili sera ya ubia na kuanzia sasa kampuni itakayotaka kushirikiana nao itapaswa kuwa na chini ya asilimia 60 za hisa.

Hilo linatokana na uzoefu walioupata kwenye baadhi ya mikataba ya siku za nyuma ambako shirika lilikuwa na chini ya asilimia 30 hivyo kutokuwa na ushawishi mkubwa kwenye kufanya uamuzi.

Advertisement