TEWW: Kutoka kisomo cha ngumbaru hadi kampeni za Tanzania ya viwanda

Muktasari:

  • Ni miongoni mwa taasisi kongwe za elimu nchini zilizovuma kwa kiwango kikubwa miaka ya 1970 na 1980.
  • TEWW ilianzishwa mwaka 1960 kama sehemu ya kitengo cha mafunzo ya ziada cha Chuo Kikuu kishiriki cha Makerere Kampala, Uganda ambacho kilikuwa chini ya Chuo Kikuu cha London, Uingereza.

Unapotaja taasisi kongwe za elimu nchini, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), haiwezi kukosekana kwenye orodha.

Ni miongoni mwa taasisi kongwe za elimu nchini zilizovuma kwa kiwango kikubwa miaka ya 1970 na 1980.

TEWW ilianzishwa mwaka 1960 kama sehemu ya kitengo cha mafunzo ya ziada cha Chuo Kikuu kishiriki cha Makerere Kampala, Uganda ambacho kilikuwa chini ya Chuo Kikuu cha London, Uingereza.

Mojawapo ya mafanikio makubwa katika historia taasisi hii ni kusaidia harakati za Serikali ya awamu ya kwanza kuhakikisha Watanzania wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu kupitia mpango uliojulikana kwa jina la ngumbaru

Enzi hizo kiwango cha wananchi kujua kusoma kilifikia asilimia zaidi ya 80 hali iliyosukuma Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kutoa tuzo maalumu kwa Tanzania.

Mbali ya kutoa elimu ya darasani taasisi hiyo pia imejikita kuelimisha jamii kuhusiana na masuala mbalimbali yanayojitokeza.

TEWW na mchango katika viwanda

Katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuifanya Tanzania nchi ya viwanda, taasisi ya elimu ya watu wazima nayo imeonyesha mwitikio chanya.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo Dk Fidelice Mafumiko anasema tayari wameanza kushirikiana na wadau kutoa elimu katika maeneo mbalimbali, ili kuwajengea uelewa Watanzania juu ya dhana ya viwanda.

“Dhana ya viwanda inapaswa kuingia kichwani kwa mtu mmoja mmoja; mwenyewe atambue umuhimu wa ushiriki wake katika hili na kufahamu kuwa yeye anaweza kuwa kiwanda,” anasema.

Anafafanua elimu hiyo inalenga kumkomboa mtu mmoja mmoja kifikra ili popote alipo dhana ya viwanda iingie kichwani mwake na awe tayari kuifanyia kazi.

Kando na hilo programu za elimu zinazotolewa na taasisi hiyo zinalenga kumfanya mtu ajitambue, atambue changamoto zake na kutafuta namna ya kukabiliana nazo.

Dk Mafumiko anasema kuwa nchi ya viwanda haimaanishi kuwa kuna watu watatoka nchi nyingine kuja kuanzisha viwanda vipya, bali Watanzania wenyewe kila mmoja kwa nafasi yake afikirie kiwanda katika shughuli zake za uzalishaji.

“Tunashukuru kwanza kwa utashi wa kisiasa umeonekana katika hili, Serikali imeamua kwa dhati kusimamia suala la viwanda, kinachotakiwa sasa ni kulipeleka hilo kwa Watanzania wa kawaida kabisa.

‘’Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, tunaifanya kazi hii kwa kuwafuata Watanzania huko waliko, hatuna sababu ya kutegemea wawekezaji tukiamua kwa pamoja tunaweza kutimiza azma hii na tukapata mafanikio,”anaeleza.

Miradi ya taasisi

Taasisi hiyo ina miradi kadhaa ambayo inawafuata Watanzania katika maeneo yao mmoja wapo ukiwalenga wasichana na kupiga vita ndoa za utotoni.

Moja ya miradi hiyo, uliopo katika mikoa ya Lindi, Rukwa na Dodoma, unaendeshwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na mashirika ya Sido na Kiwohede.

Mkuu wa Idara ya elimu kwa umma na maendeleo ya wanawake wa taasisi hiyo, Leonia Kassamia anasema mradi huo unalenga wasichana wenye umri kati ya miaka 10-25.

Anasema kundi hilo lipo kwenye hatari ya kuingia kwenye ndoa za utotoni au tayari wameshaingia na kusababisha wakose fursa ya kupata elimu.

Hivyo mradi, anasema unalenga kuwakomboa kifikra na kuwarudisha kwenye mstari wale waliokata tamaa.

“Wengi wakishaingia kwenye ndoa wanakata tamaa, kama walikuwa wanasoma wakikatisha masomo wanaona huo ndiyo mwisho wa safari, wakati bado wanaweza kujishughulisha na uzalishaji na wakachangia katika ujenzi wa taifa, anasema na kuongeza:

“Tumeliona hilo na ndiyo maana tumeunganisha nguvu na wenzetu wa Kiwohede ambao wao wanafanya kazi ya kuwakusanya wasichana hawa kisha taasisi ya elimu tunaenda kuwafundisha mambo mbalimbali, halafu Sido wanakuja na mbinu za biashara na ujasiriamali”.

Anasema muunganiko huo unalenga kuwajengea uwezo wasichana hao kuwa tayari kuanzisha viwanda vidogo vidogo katika mazingira yao yanayowazungukua ili kujikwamua kiuchumi.

Mradi huo wa miaka mitatu unalenga kuwafikia wasichana 3000 na tayari umeshaanza matokeo chanya katika maeneo ambayo elimu imeanza kutolewa.

“Mwitikio ni mkubwa, pamoja na elimu kuna vingi ambavyo tunajifunza na kuvigundua kila kukicha. Kwa mfano, awali mabua ya mahindi yalikuwa yakitupwa lakini sasa tumegundua kuwa yanaweza kutumika kama chakula cha mifugo. Kwetu hicho ni kiwanda, mtu akiwa na uwezo wa kupukuchua mahindi kwa haraka tayari hicho ni kiwanda,” anasema Kassamia

Mikakati ya taasisi

Pamoja na miradi mingine ya kijamii, mkakati mkubwa uliopo kwa taasisi hiyo ni kuongeza wigo wa maarifa kwa walimu wa shule za msingi kwa kuwapatia elimu kwa njia ya masafa.

Dk Mafumiko anasema walimu wa shule za msingi hasa katika maeneo ya pembezoni mwa nchi wamekuwa kwenye wakati mgumu kupata ruhusa ya kwenda vyuoni kwa ajili ya kuongeza maarifa.

Hilo ndilo linaloisukuma taasisi hiyo kuongeza wigo wa elimu masafa ili walimu wapate maarifa wakiwa katika maeneo yao ya kazi.

Tayari mfumo huo umeshafika katika wilaya za Korogwe, Masasi, Kilosa, Mkuranga na Lindi. Mikoa ya Tabora, Mwanza, Songea, Dodoma, Morogoro na Mbeya nayo imeshanufaika na mfumo huo.

Changamoto

Dk Mafumiko anasema changamoto kubwa ni mtazamo hasi ambao watu wengi wanao kuhusiana na taasisi hiyo, wakiamini kuwa inawahusu wazee pekee.

“Wasichokifahamu ni kuwa elimu ya watu wazima ni eneo pana la elimu linalojumuisha elimu ya msingi, sekondari, elimu ya kujiendeleza, ufundi, elimu ya juu na hata elimu kwa maendeleo ya fani fulani,” anasema.

Pamoja na changamoto hiyo Dk Mafumiko anabainisha kuwa taasisi hiyo itaendelea kuboresha shughuli zake ili iendelee kuwa chachu katika maendeleo ya jamii hasa katika nyanja za kijamii, teknolojia, uchumi na siasa.