TEHAMA : Usichokijua kuhusu teknolojia ya AI

Muktasari:

Kwa mfano, leo mtu anaweza kupiga simu akajibiwa na mashine. Pia, mashine hiyo inaweza kupiga simu na kutoa maelezo, kuuliza maswali na mengineyo.

Ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita tumejionea maendeleo kadhaa duniani hasa kwenye nyanja za mawasiliano.

Kwa mfano, leo mtu anaweza kupiga simu akajibiwa na mashine. Pia, mashine hiyo inaweza kupiga simu na kutoa maelezo, kuuliza maswali na mengineyo.

Mtu anapoingia katika tovuti za baadhi ya kampuni anaweza kuuliza au kuongea na mtoa huduma na kudhani anaongea na mtu halisi kumbe ni mashine iliyojengwa katika mfumo wa kompyuta.

Baadhi ya migahawa katika nchi zilizoendelea kama Japan ina mashine zinazoweza kukaribisha watu na kutoa orodha ya chakula kisha mtu anachagua na kupelekewa alipokaa.

Teknolojia hii inajulikana kitaalamu kwa jina la Artificial Intelligence (AI).

AI ni uwezo wa mashine kufanya kazi na majukumu kama vile anavyofanya binadamu. Baadhi ya vitu ambavyo binadamu wanaona ni rahisi, kwa mashine inaweza kuwa tabu kidogo kama kutambua kitu katika picha, kuendesha gari, kushika na vinginevyo.

Hata hivyo, mashine zinaweza kumshinda binadamu kwenye vitu kama kucheza michezo ya kompyuta, lakini haiwezi kujifunza jinsi ya kucheza au kufanye mengineyo.

Uwezo wa mashine kufanya kazi za binadamu umeanza kuathiri sekta nyingi za ajira na kazi za kawaida ambazo zilikua zinaingiza kipato kwa watu.

Fikiria madereva wa magari walivyo wengi duniani na kama kila aliyeajiri madereva ataamua kutumia magari yasiyokuwa na madereva nini kitatokea kwa mamilioni ya watu hawa?

Hata hivyo, lazima nikiri kuwa AI nayo ina changamoto zake kwa kuwa bado mashine hizo zinamhitaji zaidi binadamu.

Kutokana na mifano kadhaa niliyotoa hapo juu, sasa kuna umuhimu wa nchi kama Tanzania kujipanga kikamilifu ili kuweza kuendana na kasi hiyo ya tekinolojia kwa kipindi kirefu kijacho na tukifanya vizuri tunaweza hata kuuza nje na kupatia vijana wetu fursa za ajira na mapato .

Kwanza tunaweza kuchagua kusomesha watu wa fani mbalimbali kuhusu masuala ya AI katika maeneo mengine duniani. Watakaporudi tunaweza kuanzisha au kuwa na maeneo maalumu ndani ya vyuo kwa ajili ya AI na kufanya utafiti na mengine mengi.

Vijana hawa watatengeneza mitalaa ya AI kwa ajili ya kutumika katika taasisi za elimu kuanzia chekechea mpaka vyuo vikuu na maeneo mengine ambayo mashine zinatumika au zitakuja kutumika katika kurahisisha kazi za binadamu .

Hapo tunaweza sasa kuanzisha kozi maalumu fupi au ndefu za watu watakaofanya kazi katika AI kwa ujumla kuanzia kilimo, huduma za usafiri, mawasiliano, miundombinu, biashara na mengine mengi.

Mfano kwenye fani zote za AI, kuna suala la kuandika programu za kutumika na mashine ili zielewe na kutenda inavyotakiwa.

Hapa Tanzania tunatumia Kiswahili, kwa hiyo mashine lazima ziseme Kiswahili na kuwa na maadili ya Kiswahili kwa ajili ya kutumika na jamii. Huu ni mfano mdogo na muhimu sana kuujua.

Lazima tuwekeze sasa kwa kupeleka vijana kusoma, wakirudi watafundisha na kuleta mawazo na fikra mpya kwa ajili ya kizazi kijacho ili nacho kifaidi matunda ya ukuaji wa sayansi na tekinolojia.

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwananchi au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz