Tanzania kinara wa uzalishaji muhogo kiteknolojia Afrika

Muktasari:

Hata hivyo, kwa muda mrefu, wakulima wamekuwa wakishindwa kupata mazao ya kutosha, kutokana na magonjwa, hali ya hewa na uelewa mdogo wa mbinu za kilimo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha muhogo barani Afrika.

Muhogo ni muhimu kwa kinga ya njaa na biashara na pia hutumika kutengeneza chakula cha mifugo malighafi kwa viwanda.

Hata hivyo, kwa muda mrefu, wakulima wamekuwa wakishindwa kupata mazao ya kutosha, kutokana na magonjwa, hali ya hewa na uelewa mdogo wa mbinu za kilimo.

Uzalishaji wa wa zao la muhogo hapa Tanzania upo chini ya kiwango cha kimataifa, kwani wakulima hupata kati ya tani tano hadi saba kwa hekta ukilinganisha na uzalishaji wa kimataifa wa tani 10 kwa hekta.

Utafiti unaonyesha kuwa muhogo unaweza kutoa mazao kuanzia tani 20 hadi 50 kwa ekari kama kanuni za kilimo bora zikifuatwa na wakulima wakatumia mbegu bora za muhogo.

Kwa kuzingatia changamoto hizo, wataalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Mikocheni (Mari), wamefanya tafiti za uzalishaji wa muhogo zilizoleta matokeo mazuri na kusambaza kwa baadhi ya nchi za Afrika.

Mkuu wa kituo hicho na mratibu wa tafiti za bayoteknolojia nchini, Dk Joseph Ndunguru anasema kuna tafiti zilizokamilika na zimeshaonyesha mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi na sasa utafiti wa uzalishaji muhogo kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (GMO), unaendelea.

Swali: Yakoje maendeleo ya utafiti mnaoufanya kuhusu zao la muhogo?

Jibu: Kwanza ieleweke kwamba tafiti hizi zina lengo kubwa la kupambana na magonjwa yanayosumbua zao la muhogo na kuongeza mazao.

Magonjwa makubwa yanayosumbua muhogo ni batobato na michirizi ya kahawia.

Tunachokifanya hapa ni kuzalisha mbegu zisizo na magonjwa na zenye ukinzani wa magonjwa.

Katika utafiti wetu wa kwanza tumesafisha mbegu za muhogo na kuzisambaza katika maeneo ya kanda ya Pwani, kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.

Swali: Mnazisafishaje mbegu?

Jibu: Kinachofanyika ni kuchukua kipande cha mche (tissue) kutoka kwenye shina au tawi kisha tunakiotesha kwenye chupa kikiwa na chakula maalum (media). Baada ya muda kipande hicho huchipua matawi na mizizi.

Baadaye mbegu hiyo huhamishiwa kwenye vitalu maalum kwa uangalifu ili hali ya hewa isije kuviathiri. Vikishamea kwenye udongo, tayari tunakuwa tumepata mbegu safi isiyo na ugonjwa. Njia hii inasaidia kuepuka magonjwa.

Swali: Kwa kuwa uzalishaji wa muhogo nchini umekuwa chini kwa muda mrefu, utafiti huu umeleta mafanikio gani katika uzalishaji?

Jibu: Kwanza umetusaidia kuepuka magonjwa sugu yaliyokuwa yakisumbua wakulima kwa muda mrefu. Pili, uzalishaji wa muhogo umeongezeka kutoka tani tano hadi tani 40 kwa hekta moja. Haya ni mafanikio makubwa katika kupambana na njaa nchini.

Swali: Mnawafikiaje wakulima ili wafaidike na teknolojia hii?

Jibu: Kama nilivyosema tumeshapeleka mbegu tulizosafisha katika kanda ya Pwani, kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini. Huko tuna vikundi vya wakulima vyenye mashamba ya mfano.

Kwa mfano, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, tuna vikundi 16 na kila kikundi kina wakulima 20, ambao tunawapatia mbegu zilizosafishwa.

Tunawaelekeza wakulima kupanda vipande 4,000 vya miti ya muhogo katika ekari moja. Baada ya miezi minane kila mche utatoa mbegu nyingine 20, kwa hiyo kila ekari moja itatoa mbegu 80,000 ambazo watasambaza kwa wakulima wengine.

Tumeziomba halmashauri kutenga bajeti ya kununua mbegu kwa vikundi vya wakulima ili wafaidi teknolojia hiyo.

Kanda ya Ziwa katika wilaya za Rorya na Butiama, tuna mashamba 18 ya kuzalishia mbegu kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima.

Wilaya ya Mbiga (Ruvuma) ilikuwa imeathirika na magonjwa, lakini sasa tuna vikundi 67 vya wakulima vinavyopata mbegu safi.

Swali: Je, katika utafiti huu mmepata uzoefu wowote kutoka nchi nyingine?

Jibu: Tanzania ndiyo tumekuwa chachu ya utafiti wa muhogo Afrika. Tumeshakwenda nchini Rwanda ambako pia tulikuta magonjwa ya muhogo yamewaathiri.

Tumetoa mafunzo ya uzalishaji wa mbegu safi na kuanzisha mashamba ya mfano. Kwa sasa wamepata mafanikio makubwa. Tumeshakwenda pia Zambia, nako tumeanzisha mashamba ya mfano na uzalishaji wa muhogo unaendelea.

Kwa sasa tumealikwa Afrika Magharibi kwenye nchi za Nigeria, Ghana, Benin, Togo na Burkina Faso. Kote huko wameshaona mafanikio yetu nao wanataka kuonja.

Tunashukuru mfuko wa Bill and Melinda Gates pamoja na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) wanaotusaidia katika tafiti zetu.

Swali: Ulitaja awali kuhusu teknolojia ya uhandisi jeni (GMO), hiyo nayo mmefikia wapi?

Jibu: Teknolojia hii ni ya uhakika zaidi kuliko hii ya sasa. Kwa sasa tuko kwenye hatua ya maabara tangu mwaka 2013.

Tunachokifanya ni kuchukua mbegu zilezile za kienyeji ambazo wakulima wanazipenda na kuziainisha kijenetiki. Ni lazima kuzitambulisha mbegu hizo kwa kutofautisha seli zake.

Lengo letu ni kuwashirikisha wakulima kwa kutumia mbegu zao kuliko kutumia mbegu mpya ambazo hawajazizoea; wanaweza kuzikataa.

Baada ya utafiti wa kimaabara unaoweza kutumia miaka mitano, tutaomba kibali cha kuendelea na majaribio shambani.

Lengo letu ni kufikisha tani 21 milioni za muhogo kwa mwaka badala ya tani milioni saba zinazozalishwa kwa mwaka.

Swali: Kuna changamoto gani mnazokumbana nazo katika tafiti hizi?

Jibu: Tatizo kubwa ni idadi kubwa ya wakulima tunaotakiwa kuwafikia ukilinganisha na rasilimali tulizonazo. Ndiyo maana tunaziomba halmashauri zisaidie kuwafikia wakulima.

Hata baada ya kuwawezesha wakulima kuzalisha muhogo kwa wingi, kumekuwa na changamoto ya masoko. Hapa ndipo tunapowaomba wataalamu wa viwanda na masoko waingilie kwa kufundisha jinsi ya kuchakata muhogo ili hatimaye wazalishe unga, biskuti, tambi na bidhaa nyinginezo.