Teknolojia itachukua ajira zetu tukitaka itatutengenezea

Muktasari:

  • Tumesikia wenzetu Rwanda kuwa kompyuta mpakato wanazotumia hivi sasa wametengeneza wenyewe. Sisi je?

Inawezekana ni mimi peke yangu sijasikia juhudi za Serikali kutengeneza mazingira mazuri ya ajira pale tutakapofika katika ulimwengu ambao kila kitu kitaendesha na mashine.

Miaka miwili iliyopita nilisikia majirani zetu Kenya kuwa wanatengeneza kijiji cha teknolojia kwaajili ya kujiandaa na dunia mpya ya teknolojia.

Tumesikia wenzetu Rwanda kuwa kompyuta mpakato wanazotumia hivi sasa wametengeneza wenyewe. Sisi je? Teknolojia zinachukua ajira za watu si utani. Nakumbuka takribani miaka nane iliyopita wakati najiunga na kampuni hii kulikuwa na wafanyakazi wengi…chumba cha habari kilikuwa kimesheheni watu haswa.

Ni kama nusu ya watu hao hawapo kazini lakini gazeti linatoka tena katika ubora wa hali ya juu. Nafasi nyingi zimechukuliwa na teknolojia kuanzia uandishi mpaka upangaji wa kurasa. Huko kwenye ushapishaji ndio sitaki kusema.

Walioanza uandishi miaka hiyo wanafahamu jinsi mlolongo ulivyokuwa mrefu wa kutoa gazeti. Habari ziliandikwa kwenye karatasi, kisha zikachapwa katika type writer na kuendelea mpaka kutua kwenye karatasi la gazeti.

Sasa hizi siyo lazima hata kuandika kwenye komputa, mwandishi popote alipoa anaandika katika simu yake ya mkononi na kuipeleka moja kwa moja chumba cha habari.

Ni watu wangapi hapa  wamepoteza kazi? Wengi sana bila shaka kwa kuwa mashine zimechukua nafasi zao. Kazi iliyokuwa ikifanywa na watu wanne sasa inafanya na mmoja. Lakini tujiulize ni kwa vipi teknolojia zinachukua kazi zetu ndipo tutapata suluhu za kutengeneza ajira nyingine.

Mimi najua teknolojia inachukua ajira zetu kwa kuzirahisisha. Yaani siyo kwamba ile kazi inaondoka, lah inarahisishwa na mashine.

Kwa hiyo kumbe ukiamua kutafuta suluhu za matatizo tuiliyonayo unaweza kujitengenezea ajira kwa kubuni teknolojia fulani.

Kwa mfano kuna mashamba ambayo yanalimwa na matrekta yanayoendeshwa na mashine siyo watu. Maana yake kilimo kipo na kitaendelea kuwepo isipokuwa kitakachotoa ajira ni kubuni teknolojia ambazo zitatengeneza ajira zetu miaka 20 ijayo. Ajira zetu miaka 20 zitakuwepo kama tutaamka kubuni teknolojia zetu wenyewe kurahisisha matatizo yetu. Ubunifu huu utatuajiri na kutututengenezea kipato cha uhakika baadaye.

Tukisubiri tutaletewa teknolojia na utaalamu kutoka ‘majuu’. Tutaajiri wataalamu kutoka majuu kwa kuwa wao ndio watakuwa wanazifahamu.