TUJADILI UCHUMI: Tanzania kuelekea uchumi wa kati, maana yake ni nini?

Muktasari:

Azma hii ilielezwa pia katika kampeni za baadhi ya wagombea katika uchaguzi mkuu wa 2015. Kuna uwezekano mkubwa kuwa baadhi ya wadau wakuu wa uchumi wa Tanzania hawaelewi maana ya nchi kuelekea katika uchumi wa kati.

Kati ya malengo makuu ya Tanzania kiuchumi ni kuwa nchi ya uchumi wa kati. Azma hii imeelezwa sehemu mbalimbali kama vile katika Dira ya Maendeleo 2025. Chini ya lengo la kuwa na uchumi imara wenye ushindani.

Azma hii ilielezwa pia katika kampeni za baadhi ya wagombea katika uchaguzi mkuu wa 2015. Kuna uwezekano mkubwa kuwa baadhi ya wadau wakuu wa uchumi wa Tanzania hawaelewi maana ya nchi kuelekea katika uchumi wa kati.

Wadau hawa wanaweza kuwa baadhi ya viongozi wanaotaka ‘kuivusha’ nchi kwenda uchumi wa kati na wananchi ‘watakaovushwa’ kuelekea huko.

Kati ya mambo muhimu ya kufahamu ni maana ya uchumi wa kati kwa maana ya kujua uchumi huu unafananaje, nini kinatakiwa ili kuufikia, tunaufikia kutoka uchumi upi, kuna faida gani kuwa katika ngazi hii ya uchumi na kadhalika. Makala haya inajibu baadhi ya maswali haya.

Uchumi wa kati kutoka wapi?

Inawezekana kuwa baadhi ya wadau hawaelewi tunataka kwenda katika uchumi wa kati kutoka katika uchumi gani. Kwa sasa Tanzania ipo katika uchumi wa chini.

Uchumi huu unazijumuisha nchi zenye kipato cha wastani kwa kila mtu cha Dola za Marekani 1,025 (wastani wa Shilingi 2,194,000) au chini ya hapo kwa mwaka kwa takwimu za mwaka 2015.

Katika orodha ya Benki ya Dunia, kuna nchi 31 katika kundi hili la nchi. Pamoja na Tanzania, nyingine ni kama vile Afghanistan, Burundi, Congo, Ethiopia, Liberia, Malawi, Msumbiji, Nepal, Somalia, Zimabwe, Uganda na kadhalika.

Matabaka ya uchumi wa kati

Katika juhudi za kuelekea uchumi wa kati ni muhimu kwa wadau wote kuelewa huu uchumi ni wa namna gani na nini kinatakiwa kuufikia.

Kwa kadiri ya vigezo vya Benki ya Dunia uchumi wa kati una matabaka mawili makubwa. La kwanza ni lile la uchumi wa kati wa ngazi ya chini na la pili ni uchumi wa kati wa ngazi ya juu.

Hivyo katika ‘kuvushana’ kuelekea uchumi wa kati ni vema ‘watakaotuvusha’ na ‘tutakaovushwa’ kuelewa kama safari ni ya kuelekea uchumi wa kati wa ngazi ya chini au ule wa ngazi ya juu. Maandishi na mazungumzo mengi yanaonyesha Tanzania inataka kuwa uchumi wa kati. Hii haitoshelezi.

Uchumi wa kati ngazi ya chini

Ni muhimu kuweka wazi kuwa maadam tupo katika uchumi wa chini lengo katika awamu ya kwanza linapaswa kuwa kuelekea uchumi wa kati wa ngazi ya chini.

Huu ni uchumi ambapo wastani wa kipato cha kila mtu kwa mwaka ni kati ya Dola za Marekani 1,026 na 4,035, yaani wastani wa kati ya Shilingi 2,195,640 na Shilingi 8,634,900.

Nchi zilizopo katika kundi hili ni 51. Hizi ni pamoja na India, Ghana, Indonesia, Morocco, Sudan, Tunisia, Pakistani, Bangladesh, Kosovo, Lesotho, Misri, Kenya, Nigeria, Zambia, Syria na kadhalika.

Hivyo juhudi za Tanzania za kuelekea katika uchumi wa kati wa ngazi ya chini ni juhudi za kufanana na nchi hizi kiuchumi.

Uchumi wa kati ngazi ya juu

Baada ya kufikia uchumi wa kati wa ngazi ya chini ndipo tunapaswa kuelekea uchumi wa kati wa ngazi ya juu.

Nchi zilizopo katika uchumi wa kati wa ngazi ya juu zinakuwa na wastani wa kipato kwa mwaka kwa kila mtu cha Dola za Marekani 4,036 na 12,475 yaani wastani wa kati ya Shilingi 8,637,040 na Shilingi 26,696,500.

Kwa kadiri ya Benki ya Dunia kuna nchi 55 katika kundi hili. Nchi hizi ni pamoja na Algeria, Angola, Botswana, Brazil, China, Irani, Jamaica, Namibia, Urusi, Afrika Kusini, Cuba, Libya, Iraki, Uturuki na kadhalika.

Hivyo tutakapoanza safari ya kuelekea uchumi wa kati wa ngazi ya juu tutakuwa tunataka kufanana na nchi hizi ikiwemo kila Mtanzania kuwa na kipato cha wastani wa Shilingi 8,637,040 na Shilingi 26,696,500 kwa mwaka yaani wastani wa kati ya Shilingi 719,753 na Shilingi 2,224,708 kwa mwezi. Kwa viwango vingi vya leo, hizi sio fedha kidogo.

Tunafikiaje uchumi wa kati?

Safari ya kuelekea uchumi wa kati kutoka ngazi ya chini ni safari ya kutoka kupata Shilingi 2,194,000 kwa mwaka na kupata Shilingi 2,195,640 hadi Shilingi 8,634,900.

Kitakwimu kinachotakiwa ni kuongeza vipato ili wastani wa sasa uweze kupanda. Ni muhimu kuelewa kuwa wastani unakusanya mapato ya watu wote na kugawanya kwa idadi yao.

Bila shaka wapo wenye vipato vikubwa sana, vya kati na vidogo sana. Ili kufikia wastani wa juu wa vipato inabidi kuongeza vipato kwa kasi kubwa kuliko ongezeko la idadi ya watu.

Hata hivyo kwa uchumi unaojali maslahi ya watu hawa walio na vipato vidogo ni muhimu sana kuongeza vipato vyao sambamba na vile vya wenye vipato vya kati na vya juu.

Kuongeza vipato hasa vya masikini ni muhimu kuongeza na kuimarisha fursa zitakazozalisha ajira.

Nini baada ya uchumi wa kati?

Kufikia uchumi wa kati wa ngazi ya juu sio mwisho wa safari ya kwenda juu katika ngazi za uchumi kwa nchi.

Ngazi inayofuata baada ya kufikia uchumi wa kati wa ngazi ya juu ni ile ya uchumi wa kipato cha juu. Kwa kadiri ya vigezo vya Benki ya Dunia hizi ni nchi ambazo pato la wastani kwa kila mtu kwa mwaka ni kuanzia Dola za Marekani 12,476 yaani Shilingi 26,698,640 na kuendelea kwa mwaka.

Hii ni sawa na Shilingi 2,224,886 kwa mwezi. 12,475. Kwa kadiri ya takwimu za Benki ya Dunia kuna jumla ya nchi 79 katika kundi hili. Hizi ni pamoja na nchi tajiri za Ulaya kama Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Norway, Uholanzi, Ubelgiji, Denmark na nchi nyinginezo za Ulaya.

Nchi za Asia katika kundi hili ni pamoja na Saudi Arabia, Oman, Japan, Kuwait, Falme za Kiarabu na kadhalia. Nyingine ni nchi kama Marekani, Kanada, Australia na kadhalika. Hivyo Tanzania itakapotaka kuwa nchi ya kipato cha juu itakuwa inataka kuwa kama nchi hizi kwa viwango vyao vya leo. Bila shaka ni safari ndefu.

Ni zaidi ya kipato

Katika kuainisha uchumi wa kati ni muhimu kusisitiza kuwa kipato ni mojawapo tuu ya vigezo vinavyotumika. Tabia nyingine za uchumi wa kati ni pamoja na maendeleo ya uchumi na teknologia, miundombinu, maendeleo ya viwanda, elimu, uwekezaji na kadhalika vilivyo juu ya uchumi wa chini lakini chini ya uchumi wa kipato cha juu.

Hivyo ni muhimu kwa wadau wote kuelewa njozi za kuelekea uchumi wa kati maana yake ni nini na tunatoka na kwenda wapi. Haya yasipofahamika tutakuwa tunasafiri kutoka na kwenda tusikopafahamu.

Mwandishi wa makala haya ni Profesa wa Uchumi, Mtafiti na Mshauri Elekezi Katika Uchumi na Biashara Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar Es Salaam