TUONGEE UJANA: Dogo Aslay songa mbele wakati ni huu

Saturday November 18 2017

 

Nimekuwa nikisikia lawama mara kadhaa kutoka kwa wafanyakazi, wasanii, wakilalama kuzuiwa kupiga hatua na wale walio juu yao.

Lawama hizi ni kama kujifungia mwenyewe ndani ya boksi. Kulalama kuwa unashindwa kutoka ni kujipangia kushindwa kabla ya kuanza.

Jambo la kwanza na muhimu ni kutambua una kipi unachotakiwa kukifanya ili uweze kusonga mbele, kisha unatafuta namna ya kukiwakilisha.

Katika kukiwakilisha ndiyo unatafuta kazi, unatafuta meneja kama msanii ili asimamie kazi zako au anaweza kukutafuta yeye kulingana na ulichokifanya, hapo utakuwa umepata pa kuanzia.

Ukipata eneo la kuanzia unatakiwa ufanye tofauti na ulichokuwa unafikiri, ili kuonyesha upo tofauti, ikishindikana kufanya hivyo hapo ulipo tambua bado hujafika safari yako na unatakiwa kutafuta namna nyingine ya kuwasilisha ulichonacho.

Ukiendelea kubaki ulipo utakuwa umejifungia ndani ya boksi na utaendelea kuwalalamikia walio juu yako ukidhani wao ndiyo sababu ya mkwamo wako.

Akili yako ianze kufanya kazi kuanzia hapo, usiondoke kwa vibweka wala vurugu, bali jadiliana na aliye juu yako jinsi ambavyo utaweza kufanya ulichonacho kwa kiwango unachoweza badala ya unavyofanya hapo ulipo.

Usikate tamaa haraka, wala usibweteke, kaza buti huku ukingoja au ukiangalia namna bora kwako.

Inawezekana alfajiri yenye mwanga inakuja, kuharakisha kwako kukata tamaa kusikufikishe unapotaka kwenda.

Unapopata nafasi ya kutoka nje ya boksi kwa namna nzuri au mbaya, hakikisha haurudi huko tena na haukati tamaa badala yake unasonga mbele kwa kasi ya kimbunga.

Hiki ndicho alichokifanya mwimbaji Aslay Isihaka, alikuwa kwenye kundi lililopata mafanikio kwa muda mfupi la Yamoto Band likiwa chini ya Said Fella.

Akiwa katika kundi hilo kupitia wimbo wa “Naenda Kusema” ambao ndiyo ulimtambulisha na aliutendea haki, ingawa hakupata nafasi ya kuonyesha kipaji halisi alichonacho.

Hakulalamika na hakukata tamaa, kwa sababu alikuwa anaheshimu taratibu za kundi na huu ndiyo uungwana, hakukimbia kivuli chake, alitambua kinamfuata kila anapokwenda na siku moja atang’aa.

Akiwa katika kundi hili alikuwa na uwezo mkubwa, lakini alishindwa kuwa juu, inawezekana alifichwa na sheria, taratibu na kanuni walizojiwekea kama kundi.

Miongoni mwa vipaji ambavyo hakuweza kuvionyesha akiwa na kundi hilo ni kutunga na kuimba na vyombo (laivu).

Ametoka kwenye kundi hilo na ameonyesha alichonacho, hii ni kwa sababu hajakimbia kivuli chake, hajabweteka, hajamtupia mtu lawama.

Msanii huyu kulingana na kutambua anatakiwa kufanya nini na kuachana na malalamiko, leo ameshika namba moja miongoni mwa wasanii ambao nyimbo zao zinasikilizwa na watu wengi kwenye mtandao wa Youtube, siyo kazi rahisi.

“Kuna watu wanazuia video za nyimbo zangu zisichezwe Youtube kwa kisingizio hazina maadili, wananionea, ninatafuta riziki na sitaacha,” alinukuliwa akisema Aslay tena kwa kujiamini kabisa.

Hapa napo hakulaumu bali alisisitiza hataacha, angerudi nyuma kwa kusema watu wanambania na kulalama na mwisho wa siku angerudi nyuma katika mbio hizo za kutafuta mkate wa kila siku.

Aslay hivi sasa anatamba katika vituo vua redio, runinga na nyimbo kali kama “Likizo”, “Mhudumu”, “Pusha” na “Hatarudi”, huku wimbo “Natamba”, ukiwa ndiyo habari ya mjini.

Aslay umeanzisha mwendo. Nenda na usonge mbele ufanye zaidi ya ulichonacho. Dunia ipo miguuni mwako sasa.

Imetayarishwa na Kalunde Jamal

Advertisement