TAFAKURI YA ABU IDDI: Watanzania tumeelimika kisiasa?

Muktasari:

  • Ukweli ni kwamba vyama vya siasa haswa vya upinzani havina uongozi makini na hayo yanajidhihirisha pale ambapo kila chama kinaweza kuhusishwa na matakwa ya ‘mtu mmoja’ kwamba atakavyo yeye ndivyo itakuwa na siyo vyenginevyo.

Wadau wa tafakuri leo tuzamishe fikra zetu tutafakari juu ya matukio kadhaa yanayohusishwa na ushindani wa kisiasa katika mfumo huu wa siasa za vyama vingi katika nchi yetu kisha tujiulize: Je, tumeelimika kwa kuzielewa itakiwavyo siasa za vyama vingi au laa?

Ni vyema tukafahamu kwamba uhai wa mfumo wa siasa za vyama vingi umeshatimiza takriban miaka 20 na tayari tumeshashuhudia Uchaguzi Mkuu mara tano tangu mfumo huo uliporudishwa nchini mwaka 1992. Tumejifunza mengi.

Katika mfumo mzima wa siasa za vyama vingi ni vyema tukayaangazia mambo makuu matano na kisha ndipo tubaini kwamba: Je, Watanzania tumeelimika au bado tunahitaji kuelimishwa?

Jambo la kwanza ni umakini wa uongozi katika vyama vya siasa. Ukweli ni kwamba vyama vya siasa haswa vya upinzani havina uongozi makini na hayo yanajidhihirisha pale ambapo kila chama kinaweza kuhusishwa na matakwa ya ‘mtu mmoja’ kwamba atakavyo yeye ndivyo itakuwa na siyo vyenginevyo.

Imefikia chama kuhusishwa na mtu kwamba chama fulani mwenyewe ni fulani na anajulikana na hata ‘majaribio’ kadhaa yamejieleza na kuonyesha wazi kwamba endapo ukigombana na ‘mwenye chama’ basi atakufukuza na taratibu za vikao ni mfumo wa kuhalilisha kufukuzwa kwako lakini uamuzi anao yule mwenye chama chake.

Watanzania tuambizane ukweli kwamba ukikiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM), vyama vyote vilivyobakia kila chama kina ‘mwenyewe’. Kwa hiyo, tatizo kubwa ndani ya vyama vya upinzani ni kukosekana uhalisia wa demokrasia ya kweli kwa sababu katiba na sera za vyama vyao ni nzuri lakini haviendeshwi kwa mujibu wa katiba zao vinaangalia zaidi fikra na uamuzi wa yule mwenye chama chake.

Je, hapo tumeelimika kisiasa katika mfumo huu wa siasa za vyama vingi wakati umekosekana umakini katika uongozi? Na sababu kubwa ya kukosekana uongozi makini ni kwa kuwa ‘unakwazwa’ au unalazimika kufuata na kutii matakwa ya ‘mwenye chama’.

Jambo la pili ni sababu zinazomsukuma mwanachama wa chama fulani kuhamia chama kingine. Kwa bahati mbaya, wanachama wengi wanaohama kutaka chama fulani kwenda chama kingine wanafanya hivyo kwa sababu binafsi tena ni za kuchunga na kulinda masilahi yao.

Anayekosa nafasi ya kugombea udiwani, ubunge, urais na kadhalika kupitia chama fulani anakihama chama hicho na kwenda katika chama ambacho ataipata fursa hiyo ili kukidhi matakwa yake ya kuwa mgombea katika nafasi husika.

Sababu hii ni dhaifu kwani inaonyesha ‘ubinafsi’ kwamba ni lazima niwe mimi katika uongozi fulani. Akishakihama chama chake cha zamani anageuka kuwa ‘turufu’ katika chama kingine na anaanza kazi ya ‘kukiponda’ wakati zamani alikuwa ‘anakipenda’.

Ni bora mwanasiasa ambaye ameiona demokrasia katika chama fulani ni pana zaidi (kwa dhana yake) akaamua kuhamia huko hata kabla ya ‘kufukuzwa’ au kunyimwa nafasi katika chama chake cha zamani.

Kama ambavyo hali tumeizoea hivi sasa, siasa za vyama vingi zimegeuzwa kuwa ni ‘faraja’ kwa wale wenye tamaa ya uongozi kwamba akiukosa kupitia hapa ataupata kupitia kule. Hii ni moja ya vigezo kwamba bado hatujaelimika katika mfumo wa siasa za vyama vingi.

Jambo la tatu ni uhusiano wa kijamii kati ya viongozi ya vyama na viongozi wengine na kati ya wanachama na wenzao wa vyama vingine. Hali ya uhusiano wa kijamii hairidhishi kwani tumeshuhudia baadhi ya wapenzi na washabiki wa vyama wakipigana, wakinyimana amani na wenzao wa vyama vyingine.

Yapo pia matukio kadhaa ya kunyimana huduma za kijamii kama vile kuuziana, huduma za usafiri na kadhalika kutokana na kutoelewana kulikosababishwa na tofauti za mitazamo ya kisiasa.

Wapo pia waliolazimika kuzihama nyumba za ibada na hata wale walionyima huduma za mazishi kutokana tu na misigano ya vyama vingi vya siasa. Katika hali hiyo ni kipimo tosha kwamba bado hatujaelimika kisiasa katika mfumo wa siasa za vyama vingi.

Jambo la nne ni mtazamo wa chama tawala kwa vyama pinzani vya siasa. Ukweli ni kwamba  badala ya chama tawala kuviangalia vyama pinzani vya siasa kwa ‘jicho jema’ kama vyama vyenye nia na malengo ya kushika dola na kutoa changamoto kwa Serikali ili iwajibike ipasavyo kwa wananchi, chama tawala kinaonyesha kuwa upinzani ni kama ‘uhalifu’ na kuwachukulia wapinzani ni kama ‘wahalifu’ fulani ambao jamii inatakiwa kuwaepuka, jambo ambalo halina usahihi.

Wapinzani ni washindani wa CCM kisiasa na kamwe siyo ‘waasi’ katika Serikali ya CCM.

Jambo la tano ni mtazamo wa vyama vya upinzani kwa Serikali iliyoko madarakani na kwa chama tawala.

Mtazamo wa vyama vya upinzani kwa Serikali bado haujaonyesha ukomavu wa siasa za vyama vingi kwani mara nyingi vyama vya upinzani vimekuwa vikipinga tu bila ya kufungulia milango ya kupongeza pale Serikali inapofanya vyema.

Upinzani umekuwa ni upinzani haswa jambo ambalo siyo sahihi.

Kuna wakati viongozi wa upinzani wanalalamikia jambo fulani ambalo ndani yake lina ukweli na masilahi kwa Watanzania lakini Serikali inapochukua hatua kuhusu jambo hilo, badala ya wapinzani hao kupongeza na kuunga mkono hatua ya Serikali wanaanzisha ajenda mpya ili jamii isitazame ‘mema’ ya Serikali.

Ni vyema tubadilishe jina badala ya kuviita vyama vya upinzani tuviite ni vyama vya siasa tu kwani huenda ile dhana ya kuwa wapinzani inawalazimisha kupinga kila jambo hata kama liwe jema.

Takriban miaka 20 sasa tangu nchi yetu iingie katika mfumo wa siasa za vyama vingi; Je, Watanzania tumeelimika kisiasa?

Haya na tutafakari.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation. Unaweza kuwasiliana naye kwa namba: +255 754 299 749, +255 784 299 749.