Tafiti ni suluhisho la kisayansi la changamoto tulizonazo

Muktasari:

  • Utafiti wowote unaofanyika kwa kuzingatia misingi ya kisayansi hupata uthibitisho na kuweza kutumika kama rejea mahala popote duniani. Kuna tofauti kati ya utafiti (research) na uchunguzi (investigation).

Utafiti kwa tafsiri ya kawaida ni mchakato wa kisayansi wenye lengo la kuibua jambo jipya lenye kuisaidia jamii au kutafuta njia mbadala ya kutatua changamoto ya aina fulani katika jamii. Utafiti una hatua kadhaa za kupitia ili matokeo yake yaweze kuthibitika kisayansi na hivyo kuwa kweli.

Utafiti wowote unaofanyika kwa kuzingatia misingi ya kisayansi hupata uthibitisho na kuweza kutumika kama rejea mahala popote duniani. Kuna tofauti kati ya utafiti (research) na uchunguzi (investigation).

Uchunguzi hufanyika juu ya jambo au mtu fulani, kwa mfano imetokea ajali, uchuguzi na si utafiti hufanyika ili kubaini chanzo cha ajali.

Serikali yoyote makini, kama ilivyo ya Rais John Magufuli hutumia wataalamu wake kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali kisha kupendekeza mikakati ya kuchukuliwa ili kumaliza au kukabiliana na jambo husika.

Kwa mfano, Serikali ya Marekani mwaka 2007 ilitenga kiasi cha Dola 137 bilioni za Marekani ambazo ni zaidi ya Sh274 bilioni za kitanzania katika eneo la utafiti.

Serikali ya Uingereza katika kipindi cha mwaka 2016/2017 imetenga kiasi cha Euro 4.7 bilioni, zaidi ya Sh11.91 trilioni kwa ajili ya tafiti. Fedha hizi ni nyingi sana, ila pungufu ukilinganisha na matunda ya matokeo ya tafiti zitakazofanyika.

Tanzania ina vituo kadhaa vya utafiti vikiwemo Taasisi ya Taifa ya utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Taaisisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (Tawiri), Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mifugo (Ilri), Taasisi ya utafiti ya Kilimo Naliendele (Nari), kituo cha utafiti wa uchumi na jamii (ESRF).

Pia kuna Taasisi ya Utafiti ya Afya Ifakara (IHI), Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia (Costech) na ile ya kupunguza umaskini (Repoa).

Taasisi au vituo tajwa hapo juu ni kwa kuorodhesha kwa uchache tu, ila vipo vingi kwenye kila sekta. Vituo hivi kwa pamoja vina kazi ya kuhakikisha mtanzania anapata huduma na bidhaa zilizo bora na kwa gharama nafuu.

Tanzania kwa sasa ina takribani vyuo vikuu 50, huko kote kuna wakufunzi ambao wamebobea kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, madini, nishati, maji, kodi, bima, takwimu, miradi, rasilimali watu, sanaa, michezo na ushirika.

Katika mazingira ya kuwa na taasisi nyingi za utafiti, za Serikali na binafsi pamoja na wataalamu waliobobea katika sekta mbalimbali Tanzania ingestahili kufikia uchumi wa kati na kuwa nchi ya viwanda kabla ya mwaka wa lengo 2025.

Ni nchi ambayo viongozi wa kisiasa wasingetakiwa kutumia nguvu nyingi kuyaelekea maendeleo isipokuwa kutumia matokeo ya tafiti zilizofanyika au zitakazofanyika kukabiliana na changamoto husika.

Ni ukweli usiopingika kuwa kufanya utafiti ni gharama, ili kuwa na tafiti zenye ubora na zenye kukidhi matakwa ya kisayansi Serikali haina budi kuziwezesha taasisi hizi kwa kuzipatia zuruku ya uendeshaji ili ziweze kujiendesha na kufanya tafiti kwa maslahi ya watanzania.

Itatuchukua muda mrefu kama nchi kufikia maendeleo mapana ya kitaifa kama tutadharau na kutokuwekeza vya kutosha kwenye tafiti.

Uwekezaji mdogo kwenye tafiti huzalisha tafiti zisizo na tija kwa wananchi.

Kwa dunia ya sasa inahitajika wataalamu wa kilimo wafanye utafiti kubaini mbegu bora za kilimo tunazoweza kutumia kwa miaka 20 ijayo, wahandisi wa madini kwa kutumia tafiti watueleze madini yaliyopo yakiendelea kuchimbwa hivi, yataishi kwa miaka mingapi na zipi njia bora ya kutunza madini yetu.

Tafiti hutumika kubashiri mambo yajayo, kwa miaka mingi mbele na kutoa njia mbadala ya kukabiliana na jambo hilo pindi linapojitokeza. Kwa vyovyote vile kama kweli kunahitaji kuondoa umaskini, maradhi na ujinga, vitu tunavyopambana navyo tangu 1961, ni lazima tuwekeze kwenye tafiti na kutekeleza matokeo ya tafiti.

Badala ya kutumia njia zisizo za kisayansi kushughulikia changamoto zinazowakabili watanzania ni vyema rasilimali fedha zikaelekezwa kwenye taasisi za elimu ya juu na nyingine za utafiti ili zije na majawabu ya matatizo yetu.

Siku za karibuni pamekuwepo na taasisi kadhaa ambazo zinafanya tafiti nyepesi, ambazo kimsingi hazimsaidii mwananchi wa kawaida kuondoka kwenye umaskini, ujinga na maradhi.

Serikali ya Rais Magufuli inaamini kwenye taaluma ndiyo maana viongozi wengi wa kisiasa na kiutendaji waonao hudumu kwenye Serikali ya sasa ni wasomi wa ngazi ya juu.

Ni rai yangu kwa Rais Magufuli kuhakikisha anaziwezesha taasisi za utafiti kutekeleza majukumu ya kufanya utafiti.

Kwa maoni yangu wasomi wa ngazi ya udaktari wa falsafa (Phd) na uprofesa ni watu waliotakiwa kuwekeza zaidi kwenye kufanya tafiti kwa manufaa ya nchi kuliko kutumikia nafasi nyingine. Tafiti kwa maendeleo ya uchumi endelevu.

Mwandishi ni mtakwimu na pfisa mipango.