Tanzania tutaendelea kutoenzi vipaji mpaka lini?

Marehemu Dk Anna Claudia Senkoro enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Dk Anna Claudia Senkoro, mwanamke wa kwanza kujitokeza na kugombea nafasi ya urais katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefariki dunia Januari 4, 2017.
  • Katika hali ya kushangaza, Senkoro amezikwa kama raia wa kawaida bila hata mbwembwe zilizozoeleka kwa wanasiasa waliofikia hata katika ngazi ya ubunge kama tulivyowahi kushuhudia mazishi ya viongozi wengine wa kisiasa nchini.

Kumetokea jambo katika siku za karibuni ambalo halikupata kuripotiwa katika vyombo vya habari kwa kiwango ambacho lilistahili.

Dk Anna Claudia Senkoro, mwanamke wa kwanza kujitokeza na kugombea nafasi ya urais katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefariki dunia Januari 4, 2017.

Katika hali ya kushangaza, Senkoro amezikwa kama raia wa kawaida bila hata mbwembwe zilizozoeleka kwa wanasiasa waliofikia hata katika ngazi ya ubunge kama tulivyowahi kushuhudia mazishi ya viongozi wengine wa kisiasa nchini.

Ingawa mimi siyo shabiki wa mazishi ya kifahari, namna ambavyo mwanasiasa huyu alipata nafasi ndogo katika vichwa vya habari mbalimbali imenifanya nitafakari maisha ya kisiasa katika nchi yetu na barani Afrika.

Senkoro alijitokeza kwa mara ya kwanza kugombea urais mwaka 2005 katika uchaguzi ambao ulikuwa na hamasa kubwa. Aligombea kupitia Chama cha Progressive Party of Tanzania (PPT–Maendeleo) kilichokuwa kikiongozwa na Peter Mziray wakati huo.

Dk Senkoro alipambana katika uchaguzi mgumu kiasi cha kusafiri kote nchini akijinadi katika mazingira ambayo alitumia mpaka rasilimali zake mwenyewe.

Hadi kufikia uchaguzi, Senkoro aliweza kuvuna kura 18,783 sawa na asilimia 0.17 ya kura zote huku wagombea wenzake wakivuna kura kama inavyoonyeshwa katika mabano, Jakaya Kikwete (milioni 9.12); Profesa Ibrahim Lipumba (milioni 1.3); Freeman Mbowe (668,756); Augustino Mrema wa TLP (84,901).

Wengine ni Dk Sengondo Mvungi wa NCCR–Mageuzi (55,819); Mchungaji Christopher Mtikila wa DP (31,083); Dk. Emmanuel Makaidi wa NLD (21,574); Profesa Leonard Shayo wa Makini (17,070) na Paul Kyara wa Sau aliyepata kura 16,414.

Katika wagombea hao wote wa mwaka 2005, wanne walikwisha kufariki dunia kabla ya Dk Senkoro. Mchungaji Mtikila aliyefariki dunia kwa ajali ya gari kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015; Dk Mvungi aliuawa na majambazi waliomvamia nyumbani kwake katikati ya mchakato wa Katiba Mpya Novemba 2013.

Dk Emmanuel Makaidi alifariki dunia ndani ya siku 10 kabla ya siku ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka jana na kufanya uchaguzi katika jimbo la Masasi alilokuwa akigombea ubunge kuahirishwa.

Majimbo mengine yaliyoahirisha uchaguzi kutokana na vifo mwaka 2015 yalikuwa ni Lushoto (Mohamed Mtoi, Chadema); Handeni Mjini (Dk Abdallah Kigoda, CCM); Ulanga Mashariki (Celina Kombani, CCM) na Arusha Mjini (Estomih Malla, ACT).

Kifo cha Dk Makaidi kilifanya idadi ya wagombea ngazi ya ubunge waliofariki dunia dakika za mwisho za uchaguzi kufikia watano.

Kuhusu uanachama katika vyama vya siasa, Dk Senkoro alikuwa na bahati ya kukubalika na vyama vingi kuanzia CCM na vya ushindani.

Katika muda mfupi alioamua kuwa mwanasiasa motomoto, Dk Senkoro aliweza kuhama kutoka CCM alikolelewa kwa miaka mingi tangu kuzaliwa kwake 1962 na kutumikia PPT Maendeleo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Desemba 14, 2005, kabla ya kujiengua na kurejea CCM baadaye mwaka 2006.

Kurejea kwake CCM kulimwezesha kupata hisani ya matibabu nchini na nje ya nchi kabla ya afya yake kudhoofu kutokana na kampeni ngumu na ndefu za urais kutengemaa. Baadaye, Senkoro ambaye kitaaluma alikuwa daktari mtabibu na mama wa watoto watatu, alijiunga na Chamac Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika harakati za mafuriko mwishoni mwa mwaka 2015 na kubakia hivyo mpaka mauti yalipomfika.

Katika tafakari yangu, Dk Senkoro siyo mtu wa kawaida. Ni mwanamke wa shoka, aliyesoma na kutumikia Taifa kama tabibu na baadaye akaamua kuvunja ukimya kwa kujitosa katika siasa na kugombea nafasi ya juu kabisa ya utumishi nchini yaani urais.

Endapo angeshinda, Dk Senkoro angekuwa Rais, Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini kwetu. Aidha, Dk Senkoro angekuwa Rais Mwanamke Afrika wakati ambao wengi walikuwa hata hawajafikiria.

Kwa sababu hiyo, namwona Dk Senkoro kama nyota na taa ya siasa za kuelekea usawa wa Kijinsia Afrika, ambaye alifaa siyo tu kuwa mfano wa vijana wa kike na wa kiume wanaochipukia katika siasa, bali alipaswa kuenziwa na kuigwa kwa kuonyesha mfano wa kuingia katika anga ambazo wakati huo zilionekana kuwa za wanaume zaidi.

Ndiyo maana naona ni fedheha kwa nchi yetu kushindwa kumpa heshima aliyostahili kama mama wa siasa za mageuzi katika kiwango ambacho wanawake waliomtangulia kama akina Bibi Titi Mohammed, Sophia Kawawa na wengineo walienziwa.

Juu ya nini cha kufanya, ninaona kuwa ni lazima tujifunze kuenzi Waafrika walio wa mfano bora. Kwa masikitiko, watu wengi nchini wamefanya vitu vizuri, lakini wameishia kujilaumu baadaye walipotelekezwa na kuishia kukosa hata pesa ya kununua vidonge vya kutuliza maumivu ya kichwa.

Kinyume chake, tunaweza kuweka utaratibu wa kuwaheshimu, kuwaenzi na kuwatuza tuzo maalumu watu waliochangia katika ‘ukombozi’ wa nchi yetu kwa namna yoyote ile na kupitia taasisi yoyote ile iwayo.

Nionavyo, Dk Senkoro anapaswa kuingia katika kumbukumbu za wanawake mashujaa wa nchi yetu ambao wamekufa wakitafuta haki.

Deus Kibamba ni mtafiti, mhadhiri na mchambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa na demokrasia ya Katiba. Anapatikana kwa: Simu +255 788 758 581 au email: [email protected]