KUZA FURSA : Tengeneza mabalozi wa biashara yako ufanikiwe

Muktasari:

  • Kuwa na balozi wa biashara ni moja ya njia za kupata wateja na kukuza soko hatimaye kuongeza faida. Balozi wa biashara ni mtu ambaye anatumika kununua bidhaa kwa bei nafuu ili aitangaze kwa wengine au ni mtu ambaye kwa hadhi au umaarufu wake analipwa na kampuni fulani ili aitangaze kampuni husika kwa muda maalumu.

Dhana biashara ni pana na inahitaji mfanyabiashara kujitahidi kusoma na kupata ushauri kwa nyakati mbalimbali ili kuendelea kupata faida na kuendelea kufanya vizuri sokoni.

Kuwa na balozi wa biashara ni moja ya njia za kupata wateja na kukuza soko hatimaye kuongeza faida. Balozi wa biashara ni mtu ambaye anatumika kununua bidhaa kwa bei nafuu ili aitangaze kwa wengine au ni mtu ambaye kwa hadhi au umaarufu wake analipwa na kampuni fulani ili aitangaze kampuni husika kwa muda maalumu.

Balozi anaweza kuwa wa bidhaa au kampuni bila kujali ndani ya kampuni kuna aina ngapi za bidhaa. Mabalozi wanaweza kuwa wengi kwa bidhaa fulani kutegemea malengo ya kampuni husika. Kuna aina nyingi ya mabalozi wa biashara, hapa tunazungumzia aina tatu ambazo kwa mazingira yetu inawezekana kuwa nao kwa urahisi.

Aina ya kwanza ni balozi wa biashara anayepata punguzo la bei za bidhaa kutoka kwa kampuni au mfanyabiashara. Balozi huyu sifa yake ni kuwa mtumiaji wa mara kwa mara wa bidhaa hizo, ndiyo maana msingi wake ni kupata punguzo la bei. Anapewa punguzo la bei kwa lengo la kuwa balozi wa bidhaa au kampuni kwa kufanya kazi ya kushawishi wenzake kununua bidhaa hizo. Punguzo linatumika kama malipo ya kazi ya kushawishi watu kununua bidhaa ili kampuni ipate kuuza kwa wingi na kupata faida.

Aina ya pili ni balozi asiyemteja wa bidhaa ila umaarufu wake au hadhi yake njema katika jamii. Balozi huyu hulipwa fedha na kampuni kwa kukubali na kuna makubaliano yanaingiwa ili afanye baadhi ya kazi ambazo zitasababisha kampuni kuongeza mauzo au kuwa na sifa nzuri kwa jamii.

Miongoni mwa kazi ambazo balozi huyu hutakiwa kufanya kwa makubaliano inajumuisha kuvaa fulana na kofia za kampuni, kuizungumzia kwa uzuri kampuni na bidhaa zake popote atakapokuwa na kuandika uzuri wa kampuni na bidhaa katika mitandao ya jamii na kushea na marafiki alionao.

Aina ya tatu ni balozi anayelipwa na kushiriki matukio muhimu ya kampuni. Balozi huyu haitajiki kuwa maarufu au kuwa na hadhi katika jamii. Huyu hutengenezwa kwa kuchaguliwa kutokana na vigezo vitakavyowekwa na kampuni.

Atafanya kazi zote za balozi wa aina ya pili ila huyu atapewa mafunzo maalumu ya namna ya kufanya kazi zake kama balozi. Pia, atashiriki kwa vitendo katika maonyesho ya biashara, promosheni za barabarani na matukio ya biashara ya kampuni.

Biashara za aina zote na zenye ukubwa tofauti zinahitaji mabalozi kama njia mojawapo ya kuongeza wateja na mauzo ili kupata faida na kukua kibiashara. Kila biashara itatengeneza mabalozi wake kwa mujibu wa uwezo wake na aina ya bidhaa na wateja walionao.

Hivyo hakuna haja ya kujiuliza au kuliacha suala hilo kwa kampuni kubwa pekee kama mazoea yalivyo nchini. Bila kujali ukubwa wa mtaji au soko biashara husika inalouza bidhaa zake, mabalozi ni muhimu.

Kuna faida nyingi za uwapo wa mabalozi wa biashara katika biashara zetu. Miongoni mwa faida hizo ni kuongeza mauzo, kuongeza faida, kukuza jina la biashara ili lifahamike kwa watu wengi zaidi, kukuza biashara na kupanuka na kuwa na uhakika wa soko la bidhaa.

Tuone mifano ya mabalozi gani wa biashara wananaweza kufaa katika biashara ya mama nitilie. Mfano huu ni katika biashara ndogo sana, ambayo kwa dhana ya kawaida inaonekana kama haiwezi kuwa na mabalozi wa biashara.

Tumeshuhudia bodaboda na madereva wa daladala wanavyochukua nafasi kubwa ya kupata mlo kwa kina mama na baba ntilie. Ni elimu ndogo tu inahitajika ya kuona bodaboda gani ana ushawishi kwa wenzake. Ukimpata huyo unaongea naye kwa kumpa punguzo la bei ya chakula kwa kila siku akija na wenzake watano na zaidi. Hali hii itamhakikishia mama ntilie huyu kuuza kila siku na kupata faida. Vivyo hivyo kwa madereva daladala.