Tanzania inaweza kujifunza kwa China uzalishaji wa umeme jua

Muktasari:

Wanapaswa kujitokeza wawekezaji wa ndani wa kuzalisha nishati ya umeme jua vijijini ambako ziko fursa nyingi za kutengeneza faida

Sehemu kubwa ya Bara la Afrika imo katika eneo la kitropiki. Tanzania ipo karibu kabisa na mstari wa Ikweta, Ukanda wa Kusini mwa dunia.

Mtaalamu bingwa wa uchumi wa mazingira wa Chuo Kikuu cha Renmin jijini Beijing, China, Profesa Ma Zhong anasema nchi za eneo hili zipo katika mazingira mazuri ya kuwekeza katika kuzalisha nishati ya jua. Hii ni kutokana na kupata jua la utosi kwa kipindi kirefu cha mwaka.

“(Afrika) Mnayo bahati kubwa. Bara lenu linapata mwanga wa jua wa kutosha ambao mionzi yake inaweza kuzalisha umeme kwa mwaka mzima,” anasema Profesa Ma ambaye ni Mkuu wa Shule Kuu ya Mazingira na Maliasili katika Chuo Kikuu cha Renmin.

 

Anasema serikali ya China kwa sasa inapunguza matumizi ya nyukilia katika nishati baada ya kusababisha janga la Fukushima Japan ambao watu kadhaa walipoteza maisha. Badala yake, anasema sasa wamejikita katika vyanzo vikuu vine vya nishati; upepo, jua, taka ngumu na mafuta.

Anasema kwa sasa serikali ya China inaondokana pia na matumizi ya makaa ya mawe kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Profesa Ma ambaye ni mshauri mwandamizi wa serikali na baraza la hifadhi ya mazingira nchini China, anasema kwamba bado hajaridhika na kiwango cha utunzaji wa mazingira nchini humo kwa sababu kilimo ambacho ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa hilo ndicho chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira.

“Tunapata shida kidogo katika kuweka uwiano wa utunzaji wa mazingira na shughuli za kilimo. Hatutaki watu wetu wapate njaa lakini ni lazima pia tuyalinde mazingira yetu,” anasisitiza.

Anasema miaka kadhaa iliyopita hata yeye alijihusisha kwa kiwango kikubwa na shughuli za kilimo na alitumia mbolea na sumu za kuulia wadudu bila kufahamu kwamba alikuwa anachafua mazingira.

Hata hivyo, anasema uwekezaji uliofanywa na serikali yake katika sekta ya nishati kwa sasa umefikia viwango vizuri na pia unazingatia suala la uhifadhi wa mazingira.

Anabainisha kwamba serikali ya China iliamua kubadilisha muundo wa bwawa la umeme katika Mto Yangtze ili lisitumike katika kuzalisha umeme na badala yake litumike kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na samaki.

“Serikali iliomba ushauri kwa wataalamu iwapo samaki aina ya dolphin hawataangamia kutokana na uzalishaji wa umeme na wao wakaihakikishia serikali kwamba hapatakuwepo na madhara yoyote, baadaye ikafahamika kwamba samaki wote wa aina hiyo wamekufa,” anasimulia.

Anasema iligundulika baadaye kwamba kilichowaua samaki hao ni ubaridi uliokuwamo chini ya bwawa hilo kutokana na kujenga kuta za saruji na vilevile msukumo mkubwa wa maji.

Kwa sasa serikali imeunda utaratibu wa kuwatoza kodi kubwa watu wote wanaojihusisha na biashara zinazoathiri mazingira kama vile ukataji wa miti. Lakini wafanyabiashara hao wamekuwa wakipata faida kubwa kiasi kwamba kodi hizo haziwaathiri kwa namna yoyote hivyo wanajipanga upya katika hilo.

Mtaalamu huyo anasema taifa lake linajipanga kutumia taka ngumu katika kuzalisha umeme kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu zaidi ya 1.36 bilioni, kulingana na takwimu za mwaka 2014. Kutokana na kutathmini mazingira serikali ya China imekuwa ikiyasafisha maji yote yatokayo viwandani na kisha kuyarudisha katika mzunguko kwa ajili ya matumzi mengine kama vile kilimo cha umwagiliaji ili kuhifadhi hazina ya maji iliyopo.

Njia nyingine ya uhifadhi wa mazingira ni ujenzi wa mabwawa ya uhifadhi wa maji na ujenzi wa majengo yenye mapaa yanayozalisha umeme wa jua na wakati huohuo kuvuna hazina ya maji na kuyatunza katika matanki maalumu.

“Kwa kuzingatia kilimo kinachotunza mazingira kwa sasa serikali yetu inatosheleza mahitaji ya mchele na viazi kwa taifa isipokuwa tunaagiza maharage ya soya kutoka Marekani, Argentina na kwingineko,” anafafanua.

Anaeleza uchumi wa China inategemea kilimo, uzalishaji wa umeme na utunzaji wa mazingira.

Maendeleo ya nishati China

Jimbo la Hainan Kusini mwa China, kipo kiwanda cha Yingli kinachozalisha nishati ya umeme jua. Pia kuna paneli kubwa zinazotumika katika kiwanda hiki.

Miongoni mwa vivutio vingine kiwandani hapo ni pikipiki zinazotembea kwa kutumia umeme.

Naambiwa kuwa betri hilo linaweza kutumika kwa saa nane, bila kupumzika na iwapo litaishiwa nguvu mhusika atabadilisha na kuchukua jingine kama ambavyo madereva hujaza mafuta kwenye vituo vya maalumu vya petroli au dizeli.

Wenye vituo hujaza umeme tayari kwa yule anayesafiri mwendo mrefu pale anapopatwa na hitaji la aina hiyo.

Lakini pia zipo tochi zinazotumia mionzi ya jua ambazo pia zinatumika nchini Tanzania. Pia yapo magari ambayo paa lake huzalisha umeme unaoweza kutumika kwa kuwasha taa ingawaje bado litahitaji mafuta kwa ajili ya kuwasha injini yake.

China ina teknolojia hizo lakini haipo kwenye mazingira mazuri kama Tanzania ambayo ni nchi ya kitropiki. Hii ni kusema Tanzania na nchi yoyote ya Afrika Mashariki na Kati, inaweza kuiga na kuimarisha uchumi wake hasa maeneo ya vijijini ambako kuna ukosefu mkubwa wa nishati.

Umeme jua ukiwekezwa kikamilifu maeneo ya vijijini unaweza kuharakisha mpango wa usambazaji wa umeme katika maeneo hayo kupitia mradi wa Rea. Kwa kuwa Tanzania imekusudia kuinga kwenye uchumi wa kati wa viwanda ni fursa wawekezaji kujitokeza kutengeneza vifaa mbalimbali vya nyumbani na ofisini vinavyotumia nishati ya jua.

Wanaweza kujitokeza pia watu binafsi wa kuwekeza kwenye nishati ya umeme jua maalumu kwa ajili ya kuchaji betri za pikipiki maeneo ya vijijini na hata mijini. Mpango huu unaweza kuimarisha usafiri wa pikipiki ambao umejijengea umaarufu hapa nchini katika miaka ya karibuni.