Tarehe ya uchaguzi DRC na zawadi ya Krismas mwakani

Mwakani tumtarajie “Father Christmas (Santa Claus)”. Mjini Kinshasa wiki iliyopita Tume ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ilitangaza kwamba Desemba 23, 2018, siku mbili kabla ya Krismasi itakuwa siku ya kumchagua Rais mpya wa nchi hiyo na pia mabunge mapya ya mikoa.

Kwa hakika, vipindi vya utawala wa Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo pamoja na Bunge la Taifa vilimalizika tangu Desemba 2016. Kipindi cha mabunge ya mikoa kilimalizika miaka kabla. Lakini DRC haijaweza kuandaa chaguzi mpya kwa wakati. Kabila aliendelea kutawala. Baada ya kufanyika maandamano makubwa ya wananchi yaliosababisha damu kumwagika, upinzani, chini ya upatanishi wa Kanisa Katholiki la nchi hiyo, ulikubali chaguzi hizo zifanywe mwisho wa mwaka 2017.

Sasa Tume ya uchaguzi imeamua chaguzi hizo zifanywe si kabla ya mwisho wa mwakani 2018. Yaonyesha tume hiyo ya uchaguzi sasa imegundua njia ya kupata fedha za kuandaa chaguzi hizo kwa wakati huo. Kazi kubwa ni kuwaandikisha upya wananchi katika daftari la wapiga kura. Daftari la sasa la tangu mwaka 2006 ni kongwe mno, halifai.

Wengi wa watu waliomo ndani yake huenda wameshaaga dunia, na kuna watu wengi ambao sasa wameshafikia umri wa kuwa na haki ya kupiga kura - miaka 18 - hivyo wanahitaji kuingizwa katika daftari jipya.

Na endapo makamishna wa uchaguzi watabeba kutoka mkoa mmoja hadi mwingine vifaa vya kuwaandikisha na kuwapiga picha wapiga kura, basi zoezi hilo litachukua miaka. Tena hasa katika nchi kubwa na iliyo na wakazi milioni 80 kama ilivyo DRC. Pia nchi hiyo ina miundombinu mibovu kabisa. Wakati watu wote hao watakapomalizika kuandikishwa daftari hilo litakuwa tayari limeshapitwa na wakati.

Uandikishaji mpya wa wapiga kura ulianza Agosti 2016. Kwa mujibu wa Tume umeshakamilika katika mikoa 13 kati ya 26, katika mikoa mingine 11 karibu utamalizika, na katika mikoa miwili bado unaendelea - yaani katika Mikoa ya Kasai na kasai ya Kati iliyokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Huko uandikishaji ulianza Septemba 12, mwaka huu.

Kwamba Tume imeamua wakati wa uchaguzi uwe angalau mwisho wa mwaka 2018 ni jambo lililotarajiwa. Kwa njia hiyo ina maana daftari la wapiga kura litakuwa na kila jina la Mkongomani ambaye amezaliwa hadi mwisho wa mwaka 2000, yaani yeyote atakayetimiza umri wa miaka 18 hadi wakati wa kufanyika uchaguzi.

Mwezi Oktoba mwaka huu tume hiyo iliarifu kwamba baada ya kumalizika kipindi cha kuwaandikisha wapiga kura, itahitaji angalau zipite siku 504 hadi tarehe ya kufanya uchaguzi. Hiyo inamaanisha wakati wowote katika mwaka 2019, na huenda hata baada ya hapo.

Kwamba sasa imeamuliwa chaguzi hizo zifanywe mwisho wa mwaka 2018- jambo hilo ni la kushukuriwa, linatokana na mbinyo wa kimataifa.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, alitangaza kabla ya wiki iliyopita mjini Kinshasa kwamba chaguzi hizo lazima zifanywe mwaka 2018, ama sivyo hakutatolewa misaada kwa zoezi hilo kufanyika baadaye. Sasa Tume imebadili dira na inasema pindi chaguzi zitabidi zifanywe mwaka 2018, basi jamii ya kimataifa itabidi ilipie gharama.

Mkuu wa Tume, Corneille Nangaa Jumapili iliyopita alionya kwamba ratiba yake itafanya kazi kama hakutazuka matatizo ya kisheria, kiusafiri, kifedha au kisiasa. Lakini kila mtu anatambua kwamba katika Congo hakukosekani kuzuka matatizo ya kisheria, kiusafiri, kifedha na kisiasa.

Kwa hivyo, waangalizi wengi wa mambo ya siasa wanahisi kwamba hiyo Desemba 23, 2018 iliyowekwa kama siku ya kupiga kura katika chaguzi hizo haijakusudiwa kikweli. Itakuwa ajabu kama tarehe hiyo itaheshimiwa.

Vizingiti na visiki vya mwanzo tayari viko mbele, vimeshachomoza. Hadi mwisho wa mwezi huu wa Novemba Bunge linatakiwa lipitishe sheria mpya ya uchaguzi. Pia Serikali na wafadhili watahitaji waafikiane kuhusu namna ya kuzigharamia chaguzi hizo. Hayo si mambo rahisi.

Kwa mujibu wa ratiba uandikishaji wapiga kura utamalizika mwisho wa Januari 2018. Baada ya kuwekwa hadharani daftari la wapiga kura lililopitiwa, mnamo wiki mbili majimbo ya uchaguzi yanatakiwa yawe yameshakatwa na kujulikana mipaka yake. Huo ni muda mfupi sana. Pale mambo yote hayo yatakapomalizika, baina ya Julai na Septemba Wakongomani wote walioko ughaibuni “wataandikishwa” kama wapiga kura. Hilo ni jambo jingine litakalozusha mabishano.

Kwa mujibu wa upinzani, mambo yote hayo yatafanyika kwa njia isiyokuwa ya kisheria: Kipindi cha utawala wa Kabila kimemalizika zamani. Hivi sasa yeye ni rais wa kujishikiza hadi ilivyopangwa hapo kabla kwamba aache madaraka mwisho wa mwaka huu wa 2017.

Tamko hilo limetolewa na Muungano wa Upinzani na umewataka wananchi wafanye maandamano. Lakini dai linalotaka iwekwe madarakani Serikali ya mpito badala hii ya sasa ya Kabila halijaungwa mkono na vyama vingine vya siasa. Pia vyama hivyo havijakubaliana kama viwache kuendelea kufanya kazi ndani ya Tume ya Uchaguzi.

Kikundi cha vijana ambacho ni cha siasa kali kinachoitwa Lucha (Mapambano ya kutaka Mabadiliko) kimeielezea kalenda hiyo ya uchaguzi kutoka Tume kuwa ni “Tangazo la Vita” dhidi ya wananchi na kikatoa mwito ufanywe uasi ambao utaliingiza pia jeshi.

Kimetaka yaitishwe maandamano nchi nzima na kutaka Novemba 28 - siku ya kuukumbuka uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2011- vianze vitendo vya kuweka vizuizi nchi nzima ili kumlazimisha Kabila aondoke madarakani. Jumatatu iliyopita maduka kadhaa katika Kinshasa yalifungwa kwa kuhofia kutokea vurugu.

Mwisho wa mwezi uliopita kulitokea machafuko katika mji wa Goma, mashariki ya nchi hiyo, ambapo inasemekana raia watatu hadi wanne waliuawa pamoja pia na polisi mmoja. Hali hiyo ilitokea pale waandamanaji kutoka upinzani katika saa za alfajiri waliweka vizuizi barabarani na kuvitia moto vizuizi vilivyowekwa na polisi.

Polisi waliwazuia kwa nguvu waandamanaji hao katika mji huo wa watu milioni moja. Polisi mmoja aliuawa kwa kupigwa mawe ya madongo yanayotokea mlima wa volkano karibu na Goma. Polisi ilisema watu waliomshambulia polisi huyo si waandamanaji wa kawaida bali ni maharamia waliokuwa na mapanga, mawe na visu.

Kikundi cha vijana cha Lucha kiliitenga Oktoba 30 kuwa siku ya mgomo mkuu wa nchi nzima katika Congo. Lengo ni kuuendeleza mbinyo kutaka Rais Kabila ajiuzulu angalau hadi mwisho wa mwaka huu. Lucha ilisema maandamano hayo yalifanikiwa na yatafuatwa na mengine katika miji mingine. Kilisema kwamba Kabila itambidi awaue Wakongomani milioni 80 ili abakie madarakani.

Alipokuwa katika ziara yake ya Congo, mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley alifika Goma na huko alikutana pia na wanaharakati wa Lucha. Wanaharakati hao walibeba mabango mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa katika mji huo, yalioandikwa: “ Miaka 17 ya utawala wa Kabila ni miaka 17 ya shida kubwa.” Walitaka iundwe serikali ya mpito huko Congo kuanzia mwisho wa mwaka huu wa 2017 bila ya Kabila.

Vitisho vya Upinzani vinaelekea kuipeleka Congo katika njia ya hatari na si vyenye dhamana, hasa kwa vile sasa kuna tamaa ya kufanyika uchaguzi huko Congo, angalau mwisho wa Desemba mwakani. Kuufanya uchaguzi kabla ya hapo, bila ya matayarisho ya kutosha, tena katika nchi kubwa kama Congo isiyokuwa na miundombinu ya maana, ni kukaribisha fujo na vurugu zaidi kuliko zile zilioko sasa.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inahitaji kupumua kwa kila hali, imeugua vya kutosha. Miito ya kutaka kumwaga damu zaidi kutoka upande wowote ule isikubaliwe hata kidogo. Kila tone moja la damu ya Mkongomani lina thamani. Kuna ubaya gani zaidi kuungojea uchaguzi mpya utakaofanywa kwa haki na njia huru mwisho wa mwaka 2018, jambo lililoahidiwa na Tume ya uchaguzi? Na hasa kwa vile Joseph kabila hatakuwa mgombea tena?