Tabia tano unazozihitaji ili uishi vizuri na watu kazini

Muktasari:

  • Kama ilivyo mitaani tunakoishi, wapo watu kazini huwezi kuwaridhisha. Unaweza kufanya kila lililo kwenye uwezo wako, lakini bado wakaendelea kukuchukia.

Sehemu kubwa ya maisha ya kazi hutegemea vile unavyoweza kukaa na watu bila migongano.

Unapofanya kazi na watu msioelewana, unajiweka kwenye mazingira yanayoweza kukupunguzia si tu ari ya kufanya kazi, bali hata ufanisi wako.

Kama ilivyo mitaani tunakoishi, wapo watu kazini huwezi kuwaridhisha. Unaweza kufanya kila lililo kwenye uwezo wako, lakini bado wakaendelea kukuchukia.

Hata hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa si mara zote watu hujenga chuki na wewe kwa sababu tu hawakupendi. Wakati mwingine, tabia ulizonazo (bila wewe kujua) zinaweza kuchochea hisia za wivu, uadui na hata mashindano yanayoweza kuathiri mahusiano yako na watu.

Katika makala haya, tunajifunza tabia tano zitakazokusaidia kuwa na uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzako.

Kuwa tayari kuzidiwa

Katika mazingira ya kazi hisia za kuzidiana hazikosekani. Watu huweza kushindana kimyakimya kwa viwango vya elimu; uzoefu; utendaji wa kazi; ushawishi na hata tija waliyoileta kwa kampuni.

Usipokuwa makini unaweza kuingia kwenye mtego wa mashindano haya yanayoweza kuwa chanzo cha misuguano na wafanyakazi wenzako.

Mtu anayeona fahari kushindana na wenzake, mathalani, anaweza kuwa mtu wa kuzungumza sana kwenye vikao. Atashauri mahali ambako ushauri wake haujaombwa ilmradi tu aonekane ni mjuzi wa mambo.

Lakini pia, kwa kuwa anataka kuonekana anawazidi wengine hatakuwa tayari kujifunza kwa wenzake. Haya yote yatamtengenezea ufa wa uhusiano kati yake na wenzake.

Unahitaji kujifunza kuwa mnyenyekevu hata kama kweli inawezekana unawazidi watu. Jijengee mazingira ya kuomba msaada kwa watu wanaokuzidi uzoefu na ujuzi. Fanya hivyo kwa uangalifu bila kuwafanya watu wawe na wasiwasi na uwezo wako.

Sambamba na hilo, usiwe mwepesi wa kushauri kama ushauri wako haujahitajika. Badala yake jenga weledi utakaowafanya watu wakufuate wenyewe kwa ushauri.

Ukiweza kufanya hivyo, watu watakuchukulia kama rafiki asiye mshindani. Utajipunguzia maadui na mapambano yasiyo ya lazima.

Tatua changamoto za wengine

Kila mtu kazini huwa na malengo yake. Inawezekana, kwa mfano, kwa nafasi yako, ukawa na malengo ya kuongeza uzalishaji wa kampuni. Haya ni malengo ya kitaasisi.

Lakini pia unaweza kuwa na malengo yako binafsi kama kupanda cheo. Si jambo baya kuwa na malengo yako kama mfanyakazi anayejitambua.

Unapofanya hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa kila mfanyakazi naye ana malengo yake.

Wakati mwingine malengo yako yanaweza kuingilia na malengo ya mwingine.

Ukitaka kukaa na watu vizuri, jifunze kuongeza thamani yako kwa kufikiria namna unavyoweza kuwasaidia wenzako kufikia malengo yao.

Jambo la kukumbuka ni kuwasaidia wengine kufikia malengo yao, unaweza kujikuta wakati mwingine watu hao wanapata sifa kupitia mgongo wako.

Huna sababu ya kuumia wala kujiona umetumika.

Watu hao mbali na kuwawekea mazingira ya kukulipa fadhila siku nyingine utakapowahitaji, hawatakuwa na sababu ya kushindana na wewe.

Jifunze kuanzia chini

Kwa kawaida watu wanaoanza kazi huwa na matarajio makubwa. Inawezekana ni ndoto za kulipwa mishahara minono itakayobadilisha maisha yako ndani ya muda mfupi.

Ukiacha kipato, kuna mambo ya vyeo. Wafanyakazi wapya hufikiri ni rahisi kukwea ngazi na kupewa madaraka makubwa.

Fikra kuwa unaweza kuanzia juu haraka zinaweza kukuingiza kwenye matatizo yasiyo ya lazima. Kwanza, utakosa uvumilivu wa kufanya kazi chini ya watu wengine kwa kujiona una sifa za kutosha kukupandisha juu kimamlaka. Lakini pia tabia yako inaweza kuonesha papara na kiburi kisicho na sababu.

Unahitaji kuwa mtu wa subira

Jizuie kujipatia sifa za harakaharaka. Ukweli ni kwamba, mafanikio yoyote kazini ni matokeo ya jitihada na bidii zinazoweza kuchukua muda kulipa. Kila aliyefanikiwa leo alianza chini. Ili ufanikiwe unahitaji kuwa na subira.

Kuwa mwaminifu kwa wenzako

Mazingira ya kazi hayakosi watu wanaopenda kueneza habari mbaya. Utakaa na mtu unayemheshimu wakati wa chai kisha ataanzisha mazungumzo yanayomhusu mtu asiyekuwepo kwenye mazungumzo hayo.

Mara nyingi mazungumzo haya huwa na lengo la kuwabomoa wengine. Tabia hii wakati mwingine hulenga kuimarisha makundi ya kimaslahi kazini.

Kwa kawaida, majungu ni kazi ya watu wasio na kazi; watu wasiojiamini au watu wanaolinda maslahi binafsi kwa kubomoa heshima za wengine. Jambo la kuzingatia ni kuwa hao hao unaopiga nao majungu hukosa imani na wewe.

Jenga utaratibu wa kulinda heshima ya wenzako hata wanapokuwa hawapo kwenye mazungumzo.

Unaposikia habari mbaya za mfanyakazi mwenzako, usiwe mwepesi kushabikia. Habari mbaya zilizobomoa heshima ya mwenzako hazikusaidii kuongeza ufanisi wako.

Badala ya kushabikia mazungumzo yanayomharibia mwenzako asiyekuwepo, tafuta jambo jema na liseme kwa ujasiri. Watu wakikufahamu kwa tabia hiyo ya kukwepa kuwa sehemu ya makundi yanayofuga ‘siasa’ za maslahi kazini, utajenga kuaminika kazini. Mbinu chafu zinaposukwa dhidi yako, utakuwa na watu watakaokuwa tayari kukutetea.

Kubali kukosewa na watu

Unajisikiaje unapogundua mtu uliyemheshimu anasuka mpango wa kukuchafua na kukuharibia heshima yako? Je, utafikiria kulipa kisasi au kuachana naye na kuendelea na hamsini zako?

Ofisi hukutanisha watu wenye mawazo na hulka tofauti. Unaweza kujitahidi kuishi vizuri na watu, lakini bado wakawapo watu watakaochukulia wema huo kama sababu ya kukosana na wewe.

Hali hii isikuvunje moyo. Jichukulie kama binadamu anayeweza kuchukiwa bila sababu na mtu yeyote.

Jichukulie kama mtu anayeweza kufanyiwa visa na watu wenye kutumia mbinu chafu kufikia malengo yao. Ukielewa hivyo, hutapata shida unapogundua kuna watu wanakuzunguka.

Kufanya hivyo, hata hivyo, haimaanishi kukubali kuonewa bila sababu.

Hapana. Jenga ukomavu wa kufanya kazi na watu wasiokupenda bila kuathiri kazi zako.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi. http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815