Tatizo Stars hili hapa

Monday October 30 2017

 

By Charles Abel,Mwananchi [email protected]

Katika siku za hivi karibuni, timu ya taifa, ‘Taifa Stars’ chini ya kocha Salum Mayanga, haichezi katika kiwango cha kuridhisha kwenye mechi inazocheza za mashindano mbalimbali.

Matokeo ya Stars yamekuwa yakiwasononesha Watanzania, baada ya kushindwa kupata ushindi au kucheza katika kiwango kinachotakiwa katika mechi za kimataifa.

Pamoja na Stars kupoteza mchezo mmoja, kushinda mechi saba na kutoka sare mara saba tangu Mayanga apewe jukumu la kuinoa, presha kubwa imekuwa ikielekezwa kwake.

Mayanga amekuwa akipata shinikizo la kutakiwa kujiuzulu kwa kile kinachodaiwa kiwango cha Stars hakitoi dalili njema ya kufanya vizuri katika mashindano itakayoshiriki siku za usoni.

Kumekuwa na sababu mbalimbali zinazotajwa kama chanzo cha Stars kuyumba licha ya kubadilisha makocha kwa nyakati tofauti bila mafanikio.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa chanzo cha Stars kuvurunda ni kukosekana uti wa mgongo wa timu (muungano wa kikosi).

Muungano unaotajwa unaundwa na kipa, beki namba tano, viungo wawili (namba sita, nane) na washambuliaji wawili wanaocheza namba tisa na kumi.

Timu yoyote duniani inapokuwa na muungano mzuri wa wachezaji bora wanaocheza katika nafasi hizo ni chachu ya kufanya vyema katika mechi zao tofauti na Stars.

Taifa Stars inaundwa na wachezaji wasiokuwa na muunganiko mzuri kwa kuwa wanacheza timu tofauti wakiwa hawajawahi kucheza pamoja muda mrefu.

Wachezaji wanaojenga uti wa mgongo Stars ni kipa Aishi Manula

kutoka Simba, beki Abdi Banda (Baroka, Afrika Kusini), Hamisi

Abdallah (Sony Sugar, Kenya) Himidi Mao (Azam FC), Mzamiru

Yassin (Simba) na Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).

Kumbukumbu zinaonyesha Stars inayotajwa kuwa bora ilikuwa chini ya kocha Kim Poulsen, ikiwa na muungano mzuri wa wachezaji waliozoeana muda mrefu.

Kipa alikuwa Juma Kaseja, beki namba tano Kelvin Yondani, waliocheza muda mrefu katika kikosi cha Simba kabla ya libero huyo kuhamia Yanga huku akiendeleza makali yake na kuaminiwa kuwa ni kati ya wachezaji mkoba makini.

Kiungo namba sita alikuwa Frank Domayo aliyekuwa akicheza na Yondani kikosi cha Yanga na sasa yuko Azam wakati kiungo namba nane alikuwa Abubakar Salum ‘Sure Boy’ ambaye bado yuko Azam.

Itakumbukwa ‘Sure Boy’ na Samatta aliyekuwa akicheza namba tisa, walicheza timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ iliyokuwa chini ya Poulsen.

Hii inamaanisha kati ya wachezaji watano waliounda uti wa mgongo Stars, watatu walizoeana kabla ya kuwemo katika kikosi hicho ambao ni Domayo, ‘Sure Boy’ na Samatta.

Mfano mwingine upo kwa timu ya taifa ya Hispania ilipotwaa Kombe la Ulaya mwaka 2008 ilikuwa na muungano mzuri kwa asilimia 80 ya wachezaji kutoka Barcelona.

Kipa alikuwa Iker Casillas wa Real Madrid, namba tano (Carles Puyor, Barcelona), namba sita Sergio Busquets (Barcelona), namba nane (Xavi Hernandez, Barcelona). Namba tisa kivuli alitumika Cesc Fabregas aliyekulia Barcelona.

Kocha na mchambuzi wa soka, Joseph Kanakamfumu aliunga mkono uchunguzi wa gazeti hili huku akitaja sababu mbili zilizochangia Stars kukosa uti wa mgongo.

“Kwanza hakuna muendelezo mzuri wa viwango kwa wachezaji wetu. Leo mchezaji anaweza kufanya vizuri kesho akacheza vibaya, jambo linalofanya makocha wa klabu au timu ya taifa

kufanya mabadiliko ya vikosi vyao na kusababisha kuanza upya kila siku kutengeneza timu.

“Lakini kingine ni timu zetu kubwa ambazo zinategemewa kuzalisha wachezaji wa Stars, kujaza na kuwatumia wachezaji wa kigeni jambo linaloipa wakati mgumu timu ya taifa kwa sababu inalazimika kutumia wachezaji wanaopata nafasi katika timu tofauti hatua inayochangia kutokuwepo muunganiko mzuri.

Kanakamfumu alisema rekodi zinaonyesha katika miaka ambayo Stars ilifanya vyema idadi kubwa ya wachezaji walitoka klabu moja.

Alidokeza mwaka 1993 Stars ilipotwaa Kombe la Chalenji, wachezaji wengi walitoka Simba iliyokuwa katika ubora na 1998 ilipofanya vyema katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia Yanga ilitoa nyota wengi.

Kocha John Tegete alisema ili Stars iondokane na tatizo hilo ni vyema kuacha mfumo wa kutegemea wachezaji kutoka Simba, Yanga na Azam FC.

“Timu ya taifa inaonekana ya Dar es Salaam kwa sababu inajaza wachezaji wengi wa klabu hizo zinazojiita kubwa hata kama uwezo wao ni mdogo, wachezaji wazuri wanaachwa katika timu za mikoani,” alisema Tegete.

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), klabu moja inaruhusiwa kusajili wachezaji saba wa kigeni, lakini wanaotakiwa kucheza katika mchezo mmoja ni watano.

Bila shaka TFF inatakiwa kuangalia upya utaratibu wa klabu moja kusajili wachezaji wachache wa kigeni ili kutoa fursa kwa wazawa kupata nafasi katika klabu zao hatua inayoweza kuimarisha timu za taifa.

Taifa Stars kwa sasa inajiandaa na mchezo na Benin utakaofanyika Novemba 11 ikiwa ni pambano lililo ndai ya kalenda ya shirikisho la soka la kimataifa, Fifa.

Advertisement