Sura mpya, hoja mpya kampeni za lala salama

Muktasari:

  • Kadri uchaguzi huo mdogo unavyokaribia, ndivyo vyama 12 vilivyosimamisha wagombea vinavyozidi kubadili gia angani kwa kuongeza sura mpya zenye ushawishi na uwezo wa kujenga hoja mpya za kampeni ili kuwavutia wapiga kura wengi zaidi.

Bado siku mbili wananchi wa majimbo mawili ya Siha, Kilimanjaro na Kinondoni, Dar es Salaam pamoja na kata tisa nchini wajimwage katika vituo vya kupigia kura kuwachagua wawakilishi wao.

Kadri uchaguzi huo mdogo unavyokaribia, ndivyo vyama 12 vilivyosimamisha wagombea vinavyozidi kubadili gia angani kwa kuongeza sura mpya zenye ushawishi na uwezo wa kujenga hoja mpya za kampeni ili kuwavutia wapiga kura wengi zaidi.

Tayari vyama hivyo, hasa CCM na Chadema vyenye ushindani mkubwa, vimeongeza idadi ya makada wake wanaoshiriki kwenye mikutano ya hadhara ya kampeni huku vikionekana kuanza kutumia vigogo kupiga kampeni.

Kampeni CCM

Kwa upande wa chama tawala cha CCM ambacho tayari kina kata moja ya Kimagai wilayani Mpwapwa mkononi ambayo mgombea wake alipita bila kupingwa, wabunge kadhaa pamoja na mawaziri ambao hawakupo kwenye kampeni tangu awali wamejitokeza kuwanadi wagombea wao wa ubunge Maulid Mtulia (Kinondoni) na Dk Godwin Mollel wa Siha.

Katika mkutano uliofanyika Mtaa wa Idrisa Magomeni mwisho mwa wiki waliohudhuria kampeni hizo ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile.

Kwa upande wa wabunge waliohudhuria kutoka chama hicho ni Hussein Bashe (Nzega Mjini), Musa Azzan Zungu (Ilala), Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ (Mtera), Halima Bulembo (Viti Maalumu), Steven Ngonyani ‘Majimarefu’ (Korogwe Vijijini) na Oliver Semuguruka (Viti Maalumu).

Wengine ni Sixtus Mapumba (Mbinga Mjini), Joseph Musukuma (Geita Vijijini) na Rita Kabati (Viti Maalumu).

Katika Jimbo la Siha chama hicho pia kimeendelea kuongeza nguvu ili kuwahamasisha wananchi kuchagua mbunge anayetokana nacho.

Miongoni mwa mawaziri waliofika katika kampeni za jimbo hilo ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na wabunge Mary Chatanda (Korogwe Mjini) Profesa Jumanne Maghembe (Mwanga) pamoja na Bupe Mwakang’ata, Anna Lupembe na Shally Raymond (wote Viti Maalumu).

Kampeni za Chadema

Kwa upande wa Chadema ambayo imemsimamisha Elvis Mosi (Siha) na Salum Mwalimu Kinondoni, pia sura mpya za makada zimejitokeza katika kipindi cha lala salama ili kupamba kampeni hizo na kujihakikishia ushindi.

Miongoni mwa sura hizo ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini); Makamu Mwenyekiti (bara), Profesa Abdallah Safari na aliyewahi kuwa mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali na Susan Lyimo (Viti Maalumu).

Hoja zilizotikisha

Wakati katika kipindi cha awali suala kubwa la kampeni lilikuwa ni kitendo cha wabunge kujiuzulu na kisha kuomba upya nafasi hiyo na mmoja wa wabunge kuzaliwa Zanzibar, upepo umebadilika katika kipindi cha lala salama.

Safari hii hoja kubwa zinazotikisa ni suala zima la kuleta maendeleo na nani hasa anaweza kuleta maendeleo hayo. Wakati wabunge wa upinzani wakijinadi wanaweza kujenga hoja na kushawishi, upande wa chama tawala wanadai itakuwa rahisi kwao kuleta maendeleo kutokana na kuwa karibu na Serikali.

Akiwa katika Jimbo la Siha, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anawataka wananchi kumchagua Dk Mollel ili aweze kushirikiana na Serikali kuwaletea maendeleo na kutetea kwamba anachofanyika si rushwa kwa wapigakura.

Mwalimu anasema Dk Mollel ni jembe na endapo atashinda atakuwa na nafasi kubwa ya kushirikiana na Serikali ili kutatua changamoto ambazo zimekuwa kero kwa wananchi wa jimbo hilo.

Ameahidi kuwa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha na kuboresha vituo vya afya na zahanati ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora.

Pia, anasema Serikali tayari imetuma Sh700 milioni kwa ajili ya kuboresha kituo cha afya cha Naibili na kuwa katika kipindi cha miezi tisa ijayo wataboresha zahanati ya Magadini iliyopo Kata ya Gararagua ili kuiwezesha kutoa huduma zote muhimu.

Mwalimu anasema Serikali inathamini na kuheshimu kutoa huduma bora kwa wananchi na kinachofanyika kwa sasa si rushwa bali kutekeleza ilani ya CCM.

“Hatutoi rushwa kwani ni jambo ambalo liko kwenye ilani ya CCM, Mollel tangu akiwa Chadema aliniomba kama waziri nimsaidie ujenzi wa kituo cha afya Naibili kwa kuwa hakikuwa na chumba cha upasuaji, wodi ya wajawazito, nyumba ya watumishi pamoja na maabara ya damu.”

“Tumeahidi tunampa Sh700 milioni kwa ajili ya kuboresha kituo hicho na fedha hizo tayari tumezituma katika halmashauri. Ndugu zangu tuleteeni jembe Mollel ili tufanye naye kazi,” anasema Mwalimu na kuongeza: “ Rais Magufuli amedhamiria kuipeleka Tanzania mbele na kwamba kabla hajaingia madarakani, Hospitali ya Wilaya ya Siha ilikuwa ikipewa Sh17 milioni kwa ajili ya dawa lakini sasa inapewa Sh44 milioni.”

Naibu Spika, Dk Tulia anasema wabunge wanaozungumza sana bungeni ni kutoka CCM kwa sababu wapo wengi, hivyo kuwataka wananchi kumchagua Mtulia kwa sababu hatapanga foleni kuzungumzia shida zao, nafasi yake ipo inamsubiri.

Anasema kule bungeni kuna nafasi wanakaa wanaopoteza kila mara na kuna upande wanakaa wenye Serikali yao na wenye maamuzi, “Mchagueni Mtulia akafanye maamuzi pamoja nao.

“Hatapanga foleni kubembeleza aongee kwa sababu chama chake kimeshika dola, ataongea kila anapohitaji kufanya hivyo,” anasisitiza Dk Tulia.

Kampeni ya Chadema

Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Suzan Lyimo anasema Mwalimu ni jembe amefanya kazi kubwa na kwamba ana historia isiyotiliwa shaka. Mbunge wa Kawe, Halima Mdee anasema uchaguzi wa Jumamosi si uchaguzi wa Kinondoni tu bali wa Taifa zima kwa kuwa Watanzania watakuwa wanauangalia kwa hamu kubwa.

“Uchaguzi uliopita wa kata 43 ulikuwa wa kusikitisha, kura feki ziliingizwa kwenye vituo kuipendelea CCM. Sasa wananchi watataka kufuatilia kuona katika uchaguzi huu endapo hilo litaendelea, tumechoka.”

“Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, tunajua mbinu zao zote tunawaomba waache, iwe mvua, liwe jua tunataka mwenye haki apewe ubunge awe Mwalimu, awe Mtulia vinginevyo hatutavumilia.”

Kampeni za CUF

Katika kampeni za CUF, mgombea wa CUF, Rajabu Salum naye ameendelea kupata sapoti ya makada wa chama hicho, zikiwamo sura mpya, huku wakiendelea kumbaa mgombea wa CCM, Maulid Mtulia aliyehama chama na kutelekeza ubunge kupitia chama hicho.

Aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu CUF, Hassan Khamis anasema Februari 17 ndio siku wananchi wa Kinondoni watapimwa akili kama wataamua kumchagua mbunge waliyemuamini wakamchagua na kisha kujiuzulu.

Khamis anasema atashangaa sana kuna CCM ikishinda kwa kuwa imeishiwa hoja na kueleza kwamba jimbo hili ni la CUF.

Amesema CCM na Serikali yake inayojinadi kubana matumizi leo hii imeigharimu nchi kutumia zaidi ya Sh1 bilioni ambazo zingeweza kujenga madarasa au kununua dawa za kutisha katika hospitali.

“Tabia ya usaliti aliyoifanya Mtulia hajaanza jana wala leo, kwani alishauza dakika za mwisho ujumbe wa klabu ya Simba.”